Mkuu wa Wilaya
ya Handeni Bw.Godwin Gondwe (pichani) amepiga marufuku wananchi wa wilaya yake kucheza
mchezo wa bao na "pool table" wakati wa mchana muda ambao ni wa
kufanya kazi ili kutekeleza falsafa ya Serikali ya Awamu ya Tano ya "Hapa
kazi Tu". Anaandika Abushehe
Nondo -MAELEZO.
Gondwe alitoa
kauli hiyo hivi karibuni jijini Dar es Salaam wakati akizungumzia mambo
mbalimbali yanayohusu wilaya yake ya Handeni ambapo alisema katika wilaya hiyo
baadhi ya vijana hawana muamko wa kufanya kazi badala yake wamekua wakijishughulisha
na kucheza bao na "pool table" vitu ambavyo haviwaletei maendeleo.
"Nimekataza
vijana katika wilaya yangu kucheza michezo ya bao na "pool table"
wakati wa kazi na nimewahamasisha kushiriki shughuli za ufugaji na kilimo kwa
ajili ya kujiletea maendeleo na kuondokana na hali ya umasikini" alisema
Gondwe.
Mkuu huyo wa
Wilaya aliwashauri wakazi wa Handeni kujishughulisha na kilimo cha mazao
mbalimbali ya biashara ikiwemo alizeti, ufuta na ufugaji wa mbuzi na
kuku ili waweze kujipatia fedha zitakazowasaidia kujikimu kimaisha.
Pia Gondwe
alisema kuwa wamekubaliana na Idara ya Ardhi wilayani humo kutenga maeneo
maalum ya uwekezaji kwa vijana ambapo Serikali itawawezesha kwa ajili ya
kufanya shughuli mbalimbali za kilimo.
Amewataka vijana
kujiunga katika vikundi waweze kupatiwa fedha ambazo kila Halmashauri
imetenga kwa ajili ya vijana na wanawake na watumie mikopo hiyo
kujikwamua kimaisha kwa kufanya shughuli za ujasiliamali.
Akizungumzia
tatizo la ukosefu wa maji katika baadhi ya maeneo ya wilaya hiyo, Gondwe
alisema bado anaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali kuhakikisha
tatizo la maji wilayani Handeni linapungua ili wananchi waweze kuondokana
na adha hiyo ambayo inawakabili kwa muda mrefu.
Alisema wananchi
wa Handeni hasa wanawake wanapata tabu ya kutafuta maji safi na
salama ingawa Serikali bado inaendelea kushirikiana na wadau wa maendeleo
kuhakikisha wananchi wake wanapata huduma hiyo kwa uhakika.
0 comments:
Post a Comment