Nafasi Ya Matangazo

May 05, 2016

Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii,Meja Jenerali Gaudence Milanzi akikagua gwaride maalum la wahitimu wa Mafunzo ya Mabadiliko ya Mfumo wa utendaji kazi wa kiraia kuwa Jeshi Usu kwa Wahifadhi za Taifa (TANAPA) yaliyofanyika kambi ya mafunzo Mlele mkoani Katavi juzi.
Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii,Meja Jenerali Gaudence Milanzi akipongezana na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA) Allan Kijazi mara baada ya kufunga Mafunzo ya Mabadiliko ya Mfumo wa utendaji kazi wa kiraia kuwa Jeshi Usu kwa Wahifadhi na askari waajiriwa wa Shirika la Hifadhi za Taifa yaliyofanyika kambi ya Mafunzo Mlele mkoani Katavi. 
Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Hifadhi za Taifa nchini (TANAPA) Allan Kijazi (kulia) akimuongoza Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii,Meja Jenerali Gaudence Milanzi kuelkea katika uwanja wa Mafunzo katika kambi ya Mlele kwa ajili ya kufunga Mafunzo ya Wahifadhi na Askari wapya waajiriwa wa shirika hilo . BOFYA HAPA KUSOMA ZAIDI

Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii,Meja Jenerali Gaudence Milanzi akipiga saluti wakati akipokea salamu za heshima wakati wa gwaride maalumu la ufungaji wa mafunzo ya awamu ya  mabadiliko ya mfumo wa utendaji kazi wa kiraia kuwa mfumo wa jeshi usu.
Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii,Meja Jenerali Gaudence Milanzi akipokea heshima ya saluti wakati akikagua gwaride la heshima la askari wapya na Wahifadhi waliohitimu mafunzo ya awamu ya kwanza ya mabadiliko ya mfumo wa utendaji kazi wa kiraia kuwa mfumo wa jeshi usu yaliyofanyika katika kituo cha mafunzo Mlele mkoani Katavi.

