MKUU wa Wilaya ya Buhigwe mkoani Kigoma, Kanali Marco Gaguti (mwenye sare za JWT) akihojiana na mkazi wa Kijiji cha Kibande, wakati alipofanya ukaguzi wa kushtukiza katika maeneo ya mpaka wa Tanzania na Burundi.
Na Rhoda Ezekiel, Buhigwe
KATIKA hali ya kuhakikisha
mipaka ya nchi inakuwa salama na hakuna wageni wanaoingia nchini bila vibali na
kufuata utaratibu, Mkuu wa Wilaya Buhigwe mkoani Kigoma, Kanali Marco Gaguti amefanya
ukaguzi wa hali ya ulinzi na usalama wa mpaka wa Tanzania na Burundi.
Kanali Gaguti alifanya ukaguzi
huo hivi karibuni akiwa na wajumbe wa kamati ya Ulinzi na Usalama wa Wilaya
hiyo ambapo waliridhishwa na hali ya ulinzi
na usalama katika mpaka huo..
Gaguti na ujumbe wake walitembelea
vijiji vya Kibande,Nyamugali na Mnanila ambako aliambaa ambaa na ukingo wa Mto
malagarasi unaotengenisha nchi za Tanzania na Burundi kuona hali halisi ya
ulinzi na usalama na kuona hali ya usafirishaji wa bidhaa za magendo kupitia
maeneo hayo.
Akizungumza na waandishi wa
habari majira ya saa tisa alfajiri baada ya kukamilisha zoezi hilo Mkuu huyo wa
wilaya alisema kuwa ulinzi shirikishi uliowekwa kuanzia ngazi za vitongoji na
uelimishaji jamii kuhusu hatua za kuimarisha ulinzi maeneo ya mpakani imekuwa
na mafanikio makubwa na kwamba ofisi yake itaendelea kusimamia hali hiyo kuhakikisha
ulinzi na usalama wakudumu unakuwepo wakati wote.
Sambamba na kuangalia hali ya
ulinzi na usalama pia zoezi hilo lilihusisha upekuzi katika baadhi ya nyumba
zilizokuwa zinahisiwa kuhifadhi wahamiaji haramu na kutembelea maeneo ya mpaka
ambayo yanatuhumiwa kwa usafirishaji wa bidhaa za magendo kwenda nchini Burundi
na zinazotoka huko kuingia mkoani Kigoma.
Mkuu huyo wa wilaya alisema
kuwa amekuwa akifanya ukaguzi huo mara kwa mara na kwamba mafanikio ni makubwa
ingawa alikiri kuwepo kwa changamoto ya baadhi ya wananchi na viongozi wa
vijiji katika maeneo hayo ya mpakani kushirikiana na wahalifu kutenda makosa ya
uingizaji wa bidhaa zamagendo na wahamiaji haramu.
Kwa upande wake Mkurugenzi
Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya Buhigwe, Anosta Nyamoga alisema kuwa zoezi la
ukaguzi wa mpaka wakati wa usiku limesaidia kupunguza vitendo vya usafirishaji
wa bidhaa mbalimbali hasa mazao kwenda nchini Burundi bila kulipiwa ushuru.
Mkurugenzi huyo alisema kuwa
vitendo vya usafirishaji wa mazao na bidhaa bila kulipiwa ushuru vimekuwa vikiiokosesha
mapato halmashauri yake na kwamba mkakati wa kuziba mianya ya upotevu huo wa
mapato ya serikali inaendelea kufanyiwa kazi.
0 comments:
Post a Comment