Nafasi Ya Matangazo

December 21, 2018

Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Dkt. Mary Mwanjelwa (Mb) akizungumza na watumishi wa Idara ya Ukuzaji Maadili, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora alipoitembelea idara hiyo kwa lengo la kufahamu majukumu ya idara na kuhimiza uwajibikaji.
Mkurugenzi wa Idara ya Ukuzaji Maadili, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Bw. Fabian Pokela (kulia) akifafanua majukumu ya Idara yake kwa Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Dkt. Mary Mwanjelwa (Mb) (hayupo pichani) alipoitembelea idara hiyo kwa lengo la kufahamu majukumu ya idara na kuhimiza uwajibikaji.
Baadhi ya watumishi wa Idara ya Ukuzaji Maadili,Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora wakipokea maelekezo kutoka kwaNaibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Dkt. Mary Mwanjelwa (Mb) (hayupo pichani) alipoitembelea idara hiyo kwa lengo la kufahamu majukumu ya idara na kuhimiza uwajibikaji.

Na Happiness Shayo
Watumishi wa umma nchini wametakiwa kuzingatia maadili na nidhamu ya kazi kwani ndio msingi na nyenzo kuu itakayowawezesha kutekeleza majukumu yao kikamilifu. 

Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Dkt. Mary Mwanjelwa (Mb) alipokutana na watumishi wa Idara ya Ukuzaji Maadili, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa lengo la kufahamu majukumu ya idara hiyo na kuhimiza uwajibikaji. 

Mhe. Dkt. Mwanjelwa amesema, maadili mema kwa watumishi wa umma ndio kitovu cha utumishi wa umma hivyo ameitaka Idara ya Ukuzaji Maadili kuhakikisha watumishi wa umma wanazingatia misingi ya maadili mema na nidhamu katika utendaji ili waweze kutoa huduma bora na kwa wakati kwa wananchi. 

Mhe. Dkt. Mwanjelwa amefafanua kuwa mtumishi wa umma akiwa na maadili mema, utendaji kazi wake utaimarika pia utii, heshima na adabu vitaongezeka hivyo atakuwa mchapakazi hodari na anayezingatia weledi. 

Mhe. Dkt. Mwanjelwa ameongeza kuwa, mtumishi wa umma anatakiwa ajitambue katika mwenendo wake, azingatie mavazi ya heshima mahala pa kazi, awe na lugha nzuri yenye staha kwa wateja ili awe kioo na mfano mzuri wa kuigwa katika jamii. 

Mhe. Dkt. Mwanjelwa ameisisitiza Idara ya Ukuzaji Maadili kutengeneza mkakati madhubuti wenye ubunifu utakaowezesha kutoa elimu ya maadili kwa umma ili jamii itambue umuhimu wa maadili mema mahala pa kazi, na ameongeza kuwa Idara hiyo iweke utaratibu wa kuzitambua Taasisi na watumishi wa umma wanaozingatia maadili ya kazi kwa kuwapa tuzo lengo likiwa ni kuwapa motisha ya utendaji kazi. 

Mhe. Dkt. Mwanjelwa ameainisha kuwa, watumishi wa umma wakiwa waadilifu na wazalendo, watawezesha kupunguza malalamiko ya wananchi dhidi ya huduma zinazotolewa na Taasisi za Umma. 

Aidha, Dkt. Mwanjelwa ameitaka Idara hiyo kuunga mkono jitihada za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli kwa vitendo katika kuhimiza uadilifu na uwajibikaji kwa watumishi wa umma nchini ili utumishi wao uwe na tija katika maendeleo ya Taifa. 

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Idara ya Ukuzaji Maadili, Bw. Fabian Pokela amesema kuwa, majukumu ya Idara hiyo yamegawanyika katika sehemu kuu mbili ambazo ni Ukuzaji Maadili katika utumishi wa umma na Ufuatiliaji wa Uzingatiaji wa Maadili katika utumishi wa umma sanjari na ushughulikiaji wa malalamiko ya wananchi yanayohusu ukiukwaji wa maadili katika Utumishi wa Umma. 

Bw. Pokela amefafanua kuwa, jukumu la sehemu ya Ukuzaji Maadili ni kuhakikisha kuwa watumishi wa umma na wananchi kwa ujumla wanapata uelewa kuhusu maadili ya utumishi wa umma kupitia kampeni za uhamasishaji, maonesho mbalimbali, vipeperushi, majarida mbalimbali, semina, warsha, mikutano na mafunzo ya muda mfupi. 

Bw. Pokela amesema Idara yake pia imeandaa vipindi vya redio na televisheni vitakavyotoa elimu kwa umma juu ya maadili mema mahala pa kazi na kuhimiza uadilifu kwa Watendaji Wakuu wa Taasisi na mtumishi wa umma mmoja mmoja. 

Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Dkt. Mary Mwanjelwa (Mb) ameitembelea Idara ya Ukuzaji Maadili ikiwa ni mwendelezo wa ziara yake katika Idara na Vitengo vya Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora ili kuhimiza uwajibikaji.
Posted by MROKI On Friday, December 21, 2018 No comments

0 comments:

Post a Comment

  • Facebook
  • Twitter
  • Youtube

Labels

Blog Archive

Nafasi Ya Matangazo