Wafanyakazi wa Kampuni ya TARMAL ya jijini Dar es Salaam inayofanya kazi za PSI katika ghala lake la kuhifadhia dawa na vifaa mbalimbali kama Condomu za kike na kiume wakiimba wakiwa na mabango wakimtaka Waziri Mkuu Kassim Majaliwa kusimama na kusikiliza kilio chao. Baadae Waziri Mkuu alisimama na kuwasikiliza.
KUNDI la watumishi wa kampuni
ya TARMAL inayofanya kazi katika ghala la PSI katika bohari ya vifaa tiba lililopo Ubungo
jijini Dar es Salaam leo waliuzuia msafara wa Waziri Mkuu Kassim Majaliwa kwa
dakika kadhaa ili wampe kilio chao. Mwandishi wa Father Kidevu Blog anaandika zaidi.
Watumishi hao wengi wao
wakiwa ni wanawake walipaza sauti zao wakati Waziri Mkuu akipita alipokuwa
akitokea Bohari ya Dawa (MSD) katika
Ghala la vifaa tiba kupokea msaada wa vifaa tiba vyenye thamani ya Sh Bilioni
10 kutoka kampuni za Uzalishaji vinywaji Baridi nchini vya Coca Cola, Pepsi na
Azam.
Waziri Mkuu Majaliwa baada
ya kuona kundi hilo la watumishi aliamua kuteremka katika gari na kuzungumza
kidogo na wasaidizi wake kasha kuwasalimu watanzania hao na kupokea kilio chao
kilicho wasilishwa kwake na kiongozi wao Amin Athumani.
Athumani alisema kubwa
linalowaumiza ni wao kudumu kama vibarua kwazaidi ya miaka saba, huku wakipewa
ujira wa sh 5,550/= kwa siku sawa na Sh 27,500 kwa wiki au 110,000 kwa mwezi.
Kilio kingine ni kukosa
huduma za afya pindi wanapoumwa, kutopelekewa makato ya PPF au NSSF, kukosa
ajira na kupewa mikataba ya ajira ambayo haina kikomo na ambayo haina maslahi
yoyote ili mradi kuzidanganya mamlaka za serikali.
Aidha
kilio kingine ni kukosa malipo pindi mama akiwa katika likizo ya uzazi,
manyanyaso ya mwajiri wao TARMAL, pamoja na malipo hayo ya 5,500 ambayo wakati
mwingine hulipwa pungufu.
“Tunakuomba Waziri Mkuu, Serikali yako imeonesha nia ya
dhati kuwasaidia wanyonge, kwahiyo maombi yetu tunakuomba walau mshahara wetu
uwe sh 10,000 kwa siku na tulipwe kwa mwezi,”alisema Athumani kwa niaba ya
wenzake.
Baada
ya kusikia kilio chao hicho kutoka kwa wafanya kazi hao katika ghala la PSI na
kazi yao kubwa ni kupaki bidhaa mbalimbali za PSI Waziri Mkuu Kassim Majaliwa
aliwasihi kuendelea na kazi lakini kesho Ijumaa, February 26,mwaka huu majira
ya Saa 2:00 asubuhi Waziri mwenye dhamana ya Kazi atafika na kuzungumza nao.
Waziri
Mkuu aliwaeleza haya katika kujibu hoja zao …”Nimeyasikia malalamiko yenu na
tunakutana leo kwa mara ya kwanza, lakini serikali hii inasimamia pale pote
ambapo pana matatizo na wizara yangu ndio inahusika na mambo ya ajira, kazi na
maeneo yote yale yanayohitaji kutatuliwa matatizo haya, na mimi nina waziri
anaeshughulikia jambo hilo mheshimiwa Jenista Mhagama.
Nawasihi
wote kesho mje kazini asubuhi, Saa mbili mama Jenista Mhagama atakuwa hapa,…
kwakua mmelalamikia hata makato ya PPF hayakatwi atakuja na Mtendaji wa PPF
hapa ili aje amthibitishie mheshimiwa Mhagama kwamba hakuna makato yanakuja kwake,
kwahiyo na wasihi sana Yule kiongozi ayaandike vizuri yale matatizo ili kesho
akija ayasome vizuri, ayasikie na atazungumza na Management kesho hiyo hiyo na
utatuzi utaoata njia kesho hiyo hiyo.
Kwahiyo
na wasihi sasa kwakua jambo lenu mmeliwasilisha kwa mara ya kwanza, wala
msigomee kazi mmesha yaleta serikalini, Waziri mwenye dhamana anakuja
atawasikiliza na atashughulikia kikamilifu na atawapa ufumbuzi naomba mniruhusu
nipite!,” alimaliza kuzungumza na kuingia katika gari na kuondoka katika eneo
hilo.
Wafanyakazi
hao wa kampuni ya TARMAL walibaki wakiimba na kufurahi huku kesho wakimsubiri
kwa hamu Waziri wa Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Walemavu, Jenista
Mhagama akiambatana na Mkurugenzi Mkuu
wa Mfuko wa Pensheni wa PPF, William Erio kwenda kuwasikiliza kama Waziri Mkuu
alivyo elekeza.
0 comments:
Post a Comment