Nafasi Ya Matangazo

September 30, 2019

Bwawa la kilimo cha umwagiliaji Mwamapuli upande ambao wanachi wanaweza kutumia maji hayo kwa matumizi ya nyumbani na kunyweshwea mifugo na sehemu ya maji ya bwawa hilo pia hutumika kwa shughuli za uvuvi.
**********
Na Mwandishi Wetu, Igunga Tabora
WAKULIMA katika Halmashauri ya Igunga mkoani Tabora wameipongeza serikali kwa kuwekeza katika ujenzi wa miundo mbinu bora ya umwagiliaji na kwamba sasa wameondokana na umaskini.

Wakizungumza na maofisa wa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji mwishoni mwa wiki waliotembelea Skimu ya Mwamapuli wilayani humo, wakulima hao wamesema juhudi za serikali za kuwajengea bwawa lenye mita za ujazo 28,000,000 ambalo linamwagilia takribani hector 630 za mpunga zimezaa matunda kwani wakulima sasa sio maskini tena kutokana na uzalishaji wa mpunga kuongezeka.

Wamesema kabla ya uboreshaji wa miundombinu uzalishhaji ulikuwa tani 2.5 kwa hector wakati kwa sasa uzalishaji umefikia tani 7.5 kwa hekta hivyo kuifanya wilaya ya Igunga kuwa na usalama wa chakula na kuongeza mapato ya halmashauri na kuinua kipato cha familia.

Akizungumza awali Afisa Umwagiliaji wa Wilaya ya Igunga Bw. Elibariki Kisanga amesema uwekezaji wa serikali katika maboresho ya miundombinu ya umwagiliaji katika skimu ya Mwamapuli kupitia mradi wa kuendeleza wakulima wadogo wadogo (SSIDP) umegharimu zaidi ya shilingi milioni 537.

Hata hivyo amesema katika mipango ya halmashauri wameiomba serikali iwapatie kiasi cha shilingi bilioni 1.1 ili waweze kuongeza kina cha maji ambacho kitaongeza uzalishaji zaidi.

Amesema serikali imejenga mifereji mikubwa mitatu na mingine midogo midogo ambayo inamwagilia mashamba ya wakulima wapatao 970 katika skimu ya Mwamapuli iliyoko kilomita 9 toka Igunga mjini.

Bwana Kisanga amesema wakulima wamekuwa wakifuata maelekezo ya wataalamu hususan matumizi bora ya mbolea, mbegu na maji hivyo kuongeza uzalishaji.

Naye mwenyekiti wa Chama cha Ushirika cha Umwagiliaji wa Mwamapuli Bw. Robert Lufunga amesema kilimo cha umwagiliaji kimeleta ukombozi kwa wakulima wilayani humo ambao awali walionekana kuwa wanyonge.

“Katika skimu yetu hii mkulima sio mtu mnyonge tena , wakulima wetu ndio wenye pesa na maisha yao yamebadilika sana” , alisema Bwana Lufunga.

Amesema wakulima wengi wanamiliki vyombo vya usafiri, wamejenga nyumba bora na wanajitosheleza kwa chakula na wanasomesha watoto wao kwenye shule za kulipia.

Lufunga amesema kutokana na uzalishaji kuongezeka Chama chao kila msimu huchangia kwenye shughuli za elimu na ujenzi wa barabara na pia kila mkulima huchangia sh.1000 kwa kila gunia analovuna.

Ameongeza kuwa kila msimu Skimu ya umwagiliaji ya Mwamapuli hutoa ajira kwa watu wengi wakiwemo vijana ambao hushughulika na maandalizi ya mshamba, kulima na kuvuna.

Amesema zaidi ya milioni 700 hutumika katika kulipa ajira mbalimbali ikiwemo kulima kwa kutumia zana za kisasa.

Bwawa hilo lilijengwa mwaka 1970 kwa gharama za shilingi milioni 7 linahudumia kata za Mwamapuli, mwanzugi , Mwalala na makomero.
Posted by MROKI On Monday, September 30, 2019 No comments

0 comments:

Post a Comment

  • Facebook
  • Twitter
  • Youtube

Labels

Blog Archive

Nafasi Ya Matangazo