Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter
Muhongo (katikati) akiwa katika kikao na watendaji wa kampuni ya Tanzgraphite
(TZ) inayofanya utafiti wa madini ya graphite katika eneo la Epanko wilaya ya Ulanga mkoani
Morogoro.Kutoka kulia kwa Waziri, ni
watendaji wa kampuni hiyo, Jacka Mwambi,
Grant Pierce, Nassoro Soud,
Mariam Mavura na Sauda Simba.Kulia ni watendaji wa Wizara ya Nishati na
Madini.
****************
Na Teresia Mhagama
Waziri wa Nishati na
Madini Profesa Sospeter Muhongo ameeleza kuwa Serikali inatoa kipaumbele katika
uchimbaji wa madini ya graphite nchini kutokana na umuhimu wake duniani ikiwemo
kutumika kama malighafi ya kutengenezea betri za simu, penseli na kompyuta
mpakato.
Aliyasema hayo wakati
alipokutana na kampuni ya Tanzgraphite (TZ) ambayo ni kampuni tanzu ya Kibaran
Resources inayofanya utafiti wa madini hayo kutoka mwaka 2012 katika eneo la Epanko wilaya ya Ulanga mkoani
Morogoro. BOFYA HAPA KUSOMA ZAIDI.
Profesa Muhongo alisema
kuwa madini hayo yana soko kubwa duniani
kwani hutumika pia katika utengenezaji wa vilainishi mbalimbali.Profesa Muhongo
alitoa kauli hiyo baada ya Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni hiyo, Jacka Mwambi
kumueleza Waziri Muhongo kuwa kampuni hiyo imepanga kuanza uzalishaji wa madini hayo mwaka 2017
lakini ili kutekeleza sula hilo kwa ufanisi wanahitaji msaada serikalini
ikiwemo wa ujenzi wa kituo cha kupoozea umeme cha Ifakara kitakachowasaidia kupata
umeme wa uhakika katika eneo la
uzalishaji.
Alisema kuwa pia
wanaiomba Serikali kukamilisha ujenzi
wa daraja litakalokatisha mto Kilombero ambalo litawapa uhakika wa usafirishaji
wa madini hayo tofauti na kivuko kinachotumika sasa.
“ Changamoto nyingine ni
baadhi ya wananchi wanaozunguka eneo hilo la uchimbaji ambao wanaonekana
kutokukubaliana na mradi kufanyika katika eneo husika, tumejaribu kujadiliana
nao kwa kuhusisha ngazi mbalimbali za
uongozi lakini bado kuna changamoto ya mawasiliano chanya kati ya kampuni na
wananchi,” alisema Jacka Mwambi.
Akizungumzia uchimbaji
wa madini ya graphite duniani, Mwambi alisema kuwa kwa sasa nchi
za China, Brazili na India ndizo zinaongoza kwa usambazaji wa madini
hayo ambapo kwa wanazalisha tani milioni
1.2 kwa mwaka .
Alisema kuwa kwa Afrika
nchi ya Msumbiji imeonekana kuwa na mashapo mengi na kueleza kuwa endapo
Tanzania itafanikiwa kuchimba madini hayo katika eneo la Epanko itaifanya nchi
kuwa mzalishaji mkubwa wa madini hayo barani Afrika.
Alisema kuwa gharama ya
uendeshaji wa mradi huo wa Epanko itakuwa ni Dola za Marekani milioni 77.5 na
uhai wa mgodi unatarajiwa kuwa miaka 25.
Alisema faida
zitakazotokana na uzalishaji wa madini hayo wilayani Ulanga ni pamoja na ajira
1500 za moja kwa moja huku akieleza kuwa
ajira zisizo za moja kwa moja zitaongezeka mara sita zaidi ya zile za
moja kwa moja, pia wafanyakazi katika kampuni hiyo wenye ujuzi na wasio na ujuzi watapatiwa
mafunzo ya kuwaendeleza.
Mwambi aliongeza kuwa
mgodi huo unatarajia kulipa mrabaha wa Dola za Marekani 32,760,000 na kodi ya
Dola za Marekani 126,945,000 katika kipindi
cha uhai wa mgodi.
Kuhusu changamoto ya
wananchi kuchelewesha utekelezaji wa mradi huo, Profesa Muhongo ametuma timu ya
wataalam kutoka Wizara ya Nishati na Madini kwenda katika eneo hilo kuzifahamu
changamoto hizo kwa undani na kuwasilisha kwake ripoti siku ya Ijumaa tarehe 8
saa nne Asubuhi.
Alieleza kuwa Wizara
inataka kuona mgogoro huo unamalizika ili uzalishaji uanze kwani soko la madini
hayo duniani ni kubwa.
“Ni lazima kama Serikali
tuhakikishe kuwa migogoro katika sehemu za migodi inamalizika kwani ni jukumu
letu kuhakikisha kuwa tunatoa leseni katika sehemu ambazo mwekezaji ataweza
kuchimba madini husika ili tusije kulaumiwa kuwa tumetoa leseni katika sehemu
ambayo hairuhusu uchimbaji madini,” alisema Profesa Muhongo.
0 comments:
Post a Comment