Askari waajiriwa wa Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA) wakipita mbele ya mgeni rasmi (hayupo pichani)  kwa mwendo wa pole na kutoa heshima wakati  ufungaji wa mafunzo ya mfumo wa jeshi usu kwa Wahifadhi 
Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii,Meja Jenerali Gaudence Milanzi akipiga saluti wakati gwarde likipita mbele ya jukwaa na kutoa heshima,wengine kutoka kushoto ni Kaimu Mkurugenzi wa Mamlaka ya Wanyamapori ,Martin Loibooki,Mkuu wa Mkoa wa Katavi,Meja Jenerali Mstaafu,Raphael Muhuga,Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Hifadhi za Taifa,Allan Kijazi,Kaimu Mkurugenzi idara ya Wanyama pori,Ndugu Karamaga.
Askari waajiriwa wa Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA) wakipita mbele ya mgeni rasmi (hayupo pichani)  kwa mwendo wa haraka wakati  ufungaji wa mafunzo ya mfumo wa Jeshi Usu kwa Wahifadhi 
Askari wapya waajiriwa wa Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA) wakionesha umahiri katika kutumia silaha wakati wa kukabiliana na majangili mara baada ya kupata mafunzo hayo katika kambi ya Mlele iliyopo mkoani Katavi. 
Baaadhi ya Wahifadhi Waandamizi na Wafawidhi wakiwa wameshika silaha mara baada ya kupatiwa Mafunzo katika Kambi ya Mlele ikiwa ni sehemu ya mabadiliko ya mfumo wa utendaji kazi wa kiraia kwenda Jeshi Usu. 
Askari wa Hifadhi akionesha umahiri katika matumizi ya silaha kwa kulenga shabaha wakati wa kuhitimu mafunzo ya  awamu ya kwanza ya mabadiliko ya mfumo  wa utendaji kazi wa kiraia kuwa mfumo wa jeshi usu yaliyofanyika katika kituo cha mafunzo Mlele mkoani Katavi
Baadhi ya Viongozi na Wageni katika hafla ya ufungaji wa Mafunzo ya Mfumo wa Jeshi Usu kwa Wahifadhi na askari waajiriwa wakifuatilia maonesho yaliyokuwa yakifanywa na wahitimu hao.
Meneja Mawasiliano wa Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA) Pascal Shelutete (kulia) akiratibu shughuli mbalimbali zilizokuwa zikiendelea katika hafla ya ya ufungaji wa Mafunzo ya Mfumo wa Jeshi Usu kwa Wahifadhi na Asakari Waajiriwa .kushoto ni Mkuu wa Mafunzo ,Genes Shayo .
Mhifadhi Sekela Mwangota akisoma risala  ya Wahitimu wa Mafunzo ya Mfumo wa Jeshi Usu kwa mgeni rasmi ,Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii,Meja Jenerali Gaudence Milanzi (hayupo pichani) wakati wa kuhitimisha mafunzo hayo kwa wahifadhi na askari wapya waaajiriwa wa shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA) yaliyofanyika kwenye kambi ya Mafunzo Mlele mkoani Katavi.
Kaimu Mkurugenzi wa Mamlaka ya Wanyamapori,Martin Loibooki akizungumza wakati wa hafla ya ya ufungaji wa Mafunzo ya Mfumo wa Jeshi Usu kwa Wahifadhi na Asakari Waajiriwa .
Baadhi ya Wahitimu.
Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA) Allan Kijazi akizungumza wakati waa hafla ya ya ufungaji wa mafunzo ya mfumo wa Jeshi Usu kwa Wahifadhi na Askari Waajiriwa .
Mkuu wa Mkoa wa Katavi,Meja Jenerali Mstaafu ,Raphael Muhuga akizungumza hafla ya ya ufungaji wa Mafunzo ya Mfumo wa Jeshi Usu kwa Wahifadhi na Askari Waajiriwa ambapo amegusia juu ya changamoto iliyopo kwa Wafugaji kuingiza Mifugo yao katika Hifadhi pamoja na mapori ya Akiba.
Katibu Mkuu ,Wizara ya Maliasili na Utalii,Meja Jenerali Gaudence Milanzi akitoa hotuba yake ya kuhitimisha Mafunzo ya Mfumo wa Jeshi Usu kwa Wahifadhi na Askari waajiriwa wa Shirika la Hifadhi za Taifa nchini (TANAPA),Mafunzo yaliyofanyika katika kambi ya Mlele mkoani Katavi.
Baadhi ya Askari Waliohitimu.
Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii,Meja Jenerali Gaudence Milanzi akitunuku vyeti kwa Wahitimu wa Mafunzo ya Mfumo wa Jeshi Usu kwa Wahifadhi za Taifa(TANAPA) yaliyofanyika kambi ya mafunzo Mlele mkoani Katavi.
******************
Na Mwandishi Wetu,Katavi.
WIZARA ya Maliasili na Utalii  imeridhia maombi ya Shirika la Hifadhi la Taifa (TANAPA) kubadili mfumo wa utendaji kazi kutoka ule wa kiraia na kuwa jeshi usu (Paramilitary) ili kukabiliana  na tatizo sugu la ujangili wa wanyamapori ,misitu, na rasilimali nyingine za nchi.

Akizungumza wakati akifunga mafunzo ya askari na wahifadhi, wa shirika hilo Katibu Mkuu wa Wizara  hiyo Meja Jenerali Gaudence Milanzi alisema maombi ya shirika hilo kutaka kubadilishwa na kuendeshwa kwa sheria za kijeshi ni ya msingi katika kipindi hiki ambacho Tanzania inakabiliwa na tatizo sugu la ujangili wa wanyamapori.

Ufungaji wa mafunzo hayo ulifanyika  juzi katika kambi Mlele ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Katavi iliyopo katika mkoa mpya wa Katavi Magharibi mwa Tanzania ambapo jumla askari 101 na wahifadhi 26  walihitimu mafunzo ya kijeshi ya miezi 3 na 6 kwa pamoja.

“Kwa sasa uhifadhi unakabiliwa na changamoto kubwa ya ujangili,hususan Tembo na Farukuporomoka kwa maadili ya askari na uingizaji wa mifugo hifadhini”alisema.

Aliongeza:“Maombi yenu yamekuja kwa wakati muafaka hivyo tutawasilisha katika mamlaka nyingine za juu za kiserikali, ili yatungiwe sheria na hatimaye kuwasilishwa bungeni ili  yajadiliwe na kupitishwa kuwa sheria”.

