Naibu Waziri wa Nishati na
Madini, Dkt Medard Kalemani, akizungumza na wananchi wa kijiji cha Ishihimulwa,
Kata ya Bukumbi, wilaya ya Nzega hivi karibuni akiwa katika ziara ya kikazi
mkoani Tabora.
Nyaya za umeme katika Kijiji cha Mambali, Wilaya ya Nzega. Kijiji hiki ni miongoni mwa vijiji vilivyounganishiwa umeme kupitia Mradi wa Umeme Vijijini unaotekelezwa na Wakala wa Nishati Vijijini (REA) katika Awamu ya Pili ya REA.
*************
Na Veronica Simba - Nzega
Naibu Waziri wa Nishati na
Madini, Dkt Medard Kalemani ameliagiza Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO),
kuwachukulia hatua kali ikiwemo kuwafikisha Mahakamani wadaiwa wake sugu
hususan Kampuni na watu binafsi.
Dkt Kalemani alitoa agizo hilo
jana wilayani Nzega, akiwa katika ziara ya kikazi Mkoani Tabora kukagua miradi
mbalimbali ya sekta za nishati na madini inayotekelezwa chini ya Wizara yake. SOMA ZAIDI BOFYA HAPA
Alisema, Serikali ilikwishaanza
kulipa madeni yake kwa TANESCO, hivyo hakuna budi Kampuni na watu binafsi
wanaodaiwa na Shirika hilo kulipa madeni yao pia.
“Meneja wa TANESCO, Sheria ya
Umeme inakuruhusu kuwachukulia hatua wadaiwa waliogoma kulipa madeni yao.
Wapeleke Mahakamani.”
Katika kuhakikisha agizo lake
linapewa uzito unaostahili, Naibu Waziri aliwaagiza Mameneja wa TANESCO wa Mkoa
wa Tabora kumpatia orodha ya majina ya wale wote wanaodaiwa na Shirika hilo
mkoani humo ifikapo kesho Ijumaa, Februari 19 mwaka huu.
“Mnipatie orodha hiyo ifikapo
Ijumaa, iwe ni kampuni ya mtu mzito au mtu mwingine yeyote,” alisisitiza. Aliongeza
kuwa, ni lazima hatua stahiki zichukuliwe dhidi ya waliokaidi kulipa kwani
kitendo hicho ni kuihujumu TANESCO.
Naibu Waziri alisema Serikali
imedhamiria kukusanya mapato yote stahiki kwa ajili ya kuwaletea maendeleo
wananchi wake, hivyo alimwambia Meneja wa TANESCO Mkoa wa Tabora kuwa
asipochukua hatua kama alivyomwagiza, hatasita kumuwajibisha yeye mwenyewe.
Katika hatua nyingine, Naibu
Waziri Kalemani ameagiza kuwa Makandarasi wote wanaojihusisha na shughuli za
kutandaza waya na vifaa vingine kwa ajili ya kuunganisha umeme majumbani na
katika majengo mbalimbali (wiring), kujisajili katika Ofisi za Wilaya za
TANESCO.
Alisema, agizo hilo linafuatia
kuwepo na wimbi la matapeli maarufu kama vishoka ambao hufanya kazi hiyo ya
kuunganisha umeme pasipo kuwa na utaalam husika.
Aidha, aliwataka wananchi
kutofautisha kazi zinazofanywa na TANESCO na zile zinazofanywa na Makandarasi
binafsi katika zoezi zima la kuunganisha umeme.
Alisema, kazi ya TANESCO ni
kusimika nguzo za umeme na kuunganisha Waya unaoingiza umeme katika nyumba au
jengo husika lakini si kazi ya Shirika hilo kufunga Waya na Vifaa vya umeme
ndani ya nyumba au jengo.
“Wananchi wengi wamekuwa
wakilalamika sana kwamba wanatapeliwa kwa kutozwa fedha nyingi na/au kufungiwa
vifaa vya umeme visivyo na ubora kwenye nyumba zao. Mara nyingi lawama hizo
huelekezwa TANESCO.”
Dkt Kalemani alisema, ndiyo
maana Serikali kupitia Wizara yake, imeamua kuwa Makandarasi wote wanaojihusisha
na shughuli hizo wasajiliwe katika Ofisi za TANESCO za Wilaya ili wafahamike na
hivyo kuwaepushia wananchi adha ya kutapeliwa.
0 comments:
Post a Comment