“Jioni
hii nimepokea kwa mshtuko na huzuni kubwa taarifa za kifo cha Mkuu wa Mkoa
Mstaafu Dkt. Joel Nkaya Bendera, natoa pole kwa familia yake na wote walioguswa
na msiba huu na pia naungana nao katika kipindi hiki cha majonzi”
Hii
ni sehemu ya salamu za rambirambi za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli alizozitoa kufuatia kifo cha aliyekuwa Mkuu wa
Mkoa wa Manyara Dkt. Joel Nkaya Bendera kilichotokea jioni ya leo tarehe 06 Desemba,
2017 katika Hospitali ya Taifa Muhimbili Jijini Dar es Salaam alikofikishwa kwa
ajili ya kupata matibabu.
Mhe.
Rais Magufuli amesema Dkt. Joel Bendera atakumbukwa kwa mchango wake mkubwa
alioutoa kwa Taifa akiwa kiongozi katika nyadhifa mbalimbali zikiwemo Mkuu wa
Mkoa wa Manyara, Naibu Waziri na Mbunge na pia kwa mchango wake mkubwa katika
maendeleo ya michezo.
“Dkt.
Joel Nkaya Bendera alikuwa kiongozi shupavu, mahiri na mchapakazi, alipenda
kufanya kazi kwa ushirikiano na daima alitamani kupata mafanikio makubwa katika
majukumu aliyokuwa nayo, hakika tutamkumbuka” amesisitiza Mhe. Rais Magufuli.
Pamoja
na kutoa pole kwa familia ya marehemu, Mhe. Rais Magufuli amewapa pole wananchi
wa Mkoa wa Manyara ambako alikuwa Mkuu wa Mkoa hadi tarehe 26 Oktoba, 2017,
wananchi wa Mkoa wa Tanga ambako alikuwa Mbunge, wanachama wote wa Chama Cha
Mapinduzi (CCM), Wanamichezo wote na
wote walioguswa na msiba huu na amemuombea kwa Mwenyezi Mungu aipumzishe roho
yake mahali pema peponi, Amina.
0 comments:
Post a Comment