Waziri wa Habari Sanaa Utamaduni na Michezo Dr. Harison Mwakyembe (kulia) akimkabidhi bendera Captain wa timu ya taifa ya riadha Marco Sylvester (kushoto) wakati wa hafla ya kuiaga timu hiyo inayokwenda kushiriki mashindano ya dunia ya mbio za nyika yanayofanyika nchini Denmark tarehe 30 mwezi huu. Tanzania imepeleka timu ya wachezaji 16 na viongozi 4. Wafadhili wakuu wa timu hiyo ni DStv na Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro.
**************
TIMU ya Taifa ya riadha itakayoshiriki mashindano ya Dunia ya Mbio za Nyika yatakayofanyika nchini Denmark tarehe 30 Machi 2019, imeondoka nchini ikiwa na wachezaji 16 na viongozi 4 na kutajwa kuwa timu kubwa zaidi ya Tanzania kuwahi kushiriki katika mashindano hayo nje ya bara la Afrika.
Timu hiyo inajumuisha timu ya nyika ya wanaume (5), Timu ya Nyika ya wasichana (5) na timu ya mchanganyiko ya mbio za kupokezana vijiti (Mixed relay)
Timu hiyo imeagwa na kukabidhiwa bendera ya Taifa jana na waziri wa Habari, Sanaa utamaduni na Michezo Dr. Harison Mwakyembe katika hafla ambayo pia ilihudhuriwa na wafadhili wakuu wa timu hiyo DStv na Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro
Waziri Mwakyembe ameikumbusha timu hiyo kuwa wana jukumu kubwa sana la kupambana kufa na kupona ili kupata medali na pia kuliletea taifa sifa. “Hivi karibuni tumeshuhudia mafanikio makubwa katika michezo hapa nchini, tunatarajia kuwa mtaliendeleza wimbi hili la mafanikio na ushindi kwa kuleta medali” alisema waziri
Amewashukuru sana wafadhili wote waliowezesha timu hiyo kwenda kuliwakilisha taifa hususan wafadhili wakuu DStv na Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro ambao wamekuwa wakidhamini riadha kwa muda sasa.
Mkuu wa uhusiano wa MultiChoice Tanzania Johnson Mshana, amesema kuwa DStv wamekuwa wakidhamini riadha kwa takriban miaka minne sasa na lengo la kubwa ni kuliandaa taifa kwa ajili ya mashindano makubwa duniani ya Olyimpic yatakayofanyika Tokyo Japan mwaka 2020.
“Tuna mkakati wa kuliandaa taifa kushiriki na kushinda katika Olyimpic. Dhamira yetu kuona wimbo wetu wa taifa unapigwa kwa mara ya kwanza kwenye mashindano hayo makubwa. Lakini hili haliwezi kutokea ikiwa hatutawekeza nguvu kubwa mapema” alisisitiza Mshana
Naye Mkuu wa Uhusiano wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro Joyce Mgaya, amesema Mamalaka hiyo imeamua kuwekeza kwenye riadha kwani ni sehemu muhimu ya kulitangaza taifa letu na hivyo fursa kubwa ya kukuza utalii ambayo ni sekta muhimu sana katika ukuaji wa uchumi wa nchi.
“Kwa kuwa na timu na wachezaji wanaofanya vizuri katika mashindano ya kimataifa, tunaweza kuitangaza nchi yetu kote ulimwenguni kirahisi zaidi na hivyo kuchangia sana katika kukuza utalii wetu na hii ndiyo dhamira kubwa ya Mamlaka yetu. Tunaamini timu yetu hii, kuw ukubwa na ubora wake itafanya vizuri kwenye mashindano haya ya Dunia”.
Timu hiyo ilichaguliwa baada ya mashindano ya Taifa ya mbio za nyika yaliyofanyika mjini Moshi Februari mwaka huu na inatarajiwa kurujea nyumbani tarehe 31 Machi 2019
0 comments:
Post a Comment