Waziri wa Ujenzi,
Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa akisisitiza jambo kwa Menejimenti
na Wafanyakazi wa Shirika la Ndege Tanzania (ATCL), katika mkutano uliofanyika jijini
Dar es Salaam.
Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Ndege Tanzania (ATCL), Eng. Ladislaus
Matindi akitoa ufafanuzi kwa Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof.
Makame Mbarawa (hayupo pichani), wakati Waziri huyo alipokutana na menejimenti
ya shirika hilo pamoja na wafanyakazi wake jijini Dar es Salaam.
Wafanyakazi wa Shirika la Ndege Tanzania (ATCL), wakimsikiliza Waziri
wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa (hayupo pichani), alipozungumza
na uongozi wa Shirika hilo na Wafanyakazi jijini Dar es Salaam. BOFYA ⇝HAPA KUSOMA ZAIDI
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa
akimpongeza mmoja wa watoa huduma wa ndege za ATCL kwa utoaji wa huduma bora
kwa wateja katika mkutano uliofanyika jijini Dar es Salaam.Picha zote na Benjamin Sawe-Maelezo
Waziri wa Ujenzi,
Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa ametoa muda wa mwezi mmoja kwa Mkurugenzi
Mkuu wa Shirika la Ndege Tanzania (ATCL), kufanya mabadiliko katika menejimenti
ya Shirika hilo ili kuongeza ufanisi na kuboresha utendaji kazi.
Ametoa agizo hilo
jijini Dar es Salaam alipokuwa akizungumza katika mkutano wa Menejimenti pamoja
na wafanyakazi wa Shirika hilo na kuwataka kutoa huduma bora ili kulifanya
Shirika hilo kuwa miongoni mwa mashirika bora ya ndege barani Afrika.
“Nataka ndani ya mwezi
mmoja uwe umeshafanya mabadiliko katika menejimenti, mabadiliko lazima yaanzie
juu kwanza kwa watoa maamuzi na ishuke hadi kwa wafanyakazi wazembe na wasio
waadilifu”, amesema Waziri Prof. Mbarawa.
Waziri Mbarawa
amepinga nyongeza ya mshahara kwa wafanyakazi wa Shirika hilo hasa katika
kipindi hiki ambacho Serikali ipo katika juhudi za kulifufua na kuliimarisha
Shirika hilo.
Aidha Waziri Mbarawa
ameitaka Idara ya Masoko ya shirika hilo kuzunguka katika taasisi zote zilizo
chini ya Wizara yake na kuzishawishi kuweza kutumia huduma za usafiri wa anga
wa ATCL.
“Serikali imekamilisha
upande wake wa ununuzi wa ndege, sasa kazi inabaki kwenu, sitaki watu wa masoko
kukaa ofisini”, amesema Prof. Mbarawa.
Ameongeza kuwa wafanyakazi
wa ATC wanatakiwa kujipanga kutoa huduma iliyotukuka kwa wateja wake ili kuweza
kuhimili ushindani uliopo katika mashirika ya ndege nchini.
“Inabidi tofauti kubwa
ionekane kati yenu na mashirika mengine, yeyote ambaye anaona hawezi kutoa
huduma bora kwa mteja atafute sehemu nyingine kwani hapa hatufai ”, amesisitiza
Waziri Mbarawa.
Profesa Mbarawa
amelitaka shirika hilo kutumia mfumo wa kisasa wa kukata tiketi kwa njia ya
simu na kompyuta ili kuwarahishia watumiaji wa shirika hilo kuweza kupata tiketi
kwa haraka na urahisi.
Kwa upande wake,
Mkurugenzi Mkuu wa Shirika hilo Eng. Ladislaus Matindi amemhakikishia Waziri
Mbarawa kufanyia kazi maagizo aliyotoa na kuahidi kuboresha utendaji kazi wa shirika hilo kwa lengo la kuteka soko la
ushindani wa usafiri wa anga nchini.
“Kwa sasa tumeanza
vizuri na naamini uwezo wa kuzalisha faida zaidi tunao, tunaahidi kuboresha
utendaji kazi ili kuendana na kasi ya mabadiliko ya Serikali ya Awamu ya Tano”,
amesema Eng. Matindi.
Imetolewa
na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na
Mawasiliano
0 comments:
Post a Comment