Rebeca Semoka akiwa ofisini kwake Kiwanda cha Bia Ilala, Dar es Salaam.
Rebecca akionyesha umakini katika kuonja bia kiwandani hapo
***************
Mfanyakazi wa kampuni ya Bia
Tanzania katika kiwanda cha Ilala kilichopo jijini Dar es Salaam Rebecca
Semoka, ameshinda tuzo ya kuwa muonjaji bora wa bia kutoka barani Afrika,
katika shindano la kuonja vinywaji lililoandaliwa na kampuni ya SABMiller na kushirikisha
wafanyakazi wake wenye utaalamu wa kuonja vinywaji kutoka kwenye viwanda vyake
vilivyopo sehemu mbalimbali duniani .
Rebecca ameweza kuwa
mwonjaji bora wa bia kutoka barani Afrika katika shindano hilo ambalo
hufanyika kila mwaka chini ya usimamizi wa kampuni ya kimataifa AROXA
inayoshughulika na usimamizi wa ubora wa bidhaa zinazozalishwa viwandani
. Mwaka huu shindano hili lilijumuisha washindani kutoka mabara ya
Afrika,Ulaya,Asia,Latin America na Amerika ya Kaskazini.
Akiongea juu ya ushindi
alioupata alisema kuwa unatokana na elimu yake, mafunzo na mazoezi mbalimbali
ambayo amekuwa akiyapata katika kampuni anayofanyia kazi ya TBL Group.
“Mimi taaluma yangu nimesomea
Sayansi ya Chakula na tekinolojia (Food Science &Technology) ambayo
inajumuisha masuala ya ubora wa vyakula na vinywaji kutoka chuo kikuu cha
kilimo Sokoine. Mafunzo mengi Zaidi kuhusiana na ubora wa bia
niliyapata nikiwa kazini hivyo kunifanya kuwa mtaalamu
niliyebobea katika fani hii ya uonjaji wa bia”.Alisisitiza
Rebecca ambaye anafanya kazi
kama mtaalamu wa ubora wa vinywaji katika kampuni ya TBL alisema kuwa jukumu
lake kubwa ni kuhakikisha bidhaa zinazozalishwa zinakuwa bora na katika
mazingira ya usafi ili kutoleta madhara kwa watumiaji wake ambao ni wateja.
Alisema uonjaji wa bia
unafanyika katika viwanda vyote ili kujiridhisha kuwa bidhaa zinazoingia kwenye
masoko ziko vizuri “Pamoja na kuwepo mashine za kupima ubora na makampuni ya
kudhibiti viwango vya ubora wa bidhaa zetu bado tunahakikisha tunazionja kabla
ya kutumiwa na wateja na uonjaji sio wa ladha tu bali hata kuzinusa na
kuziangalia kwa macho ili kuhakikisha ziko vizuri’.Alisema.
Rebecca alimalizia kwa kusema
kuwa anajivunia ushindi huu kwake binafsi na mwajiri wake “Ushindi huu
unadhihirisha kuwa watanzania tunaweza tukiamua na mfano Dhahiri wa jambo hili
ni kwa jinsi viwanda vyetu vya Mwanza na Mbeya vinavyoshikilia rekodi ya
kuwa viwanda bora barani Afrika ambavyo vinavutia wageni kutoka kwenye hata
nchi zilizoendelea kuja kujifunza jinsi vinavyoendesha kazi zake”.Alisema.
0 comments:
Post a Comment