Naibu Waziri wa Nishati na
Madini, Dkt Medard Kalemani (katikati), akiongozwa na baadhi ya viongozi wa
Machimbo ya Dhahabu ya Matinje yaliyopo katika Kijiji cha Matinje Kata ya
Mwashiku wilayani Igunga. Naibu Waziri alitembelea Machimbo hayo hivi karibuni
akiwa katika ziara ya kikazi mkoani Tabora.
Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Medard Kalemani
(Mwenye Suti-katikati) akipokea maelezo kutoka kwa Meneja wa Machimbo ya
Matinje yaliyopo Kata ya Mwashiku wilayani Igunga, Charles Nogu, wakati
alipotembelea Machimbo hayo akiwa katika ziara ya kazi hivi karibuni.
Naibu Waziri wa Nishati na
Madini (katikati) akikagua machimbo ya Matinje yaliyopo Kata ya Mwashiku
wilayani Igunga, alipotembelea Machimbo hayo hivi karibuni. Kushoto kwa Naibu
Waziri ni Mbunge wa Manonga, wilaya ya
Igunga, Seif Gulamali. Wengine pichani ni baadhi ya viongozi wa Machimbo hayo,
wataalamu kutoka Wizarani, Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) na Wakala wa
Nishati Vijijini (REA).
***************
Na Veronica Simba - Nzega
Serikali imetoa siku tano kwa
mwekezaji wa madini ambaye ni Kampuni ya NMDC Limited kutoka India,
kushughulikia utaratibu wa kuwalipa fidia wananchi wa Kata ya Ntobo iliyopo
wilayani Igunga, mkoa wa Tabora, walioachia ardhi yao kumpisha mwekezaji huyo.
Agizo hilo lilitolewa juzi,
Februari 17 na Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Dkt Medard Kalemani, wilayani
Nzega alipokutana na viongozi wa Kampuni hiyo akiwa katika ziara ya kikazi
mkoani Tabora kukagua miradi mbalimbali inayotekelezwa chini ya wizara yake.
Akiwa wilayani Igunga, Naibu
Waziri alipokea taarifa kuwa mwekezaji huyo alipewa leseni nne za uchimbaji
madini wa kati mwaka 2012 lakini mpaka sasa hajaanza shughuli za uzalishaji
kutokana na kutolipa fidia za maeneo ya wakazi wa eneo hilo.
Kutokana na taarifa hiyo,
Naibu Waziri aliagiza kukutana na Mwekezaji huyo ambapo walikutana naye juzi
akiwa wilayani Nzega akiendelea na ziara yake. SOMA ZAIDI BOFYA HAPA
Katika kikao hicho, ilibainika
kuwa, kiasi cha shilingi za Tanzania bilioni 20.7 zinadaiwa kama fidia kwa
wananchi waliopisha eneo husika.
Ilielezwa kuwa, ulipaji huo wa
fidia umekwama kutokana na mwekezaji huyo kutotaka kulipa fidia yote kwa wakati
mmoja bali anataka alipe fidia kidogo kwa kuanzia na eneo dogo kati ya lile
analomiliki ambalo anadai ndilo atakaloanza kufanyia kazi.
Aidha, alidai kwamba atakuwa
analipa fidia kwa eneo lililobaki kulingana na atakavyokuwa akilitumia.
Akizungumza katika kikao
hicho, Kamishna Msaidizi wa Madini wa Kanda ya Kati-Magharibi, Humphrey Mmbando
alimweleza Naibu Waziri kuwa, wananchi wa eneo husika wanalalamika kuwa tangia
eneo lao lichukuliwe na mwekezaji huyo, shughuli zao zilizokuwa zikifanyika
katika eneo hilo zimesimama na hivyo wanahitaji kulipwa fidia stahiki.
