Naibu Waziri wa Ardhi,Nyumba na Maendeleo ya Makazi Bwana Ridhiwani Kikwete akizungumza wakati wa kikao kazi cha Wenyeviti wa Mabaraza ya Ardhi na Nyumba ngazi ya Wilaya uliofanyika mkoani Tanga.
Katika Mkutano huo, Naibu Waziri Ridhiwani alisisitiza Uadilifu miongoni mwa wenyeviti hao kwani ndiyo msingi utakaoleta haki na kumaliza mashauri yanayopelekwa Kwenye Mabaraza ya Ardhi na Nyumba ya Wilaya.
Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii, Dkt. Allan Kijazi akizungumza wakati wa mkutano huo wa wenyeviti wa Mabaraza ya Ardhi na Nyumba ngazi ya Wilaya Nchini uliofanyika jijini Tanga.
Kijazi alisema, Wizara itaanza kuweka mfumo wa ufuatiliaji utendaji kazi wa wenyeviti wa mabaraza ya ardhi kwa lengo la kuboresha utendaji kazi.
Msajili wa Mabaraza ya Ardhi na Nyumba ya Wilaya nchini, Stella Tullo akizungumza kuhusiana na mafunzo waliyoyapata wenyeviti wa Mabaraza ya ardhi nchini alisema kuwa, yatawajengea uwezo na anaamini mara baada ya kujifunza watakaporudi kwenye vituo vyao vya kazi watakuwa na nafasi nzuri ya kusikiliza mashauri ya ardhi sambamba na kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora.
Sehemu ya washiriki wa mkutano huo wakimsikiliza Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Ridhiwani Kikwete (hayupo pichani) wakati akizungumza nao.
Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Ridhiwani Kikwete (kulia) akizungumza na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Dkt. Allan Kijazi. Kushoto ni Msajili wa Mabaraza ya Ardhi na Nyumba ya Wilaya nchini, Stella Tullo.
Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Ridhiwani Kikwete akisalimiana na baadhi ya washiriki wa mkutano huo. Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Ridhiwani Kikwete akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya washiriki.
***********
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Ridhiwani Kikwete amewataka Wenyeviti wa Mabaraza ya Ardhi na Nyumba ya wilaya nchini kuwa waadilifu sambamba na kujiepusha na vitendo vya rushwa ili kutenda haki wakati wa kutoa maamuzi ya mashauri yanayohusu migogoro ya ardhi.
Aidha, alizitaka Mamlaka za Nidhamu kuwachukulia hatua za kinidhamu watumishi wote wasiotimiza wajibu wao au wanaoidhalilisha serikali kwa kuendesha vitendo vya rushwa.
Wenyeviti wa Mabaraza ya Ardhi na nyumba ya wilaya nchini pamoja na Wasajili Wasaidizi wanakutana mkoani Tanga kwenye kikao kazi na mafunzo cha siku nne kujadiliana namna bora ya kuboresha utendaji kazi na utoaji huduma bora kwa wananchi kuhusiana mashauri ya ardhi.
‘’Daima tukumbuke ili mabaraza ya ardhi yaweze kuheshimika ni wajibu wenu wenyeviti wa mabaraza kama watumishi wa umma kufanya kilicho sahihi yaani kuzingatia weledi, kuwa waadilifu na kuwajibika. Tukumbuke kuwa sisi ni watumishi wa umma ni waajiriwa wa wananchi‘’ alisema Ridhiwani.
Akizungumza kwenye kikao kazi na Mafunzo mkoani Tanga tarehe 5 April 2022 Naibu Waziri wa Ardhi alisema, Mabaraza ya Ardhi na Nyumba ya wilaya kama vyombo vya kutoa haki yana wajibu wa kuhakikisha yanatoa huduma bora kwa wananchi ili kuondoa malalamiko dhidi ya ukiukwaji wa maadili katika kushughulikia migogoro ya ardhi.
‘’Haki na wajibu ni sawa na chanda na pete katika uwajibikaji wa daraja la juu. Mtekelezaji wa utoaji au usimamizi wa halki bila kuwa muadilifu ni mtihani mkubwa’’ alisema Ridhiwani.
Alieleza kuwa, maadili ni kitu muhimu cha kuzingatia katika utendaji kazi hasa kipindi hiki ambacho serikali ya wamu ya sita inafanya juhudi mbalimbali kuhakikisha kuwa watumishi wa umma wanazingatia maadili yanayosimamaia utumishi wa umma.
‘’Mhe Rais Samia Suluhu Hassan katika matamshi yake, mbalimbali ameonesha wazi nia yake ya kuurejesha utumishi wa umma kuwa utumishi uliotukuka na unaozingatia taratibu za utendaji na maadili yanayoongoza utumishi wa umma’’ alisema Ridhiwani.
Kwa upande wake Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Allan Kijazi alisema, Wizara yake itaanza kuweka mfumo wa ufuatiliaji utendaji kazi wa wenyeviti wa mabaraza ya ardhi kwa lengo la kuboresha utendaji kazi.
‘’Katika mfumo huo wa ufuatiliaji wale wenyeviti ambao utendaji wao utaridhisha tutakuwa pamoja na wale wasiotaka kubadilika itabidi watupishe na tutafute watendaji au wenyeviti walio tayari kutekeleza majukumu na wako tayari kutenda haki na watanzania wote bila kubagua lakini kikubwa zaidi kuwa tayari kubadilisha taswira ya wizara ya kiutendaji kutoka wizara ya malalamiko na kuwa wizara yenye kupewa sifa nzuri za utendaji’’ alisema Dkt Kijazi.
Naye Msajili wa Mabaraza ya Ardhi na Nyumba ya Wilaya nchini Stella Tullo alielezea mafunzo waliyoyapata wenyeviti wa Mabaraza ya ardhi nchini alisema kuwa, yatawajengea uwezo na anaamini mara baada ya kujifunza watakaporudi kwenye vituo vyao vya kazi watakuwa na nafasi nzuri ya kusikiliza mashauri ya ardhi sambamba na kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora.











0 comments:
Post a Comment