Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter MuhongoTeresia Mhagama na Mohamed Saif
Benki ya Dunia (WB) imeahidi kutoa Dola za Marekani milioni 4 sawa na
zaidi ya shilingi Bilioni 8, kwa ajili ya Ruzuku katika shughuli za uchimbaji mdogo wa madini
nchini.
Hayo yamebainishwa hivi karibuni jijini Dar es Salaam na Waziri wa
Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo mara baada ya kumaliza kikao na
watendaji Wakuu wa Benki ya Dunia wanaosimamia Miradi ya Sekta ya Madini.
Profesa Muhongo alisema kuwa sehemu ya fedha hizo za Ruzuku ambayo ni
ya Awamu ya Tatu zitatolewa mwezi Septemba, 2016.
Aliongeza kuwa fedha hizo zitatumika kufadhili uendelezaji wa vituo
Saba vya mfano vya utafutaji na uchimbaji mdogo wa madini ambavyo vitachaguliwa
na Wizara baada ya kufanya tathmini ya maeneo yanayoweza kuwekwa vituo hivyo. BOFYA HAPA KUPATA HABARI ZAIDI
“Sio hivyo tu, Fedha hizi za Benki ya Dunia zinalenga kuwafadhili
wanawake kwenye shughuli za uchimbaji mdogo wa madini, ukataji na uchongaji wa
madini ya vito ili idadi ya wanawake wanaojishughulisha na Sekta ya Madini iongezeke,”
alisema Profesa Muhongo.
Aidha, Profesa Muhongo alitoa wito kwa wataalam wote wanaosimamia
miradi inayofadhiliwa na Benki ya Dunia katika Sekta ya Madini kuhakikisha kuwa
utekelezaji wa miradi hiyo uende kwa kasi ili kuleta matokeo yaliyotarajiwa.
Benki ya Dunia kupitia Wizara ya Nishati na Madini imeendelea kutoa Ruzuku
katika Uchimbaji madini mdogo ambapo katika mwaka wa Fedha 2015/16 zilitengwa
takribani Shilingi bilioni 7.2 ambazo zilitolewa kwa vikundi 111 vya wachimbaji
wadogo na watoa huduma mbalimbali katika sekta ya uchimbaji madini mdogo.
Vilevile, katika mwaka wa Fedha 2013/2014, Fedha za Ruzuku zilizotolewa
kwa Wachimbaji Wadogo zilikuwa ni Dola za Marekani 500,000 sawa na takribani
Shilingi Bilioni 1 zilizotolewa kwa waombaji 11. Fedha hizi ziliwalenga
wachimbaji madini wadogo pekee tofauti na awamu zilizofuata.
Utoaji huo wa Ruzuku unaenda sambamba na utoaji wa elimu na mafunzo kwa
wachimbaji wadogo wa madini waliopata ruzuku husika ili kuhakikisha kuwa
shughuli zilizopata ufadhili zinaleta tija.
0 comments:
Post a Comment