RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt John Pombe Magufuli amemteua Rais Mstaafu wa Awamu ya Pili, Mhe. Alhaji Ali Hassan Mwinyi kuwa Mkuu wa Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS).
Mhe. Alhaji Ali Hassan Mwinyi ameteuliwa kuendelea na wadhifa huo kuanzia leo tarehe 25 Septemba, 2019.
Mhe. Rais Magufuli pia amefanya uteuzi wa wenyeviti wanne wa bodi za taasisi mbalimbali kama ifuatavyo;
Kwanza, Mhe. Rais Magufuli amemteua, Prof. Mayunga Nkunya kuwa Mwenyekiti wa Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU). Prof. Nkunya anachukua nafasi ya Prof. Jacob Mtabaji ambaye muda wake umemalizika. Prof. Nkunya ni Katibu Mstaafu wa Baraza la Vyuo Vikuu vya Afrika Mashariki (IUCEA).
Pili, Mhe. Rais Magufuli amemteua, Prof. Idrissa Bilali Mshoro kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (Rural Water Supply and Sanitation Authority – RUWASA). Prof. Mshoro ni Profesa wa Uhandisi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).
Tatu, Mhe. Rais Magufuli amemteua, Prof. Elias Tozo Bisanda kuwa Mwenyekiti wa Bodi wa Tume ya Taifa ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO). Prof. Bisanda anashika wadhifa huo kwa kipindi cha pili.
Nne, Mhe. Rais Magufuli amemteua Prof. Apollinaria E. Pereka kuwa Mwenyekiti wa Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT). Prof. Pereka anashika wadhifa huo kwa kipindi cha pili.
Taarifa iliyotolewa na Katibu Mkuu Kiongozi, Mhe. Balozi John Kijazi imeeleza kuwa uteuzi wa wenyeviti hao umeanza leo tarehe 25 Septemba, 2019.
0 comments:
Post a Comment