Nafasi Ya Matangazo

March 15, 2019

Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa, Jason Rweikiza (Mb) akitoa hatimiliki za kimila kwa mmoja wa wananchi wa kijiji cha Mbondo wilayani Nachingwea wakati wa ziara ya kamati yake ya kukagua miradi ya maendeleo mkoani Lindi.
Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa wakitoka kukagua jengo la masijala ya ardhi kijiji cha Mbondo wilayani Nachingwea linalojengwa kupitia MKURABITA wakati wa ziara ya kamati hiyo yenye lengo la kukagua miradi ya maendeleo mkoani Lindi.
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa, Jason Rweikiza (Mb) akieleza umuhimu wa hatimiliki za kimila kabla ya kuwapatia wananchini wa kijiji cha Mbondo wilayani Nachingwea wakati wa ziara ya kamati yake ya kukagua miradi ya maendeleo mkoani Lindi.
Wananchi wa kijiji cha Mbondo wakimsikiliza Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa, Jason Rweikiza (Mb) alipokuwa akizungumza nao juu ya umuhimu wa hatimiliki za kimila wakati wa ziara ya kamati yake ya kukagua miradi ya maendeleo mkoani Lindi.
Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa, Mwanne Mchemba (Mb) akitoa wito kwa wananchi wa kijiji cha Mbondo wilayani Nachingwea kuchangamkia fursa ya hatimiliki za kimila wakati wa ziara ya kamati yake ya kukagua miradi ya maendeleo mkoani Lindi.
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Dkt. Mary Mwanjelwa (Mb) akieleza azma ya serikali ya kuwainua wanyonge kwa kuwapatia hatimiliki za kimila ili waweze kujikwamua kiuchumi.
Mtendaji Mkuu wa MKURABITA, Seraphia Mgembe akizungumzia umuhimu wa wananchi wa kijiji cha Mbondo wilayani Nachingwea kumiliki hatimiliki za kimila wakati wa ziara ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa yenye lengo la kukagua miradi ya maendeleo mkoani Lindi.
***************
SERIKALI imetoa hatimiliki za kimila 100 kwa wananchi wa kijiji cha Mbondo wilayani Nachingwea ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa urasimishaji rasilimali ardhi vijijini kwa lengo la kuwawezesha wananchi hao kiuchumi. 

Hati hizo zimetolewa na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa,Jason Rweikiza (Mb) wakati wa ziara ya kamati hiyo yenye lengo la kukagua miradi ya maendeleo mkoani Lindi ikiwa ni pamoja na kujiridhisha namna Mpango wa Kurasimisha Rasilimali na Biashara za Wanyonge Tanzania (MKURABITA) inavyotekeleza majukumu yake. 

Rweikiza amesema hati hizo ni muhimu kwa wananchi hao kujiendeleza kiuchumi kwani zitawawezesha kuchukua mikopo kwenye taasisi za kifedha kwa ajili ya kuendeleza shughuli za kilimo ikiwemo zao la korosho ambalo ndio zao kuu la kibiashara mkoani Lindi. 

Aidha amewaasa wananchi waliopata hati hizo kuzitumia vizuri ili ziweze kuwanufaisha kiuchumi, na kuwahamasisha wale ambao hawaoni umuhimu wa kupata hati za kimila kuchangamkia fursa hiyo ili waweze kupiga hatua kimaendeleo. 

Ili kuwarahisishia wananchi wa kijiji cha Mbondo na vijiji jirani kupata hatimiliki za kimila, Rweikiza ameiagiza MKURABITA kuhakikisha inakamilisha ujenzi wa Masijala ya Ardhi kabla ya mwaka huu kuisha. 

Naye, Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Dkt. Mary Mwanjelwa (Mb) amesema Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli amedhihirisha kwa vitendo kuwajali wanyonge hasa walioko maeneo ya vijijini kwa kuwapatia hatimiliki za kimila ili ziweze kuwasaidia kuondokana na umaskini. 

Dkt. Mwanjelwa ameongeza kuwa, hati hizo za kimila zinatambuliwa na taasisi za kifedha nchini, hivyo zitawawezesha wananchi hao kupata mikopo kwa ajili ya kuendesha shughuli zao za kiuchumi. 

Aidha, Dkt. Mwanjelwa ametoa wito kwa taasisi za kifedha nchini, kuhakikisha zinatoa kipaumbele kwa wananchi wenye hati za kimila pindi wanapohitaji huduma ya mkopo. 

Kwa upande wake, Mratibu wa Mpango (MKURABITA), Seraphia Mgembe amesema Serikali inatoa hatimiliki za kimila kwa lengo la kuwawezesha wananchi walioko maeneo ya vijijini kuondokana na umaskini. 

Mgembe amefafanua kuwa, hati hizo zinathaminiwa na wawekezaji na taasisi za kifedha, hivyo zitawawezesha wananchi wenye hati kuingia ubia na wawekezaji na hatimaye kunufaika na umiliki wa hati hizo. 

Halmashauri ya Wilaya ya Nachingwea ni miongoni mwa halmashauri 52 zilizojengewa uwezo na MKURABITA kwa ajili ya utekelezaji wa urasimishaji rasilimali ardhi vijijini ambapo kijiji cha Mbondo ni miongoni vya vijiji vilivyonufaika.
Posted by MROKI On Friday, March 15, 2019 No comments

0 comments:

Post a Comment

  • Facebook
  • Twitter
  • Youtube

Labels

Blog Archive

Nafasi Ya Matangazo