Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipa Kodi kutoka TRA Richard Kayombo
akizungumza na waandishi wa habari kuhusu semina kwa jumuiya ya
wafanyabiashara wa china itakayofanyika tarehe 25 Novemba 2016, leo
jijini Dar es Salaam.Katikati ni Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya
Jiteng Consultancy Limited Bw. Andrew Huong na Meneja Msaidizi wa
Kampuni hiyo Bw. Wesley Huung (kushoto). Picha na Frank Shija – MAELEZO.
**************
Na Amina Kibwana,Globu ya Jamii
Mamlaka ya mapato Tanzania (TRA) kwa kushirikiana na Ubalozi wa china
hapa nchini ,imeandaa semina kwa ajili ya jumuiya ya wafanyabiashara wa
China kwa lengo la kuwaelimisha juu ya masuala mbalimbali ya ulipaji
kodi.
Semina hiyo inayotarajiwa kufanyika Novemba 25 katika ukumbi wa Benki kuu ya Tanzania (BoT), inatarajiwa
kufunguliwa na Waziri wa Biashara na viwanda Mh. Charles Mwijage pamojana na Balozi wa China hapa nchini.
Akizungumza na waandishi wa habari Mkurugenzi wa
huduma na elimu kwa walipakodi wa TRA, Richard Kayombo amesema, semina
hiyo itawawezesha wafanyabiashara wa china kutimiza na kuzingatia
sheria za kutoza kodi sahihi na kukokotoa kodi ya Zuio katika bidhaa na
huduma na hivyo kuongeza ulipaji kodi kwa hiari miongoni mwao.
Kayombo amesema, katika semina hiyo mada mbalimbali zitawakilishwa
zikiwa ni pamoja na Mabadiliko ya Bajeti ya 2016/17,Masuala ya Forodha
na uondoshaji wa bidhaa, Kodi ya Zuio hususan katika sekta ya ujenzi na
kodi ya Ajira, ambapo pia wafanyabiashara watapata fursa ya kuuliza
maswali ili kuwawezesha kufanya shughuli zao kwa mujibu wa sheria na
taratibu za nchi.
Kwa upande wake Mratibu wa
wafanyabiashara wa China, Andrew Huang amesema, Semina hiyo itawasaidia
katika kuendelea kutekeleza wajibu wao na kuhakikisha wanalipa kodi
inayostahili kutokana na shughuli zao wanazozifanya hapa nchini.
"Tunashukuru sana TRA kwa kushirikiana nasi katika kutoaji wa elimu hii
kwetu, kwani kwa kufanya hivyo ni dhahiri kwamba wanatukumbuka na
kutujali nasi tutaonyesha ushirikiano kwa kuendelea kulipa kodi
inayostahili."
Ikiwa ni semina ya 15 tangu kuanza kwa
semina kati ya mamlaka ya Mapato Tanzania na Ubalozi wa china,TRA imekuwa
ikiendesha semina mbalimbali kwa wachina kuhusu masuala ya kodi kwa
maombi au kutokana na mipango ya TRA kuelimisha makundi mbalimbali ya
walipa kodi ili kuongeza uelewa wa Masuala ya Kodi hapa nchini.
0 comments:
Post a Comment