Baada ya kimya cha muda,
Africa Magic ikishirikiana na MultiChoice, hatimaye wametangaza rasmi kuanza
kwa kinyang’anyiro cha moja ya tuzo maarufu duniani katika tasnia ya sanaa ya
filamu zijulikanazo kama Africa Magic Viewers’ Choice Awards (AMVCAs).
Tuzo hizo ambazo
hufanyika kila mwaka zimekuwa zikihusisha mamia ya washiriki kutoka kila kona
ya bara la Afrika na zimekuwa moja ya tuzo zilizojizolea umaarufu mkubwa barani
Afrika na duniani kwa ujumla na limekuwa ni jukwaa muhimu la kutambua na kuenzi
vipaji vya tasnia ya filamu katika bara la Afrika.
AMVCAs zilibuniwa kuthamini
na kutambua mchango wa watengeneza filamu wa Kiafrika, waigizaji na wataalam
katika mafanikio ya sekta ya filamu na televisheni ya bara hili na kutokana na
mafanikio ya tuzo tano zilizopita, maandalizi ya tuzo za mwaka huu ambazo
zinatarajiwa kuwa kubwa na za kuvutia zaidi yameanza na muamko tayari
umeshaanza kuonekana na ushindani unatarajiwa kuwa mkubwa sana.
Mkurugenzi wa
MultiChoice Tanzania Maharage Chande amebainisha kuwa wasanii wa Tanzania sasa
wanaweza kuanza kuwasilisha kazi zao kwa ajili ya tuzo hizo na kazi hizo
zitaendelea kupokelewa hadi tarehe 30 Aprili 2018.
“Baada ya mapumziko
mafupi, tunayo furaha kutangaza kwamba
mwaka 2018 utakuwa na toleo la mwaka wa sita mfululizo wa MultiChoice na
Africa Magic kuandaa AMVCAs kwa mafanikio na tunaendelea kujivunia mabadiliko
yanayoonekana kwenye nyanja ya filamu tangu Tuzo zilipoanzishwa. Uwekezaji wetu
endelevu unaonesha dhamira yetu katika kusaidia kuibua na kuthamini vipaji
barani Afrika na tunaamini kwamba toleo la 2018 la AMVCAs litaacha alama kubwa
zaidi katika sekta ya utayarishaji filamu ya Afrika kuliko matoleo matano
yaliyopita” alisema Maharage.
“Kwa muda mrefu tumekuwa
tukishiriki katika tuzo hizi na wasanii wetu wa filamu wamekuwa wakifanya
vizuri, lakini mwaka huu tunataka tufanye vizuri zaidi na tuwe washindi katika
Makundi mbalimbali ya tuzo hizo kwani uwezo tunao” alisema Maharage na
kusisitiza kuwa siri kubwa ni kuhakikisha watanzania kwanza wanawasilisha kazi
zao kwa wingi wakati huu na kisha wakati wa kupiga kura ukifika tuhakikishe
tunapigia kura kazi zetu na wasanii wetu.
Katika Msimu uliopita, Filamu
za Kitanzania ziliwika katika kundi la Filamu Bora kabisa Afrika Mashariki
ambapo “Aisha” ya Amil Shivji, “Naomba
Niseme” ya Staford Kihore, na
“Homecoming” ya Seko Shamte zilichaguliwa huku
“Siri ya Mtungi” ikijitokeza kwenye kundi la Filamu Bora za lugha ya
Kiswahili
Tanzania ina rikodi
nzuri kwenye tuzo hizi kwani misimu iliyopita filamu ya Kitendawili ya Richard
Mtambalike ilinyakua tuzo ya filamu bora ya lugha ya Kiswahili wakati Elizabeth
Michael ‘Lulu’ alivuma katika tuzo hizo katika filamu yake ya Mapenzi
iliyoteuliwa kuwa filamu bora kabisa Afrika Mashariki.
Tuzo hizi za AMVCAs
zinahusisha watengeneza filamu katika vipengele mbalimbali kuanzia uigizaji na
uongozaji mpaka uandishi na utengenezaji na mwaka huu, tuzo kadhaa katika
vipengele mbalimbali zitatolewa kuanzia kwenye uigizaji na uongozaji mpaka
uandishi na utengenezaji. Vipengele vingine vitahusisha: filamu fupi au video
za kwenye mtandao, muziki, ubunifu wa mavazi, sauti na mwanga kati ya vingi
vingine. Kwa 2018 kuna vipengele 27 kwa ujumla, ambapo 7 viko wazi kwa ajili ya
kura za watazamaji na 20 vitaamuliwa na jopo la majaji wenye uzoefu mkubwa
katika tasnia ya filamu ulimwenguni.
Kuingia AMVCAs ni bure
na tarehe ya kufungwa kwa maingizo ni 30 Aprili 2018. Filamu au sinema
zilizotayarishwa kwa ajili ya televisheni au tamthiliya za kwenye televisheni
ambazo ziliingizwa mwanzoni au kuteuliwa kwa ajili ya tuzo, au kutuzwa zawadi
katika shindano lingine la filamu na televisheni zinaruhusiwa kuingizwa kwenye
AMVCAs kama zinarushwa au kuoneshwa katika kipindi cha kuanzia Oktoba, 2016
hadi Machi, 2018.
Maelekezo ya kushiriki:
HATUA YA 1
Prepare a 2 to 3 minute
long showreel for your online submission. /Andaa ufupisho wa filamu yako wenye
muda wakati ya dakika 2 hadi 3 kwa ajili ya kuuwasilisha kwa njia ya mtandao
HATUA YA 2
Ingia www.africamagic.tv na uende kwenye ukurasa
wa kuwasilisha.
HATUA YA 3
Jaza fomu za
uwasilishaji na upandishe video yako. Namba ya kipekee ya utambulisho itatolewa
kwa kila ingizo la mtandaoni lililokamilika. Kisha kutegemea na eneo ulipo,
tuma ingizo lake akionesha namba zake za utambulisho.
Kwa maelezo zaidi juu ya
mahitaji ya kujiunga na taratibu za uwasilishaji, tafadhali ingia www.dstv.com
0 comments:
Post a Comment