Nafasi Ya Matangazo

March 15, 2019

 Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira, January Makamba (katika) akiongea na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge wa Viwanda, Biashara na Mazingira, Murad Sadick mara baada ya kutembelea Ziwa Manyara kuona hali halisi ya Ziwa hilo kwa sasa ambalo liko hatarini kutoweka kutokana na ongezekeo la shughuli za kibadamu pembezoni mwa ziwa hilo zisizo endelevu. Wengine pichani, ni sehemu wa waheshimiwa wabunge, wajumbe wa Kamati hiyo.
 Ziwa Manyara linavyo onekana kwa sasa, kina cha maji kimeshuka sana kutokana na kujaa tope. Kamati ya Bunge imeshauri Serikali kuchukua hatua za haraka kunusuru kutoweka kwa ziwa hilo.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira, January Makamba akifafanua jambo kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge wa Viwanda, Biashara na Mazingira mara baada ya kufanya ziara ya kikazi ya kutembelea Ziwa Manyara kuona changamoto za uharibifu wa mazingira utokanao na shughuli zisizo endelevu za kibinadamu ikiwemo kilimo katika vyanzo vya maji.
**************

Na Lulu Mussa,Manyara
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira  imeshauri Serikali kuandaa mpango Mkakati wa haraka wa kunusuru Ziwa Manyara ambalo liko hatarini kutoweka kutokana shughuli za kibadamu.  Akizungungumza kwa niaba ya Kamati yake Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Murad Sadick amesema ni wakati muafaka sasa jambo hili kupewe kipaumbele ili kunusuru hali ya sasa inayotishia uhai wa ziwa hilo.

Wakiwa  katika ziara ya kikazi Mkoani Manyara, Kamati hiyo imetembelea Ziwa Manyara na kujionea kupungua kwa kina cha maji kwa kiasi kikubwa kutokana na shughuli za kibinadamu ikiwa ni pamoja na kilimo kisicho endelevu hususan katika vyanzo vya maji kinachopelekea ziwa hilo kujaa tope pamoja na ongezeko la mimea vamizi.

“Sote tumejionea hali halisi, hali ni mbaya, mimi na Kamati yangu tunawajibu wa kuishauri Serikali, hatua za haraka na za maksudi kunusuru hali hii, hata kwa maziwa mengine pia kama Ziwa Jipe na Ziwa Chala. Endapo hatua za haraka hazitachukuliwa ndani ya miaka kumi ijayo Ziwa hili litatoweka. Ikumbukwe kuwa ziwa hili ni chanzo kikubwa cha kukuza pato la Taifa kupitia Utalii hapa nchini” Alisisitiza Sadick.

Akiwasilisha hatua za zilizochukukuliwa na Mamlaka ya Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) kuhusu kunusuru ziwa hilo Naibu Mkurugenzi,William Mwakilime amesema kuwa Ofisi yake imechukua hatua za makusudi ikiwa ni pamoja na kutoa elimu kwa Umma juu ya namna bora ya kuwa na kilimo endelevu kinachozingatia matumizi bora ya ardhi  na kujenga mabwawa maalumu kwa ajili ya kuchuja maji.

Nae Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muugano na Mazingira, Mheshimiwa January Makamba alieambatana na Kamati hiyo ya Kudumu ya Bunge katika ziara hiyo, amesema Serikali iko katika hatua za mwisho za kukamilisha andiko jumuishi litakalogusa sekta zote kwa kuwa ni suala mtambuka na kuahidi kuwa Serikali inalipa uzito jambo hilo kwa mustakabali wa nchi na ustawi wa wananchi wake.

Katika hatua nyingine Kamati imeipongeza Serikali kwa kupokea ushauri wa Kamati hiyo ya kuunda kikosi kazi cha kupambana na mimea vamizi ambayo imekuwa ikiathiri maeneo mengi hapa nchini ikiwa ni pamoja na maeneo ya Hifadhi. Waziri Makamba ameainisha kuwa Kikosi kazi hicho kilichoundwa na  Makamu wa Rais kimekamilisha kazi na taarifa yake iko katika hatua za maamuzi.

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira iko katika ziara ya kikazi Mkoani Arusha pia itatembelea miradi ya uchimbaji wa visima Bagamoyo Mkoa wa Pwani, ikiwa ni miongoni mwa miradi inayosimamiwa na Ofisi ya Makamu wa Rais chini ya Mkataba wa kuhimili mabadiliko ya tabianchi.
Posted by MROKI On Friday, March 15, 2019 No comments

0 comments:

Post a Comment

  • Facebook
  • Twitter
  • Youtube

Labels

Blog Archive

Nafasi Ya Matangazo