Nafasi Ya Matangazo

April 05, 2016

Waziri  wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo (katikati) akiwa katika kikao na watendaji wa kampuni ya Tanzgraphite (TZ) inayofanya utafiti wa madini ya graphite katika  eneo la Epanko wilaya ya Ulanga mkoani Morogoro.Kutoka  kulia kwa Waziri, ni watendaji wa kampuni hiyo, Jacka Mwambi,  Grant Pierce, Nassoro Soud,  Mariam Mavura na Sauda Simba.Kulia ni watendaji wa Wizara ya Nishati na Madini.
****************
Na Teresia Mhagama
Waziri wa Nishati na Madini Profesa Sospeter Muhongo ameeleza kuwa Serikali inatoa kipaumbele katika uchimbaji wa madini ya graphite nchini kutokana na umuhimu wake duniani ikiwemo kutumika kama malighafi ya kutengenezea betri za simu, penseli na kompyuta mpakato.

Aliyasema hayo wakati alipokutana na kampuni ya Tanzgraphite (TZ) ambayo ni kampuni tanzu ya Kibaran Resources inayofanya utafiti wa madini hayo kutoka mwaka  2012 katika eneo la Epanko wilaya ya Ulanga mkoani Morogoro. BOFYA HAPA KUSOMA ZAIDI.
Profesa Muhongo alisema kuwa madini hayo yana soko kubwa  duniani kwani hutumika pia katika utengenezaji wa vilainishi mbalimbali.Profesa Muhongo alitoa kauli hiyo baada ya Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni hiyo, Jacka Mwambi kumueleza Waziri Muhongo kuwa kampuni hiyo imepanga  kuanza uzalishaji wa madini hayo mwaka 2017 lakini ili kutekeleza sula hilo kwa ufanisi wanahitaji msaada serikalini ikiwemo wa ujenzi wa kituo cha kupoozea umeme cha Ifakara kitakachowasaidia kupata umeme wa uhakika  katika eneo la uzalishaji.

Alisema kuwa pia wanaiomba Serikali kukamilisha   ujenzi wa daraja litakalokatisha mto Kilombero ambalo litawapa uhakika wa usafirishaji wa madini hayo tofauti na kivuko kinachotumika sasa.

“ Changamoto nyingine ni baadhi ya wananchi wanaozunguka eneo hilo la uchimbaji ambao wanaonekana kutokukubaliana na mradi kufanyika katika eneo husika, tumejaribu kujadiliana nao  kwa kuhusisha ngazi mbalimbali za uongozi lakini bado kuna changamoto ya mawasiliano chanya kati ya kampuni na wananchi,” alisema Jacka Mwambi.

Akizungumzia uchimbaji wa madini ya graphite duniani, Mwambi alisema kuwa  kwa sasa nchi  za China, Brazili na India ndizo zinaongoza kwa usambazaji wa madini hayo ambapo  kwa wanazalisha tani milioni 1.2 kwa mwaka .

Alisema kuwa kwa Afrika nchi ya Msumbiji imeonekana kuwa na mashapo mengi na kueleza kuwa endapo Tanzania itafanikiwa kuchimba madini hayo katika eneo la Epanko itaifanya nchi kuwa mzalishaji mkubwa wa madini hayo barani Afrika.

Alisema kuwa gharama ya uendeshaji wa mradi huo wa Epanko itakuwa ni Dola za Marekani milioni 77.5 na uhai wa mgodi unatarajiwa kuwa miaka 25.

Alisema faida zitakazotokana na uzalishaji wa madini hayo wilayani Ulanga ni pamoja na ajira 1500 za moja kwa moja huku akieleza kuwa  ajira zisizo za moja kwa moja zitaongezeka mara sita zaidi ya zile za moja kwa moja, pia wafanyakazi katika kampuni hiyo  wenye ujuzi na wasio na ujuzi watapatiwa mafunzo ya kuwaendeleza.

Mwambi aliongeza kuwa mgodi huo unatarajia kulipa mrabaha wa Dola za Marekani 32,760,000 na kodi ya Dola za Marekani 126,945,000  katika kipindi cha uhai wa mgodi.

Kuhusu changamoto ya wananchi kuchelewesha utekelezaji wa mradi huo, Profesa Muhongo ametuma timu ya wataalam kutoka Wizara ya Nishati na Madini kwenda katika eneo hilo kuzifahamu changamoto hizo kwa undani na kuwasilisha kwake ripoti siku ya Ijumaa tarehe 8 saa nne Asubuhi.

Alieleza kuwa Wizara inataka kuona mgogoro huo unamalizika ili uzalishaji uanze kwani soko la madini hayo duniani ni kubwa.


“Ni lazima kama Serikali tuhakikishe kuwa migogoro katika sehemu za migodi inamalizika kwani ni jukumu letu kuhakikisha kuwa tunatoa leseni katika sehemu ambazo mwekezaji ataweza kuchimba madini husika ili tusije kulaumiwa kuwa tumetoa leseni katika sehemu ambayo hairuhusu uchimbaji madini,” alisema Profesa Muhongo.
Posted by MROKI On Tuesday, April 05, 2016 No comments

0 comments:

Post a Comment

  • Facebook
  • Twitter
  • Youtube

Labels

Blog Archive

Nafasi Ya Matangazo