Akizungumza jijini Dodoma wakati wa uzinduzi wa mfumo huo,Mkuu wa Idara ya biashara kutoka Benki ya CRDB,Dk.Joseph Witts alisema kwa kutumia Benki ya CRDB na mitandao ya simu mtu ataweza kulipa sadaka,zakka na michango mingine.
Dk.Witts alisema mfumo huo wa usimamizi wa fedha za kanisa utasaidia ukusanyaji wa mapato ya kanisa hilo kwani umeishafanya kazi katika Taasisi nyingi ikiwemo Hospitali za Bugando na KMC.
“Kwanza niwapongeze Kanisa kwa uamuzi huu,maana licha ya kwamba katika Kanisa kuna watu wametakwaswa lakini mmeamua kuja na mfumo wa kuzuia upotevu wa fedha kanisani,nasema hongereni sana,mmetupa heshima kwani kuna Mabenk zaidi ya 50 lakini mmeamua kuja kwetu,” Amesema.
Mkuu huyo wa Idara ya biashara alihakikishia Kanisa watausimamia mfumo huo na wala hawatawangusha huku akiahidi kuleta mageuzi makubwa.
“ Mwanadamu ni mwanadamu tu baadhi walikuwa wakishindwa kutoa matoleo lakini naamini sasa wataanza kutoa.Sisi CRDB sio tunatoa tu huduma bali tunatoa huduma zinazokidhi viwango,” Amesema Dk.Witts.
Kwa upande wake,Askofu Mkuu wa Kanisa la Waadventista wa Sabato,Jimbo Kuu la Kusini mwa Tanzania,Mark Malekana alisema matarajio yao kupitia mfumo huo waumini watakuwa na imani ya kutoa matoleo na hivyo kuongeza uchumi wa Kanisa.
“Kwanza mapato yataongezeka na yatakuwa salama na fedha hazitaibiwa kwani zikifika benki zinakuwa katika mikono salama,pia tunakuwa tupo katika matumizi ya teknolojia,” Amesema.
Mhazini Mkuu wa Jimbo Kuu la Kusini la kanisa hilo, Athanas Sigoma amesema mfumo huo umeanzishwa ukiwa na malengo makubwa kwa kutumia mabadiliko ya Sayansi na Teknolojia hivyo ni imani yao kwamba wengi watatoa sadaka na hivyo mapato kuongezeka.
Amesema kutokana na ukubwa wa Kanisa hilo awali wahasibu walikuwa wakisafiri kwenda maeneo mbalimbali kwa ajili ya kukusanya sadaka wakiwa na vitabu vya risiti lakini baada ya mfumo huo wanaamini utaokoa fedha nyingi walizokuwa wakizitumia awali.
“ Tuna Makanisa zaidi ya 4000 wahasibu kila siku walikuwa wanasafiri kwenda maeneo mbalimbali hivyo kwa sasa gharama zinapungua kwani wengi watalipa kwa njia ya simu tu kwa kutumia mitandao ya simu,” Amesema.
Naye, Mhazini Mkuu wa Jimbo Kuu la Kaskazini, Dickson Matiko alisema kupitia mfumo huo wataweza kutawala fedha huku akitoa wito kwa Wasabato wote kuupokea mfumo huo ambao ni rafiki.
Mkuu wa Idara ya Biashara kutoka Benki ya CRDB, Dk Joseph Witts akizungumza wakati wa uzinduzi wa mfumo wa ukusanyaji sadaka uliofanywa baina yao na Kanisa la Waadventista Wasabato jijini Dodoma.
Watumishi wa Benki ya CRDB na Washiriki wa Kanisa la Waadventista Wasabato jijini Dodoma wakifuatilia uzinduzi wa mfumo wa ukusanyaji sadaka uliofanywa baina ya kanisa hilo na Benki hiyo
0 comments:
Post a Comment