Hata hivyo  aliwataka askari hao pamoja na menejimenti ya ya TANAPA kufanya maandalizi ya kutosha kwa msingi kuwa sheria itakapopitishwa  baadhi ya mambo yatabadilika na kuendeshwa kwa mujibu wa taratibu za kijeshi kwa ilivyo kwa majeshi mengine nchini.

“Katika mambo ya msingi  mabadiliko hayo yatakapofanyika, ni pamoja na kuzingatia suala nidhamu kwa askari,uwajibikaji na kuepuka kujihusisha na masuala ya vyama vya wafanyakazi na pia kuhukumiwa  au kuadhibiwea katika mahakama  maalamu ya kijeshi (Court martial) pale askari atakapokiuka taratibu za kijeshi”aliongeza Meja Jenerali Milanzi.

Awali akiwasilisha maombi hayo Mkurugenzi wa TANAPA Allan Kijazi alisema shirika lake baada ya kutafakari kwa kina wakitumia wataalamu wa ndani ya shirika walibaini umuhimu wa askari wao kutumia sheria za kijeshi kutokana na changamoto ya sasa ya katika masuala ya uhifadhi.

“Askari wetu wanapewa  mafunzo  ya kivita  na pia silaha za kivita katika doria ili kukabiliana na majangili, lakini wanapotimiza wajibu wao wamekuwa  wakikabiliwa na changamoto ya kutotambuliwa na sheria za nchi na mara nyingi wamejikuta katika matatizo”alisema Kijazi.

Akitoa mfano alisema mara nyingi yanapotokea mapambano ya kati askari wetu na majangili  ndani ya hifadhi, na yakajitokeza madhara sheria zilizopo haziwalindi askari pale matumizi ya silaha zilizotumika zinavyoanishwa kisheria.

“Itambulike kuwa kwa sasa majangili hasa wanaoua Tembo wanatumia silaha za kisasa, teknolojia ya kisasa pamoja na mitandao ya kupashana habari hivyo bila kubadilisha mbinu si rahisi kukabiliana nao”alisema Mkurugenzi huyo.
  
Alisema lengo la mafunzo hayo ya kijeshi kufanyika ni pamoja na kuwajengea uwezo askari kuwa wakakamavu na kufikia maeneo hatarishi ndani ya hifadhi wakati wakiwa doria na pia kukabiliana na majangili  kwa mbinu za kisasa za kijeshi.

Aliongeza kuwa mafunzo hayo ambayo ni ya tatu kufanyika yataendelea kwa watumishi wa idara zote za shirika hilo wakiwemo maafisa wajuu ili kila moja awajibike  na kwenda na kasi ya serikali ya awamu tano ambayo inasisistiza  watumishi wa umma kufanya kazi kwa weledi na uaminifu.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Katavi Meja Jenerali Mstaafu Raphael  Muhuga  alielezea umuhimu wa kutunza maeneo yaliyohifadhiwa nchini huku akionya kuwa makundi ya wafugaji yanayovamia maeneo hayo lazima yaondolewe haraka.

“Mkoani kwangu Katavi tumefanya tathamini na kugundua kuwa kuna mifugo 800,000  imevamia mapori ya akiba na hifadhi ya Taifa ya Katavi hivyo  tatafanya opresheni maalumu ya kuwaondoa ndani ya muda mfupi ujao”alionnya Mkuu huyo wa Mkoa.

Aliongeza:”Tutawatumia askari hawa hawa   waliohitimu kufanya kazi hiyo, na operesheni hii itakuwa ya kudumu,  na katika hili hatutavumilia  wanasiasa kutuingilia katika utendaji  na utekelezaji wa  majukumu ya kiserikali,”  

Mafunzo hayo ya kijeshi  ni ya tatu kwa askari na watumishi wa shirika hilo ambalo linasimamia  hifadhi 16 katika maeneo mbalimbali nchini.
Posted by MROKI On Thursday, May 05, 2016 No comments

0 comments:

Post a Comment

  • Facebook
  • Twitter
  • Youtube

Labels

Blog Archive

Nafasi Ya Matangazo