Nafasi Ya Matangazo

February 06, 2025


MAKUSANYO  ya maduhuli ya Serikali kupitia Sekta ya madini katika Mkoa wa Njombe  yatokanayo na mrabaha, tozo na ada mbalimbali yameendelea kupaa kutoka mwaka hadi mwaka tangu kuanzishwa kwa Ofisi ya Tume ya Madini kupitia Ofisi ya Afisa Madini Mkazi ya Mkoa wa Njombe.

Akizungumza kwa niaba ya Afisa Madini Mkazi Mkoa  wa Njombe, Mjiolojia Abraham Nkya amesema kuwa, ofisi hiyo imeendelea kufanya vizuri kwenye ukusanyaji wa muduhuli kutokana na mikakati waliyoiweka ikiwa ni pamoja na kuimarisha ukaguzi kwenye maeneo yote yenye uchimbaji wa madini ya makaa ya mawe.

Akielezea hali ya makusanyo ya maduhuli amesema katika kipindi cha mwaka wa fedha uliopita 2023/2024 waliwekewa lengo la makusanyo ya Shilingi Bilioni 2.3 na waliweza kukusanya Shilingi Bilioni 4.5 sawa na asilimia 196 ya lengo na sehemu kubwa ya makusanyo yanatokana na mrabaha, ada ya ukaguzi, ada za leseni na vibali mbali mbali vinavyotolewa kwa mujibu wa Sheria ya Madini sura 123

Amefafanua katika kipindi cha mwaka wa fedha 2024/2025 Ofisi imeweka mikakati ya kuhakikisha inaendelea kuvuka lengo lililowekwa na Serikali.

Akielezea fursa za uwekezaji katika mkoa wa Njombe Mjiolojia Nkya amesema,“ Mkoa wa Njombe tuna madini mbali mbali yakiwemo ya chuma, manganizi, makaa ya mawe, madini ya ujenzi na dhahabu, na kuongeza, 

“Madini ya makaa ya mawe ndio yanayoongoza kwa kutupa  mapato makubwa mfano mwaka wa fedha uliopita wa 2023/2024  madini ya makaa ya mawe pekee yaliingiza  kiasi cha Shilingi Bilioni  4.155  na kuufanya Mkoa wa Njombe kuchangia vizuri kwenye mapato ya serikali,”amesema.

Aidha, ametoa wito kwa wawekezaji katika Sekta ya Madini  kuwekeza mkoani Njombe akitolea mfano wa Wilaya ya Ludewa ambayo ina kiasi kikubwa cha makaa ya mawe (mashapo) yaliyofanyiwa utafiti ambapo kiasi kilichobainika ni tani milioni 500 ambapo katika eneo la Nkomang’ombe kuna takribani  tani  milioni 430   za makaa ya mawe na kwamba bado kuna maeneo ambayo yanahitajika kufanyiwa utafiti zaidi.

Katika hatua nyingine, Mjiolojia Nkya amesema kuwa tayari Serikali imelipa fidia wananchi wapatao 1,143 katika maeneo mawili ya miradi ya Makaa ya mawe ya  Nkomang’ombe, na Chuma  Liganga.

Amesema, Shilingi Bilioni  10.2 imelipwa kama fidia na riba kwa wananchi 493 katika mradi wa Chuma Liganga katika vijiji vya Mundindi na Amani na Shilingi Bilioni 5.2 imelipwa kama fidia na riba kwa wananchi 650 katika mradi wa makaa ya mawe mchuchuma kwa kijiji cha Nkomang'ombe ili kupisha uwekezaji katika miradi hiyo.
 
 Aidha amesema, Agosti 2, 2024  kwa niaba ya Serikali, Shirika la Maenedeleo la Taifa (NDC) ilisaini mkataba na kampuni ya Fijian Hexingwang Industry Tanzania Co. Limited  ya nchini  China kwa ajili ya uchimbaji wa madini ya chuma yaliyopo Wilaya ya Ludewa mkabala na mradi wa Chuma wa Liganga  eneo linalojulikana kama Maganga Matitu.
 
“ Kwa sasa wabia wapo katika hatua za mwisho za usajili wa kampuni ya pamoja itakayosimamia shughuli zote za uchimbaji madini hayo ya chuma, ni matumaini yetu kama Ofisi ya Madini Mkoa wa Njombe mradi huu utaanza mapema na kuleta matokeo chanya katika Mkoa wa Njombe na Taifa kwa ujumla.




Posted by MROKI On Thursday, February 06, 2025 No comments

0 comments:

Post a Comment

  • Facebook
  • Twitter
  • Youtube

Labels

Blog Archive

Nafasi Ya Matangazo