Kamishna Mmbando aliongeza
kuwa, kufuatia malalamiko ya wananchi, Ofisi yake ilimtaka mwekezaji huyo awe
ametoa majibu ya namna atakavyoshughulikia madai ya wananchi ndani ya siku 10
ambayo ilikuwa ni juzi, Februari 17, wakati kikao hicho kikikaa.
Kutokana na maelezo hayo,
Naibu Waziri alitoa siku tano zaidi kwa mwekezaji huyo ili ashughulikie mambo
kadhaa katika kutatua mgogoro huo.
Ndani ya siku hizo tano, Naibu
Waziri alimtaka mwekezaji huyo, atoe taarifa rasmi ya kimaandishi kwa Ofisi ya
Kamishna Msaidizi wa Madini Kanda ya Kati Magharibi kuwa anakusudia kufanya
uzalishaji kwa kuanzia na eneo dogo ndani ya leseni yake.
Pia, alimtaka mwekezaji huyo
kumwomba Mthaminishaji wa Serikali kufanya uthamini kwa kujikita katika eneo
lile tu ambalo anakusudia kuanza kulifanyia kazi.
Vilevile, Naibu Waziri
alimtaka mwekezaji huyo kuzungumza na wananchi husika ili wakubaliane kiasi cha
fidia atakachotoa kwao kwa kuzuia shughuli zao za kujipatia kipato katika eneo
hilo kwa kipindi cha zaidi ya miaka miwili.
Mbali na maagizo hayo, Naibu
Waziri alimtaka mwekezaji huyo awaruhusu wananchi kuendelea na shughuli za
uzalishaji katika eneo ambalo atakuwa hajaanza kulifanyia kazi.
“Nimewapa siku tano zaidi,
mfanyie kazi maagizo niliyoyatoa vinginevyo, tutachukua hatua nyingine stahiki
za kisheria dhidi yenu.”
Katika hatua nyingine, Naibu
Waziri Kalemani ameagiza kufutwa kwa leseni zote za madini ambazo hazifanyiwi
kazi na maeneo hayo kugawiwa kwa wachimbaji wadogowadogo ili wayafanyie kazi na
kulipa mrabaha kwa Serikali.
“Kwa kuanzia, katika eneo
hili, nimeagiza leseni za utafutaji wa madini za kampuni za Kilimanjaro Mine na
Mabangu Resources ziandikiwe taarifa ya kufutwa na tutaendelea na maeneo
mengine,” alisema.
Alisema kuwa kuna wawekezaji
wengi ambao wamekuwa wakishikilia maeneo kwa muda mrefu pasipo kuyafanyia kazi
na hivyo kuikosesha Serikali mapato yatokanayo na kodi, pia kuwakosesha
wananchi maeneo ya kufanyia kazi.
Awali, Naibu Waziri
alitembelea Machimbo ya Madini katika Kijiji cha Matinje B, Kata ya Mwashiku
wilayani Nzega ambapo mbali na kumpongeza mmiliki wa machimbo hayo, Jason
Shinyanga, kwa kulipa mrabaha wa Serikali, alimtaka kuboresha mazingira ya
uchimbaji katika eneo hilo.
Meneo aliyoagizwa kuboresha ni
pamoja na kujenga nyumba za kulala watumishi wake pamoja na vyoo bora.
“Tunakupa taarifa ya siku 60 urekebishe dosari hiyo, usiporekebisha, tutasahau
kama umelipa mrabaha au la,” alisisitiza Naibu Waziri.
Aidha, Naibu Waziri
aliwashauri wananchi wanaojishughulisha na uchimbaji kuhakikisha wanapata
ushauri wa kitaalamu kutoka ofisi za madini katika maeneo yao kabla hawajaanza
shughuli hizo.
Pia, aliwataka kuhakikisha
wanakuwa na leseni halali za kuendeshea shughuli hizo za uchimbaji ili pamoja
na mambo mengine kuongeza thamani ya maeneo yao pindi wanapotaka kuyauza au
kuingia ubia na wawekezaji wa kati na wakubwa.
0 comments:
Post a Comment