Dereva Tukae Ngonyani akiwa kwenye usukani kwenye moja ya
lori la kusambaza vinywaji analoliendesha
Dereva Tukae Ngonyani akiwa amesimama katika moja ya lori
la kusambaza vinywaji analoliendesha
Dereva Tukai Ngonyani akishuka kwenye Folk Lift
anayoendesha baada ya kuchapa kazi
. Dereva Tukae
Ngonyani akiendesha Folk Lift katika kiwanda cha TBL kilichopo Ilala jijini
Dar es Salaam
********
- Atoa ushauri kwa wanawake wenzake kuzingatia falsafa ya ‘Hapa Kazi’
“Wanawake wa Tanzania tunakabiliwa na changamoto
mbalimbali kutokana na kukandamizwa na mfumo dume kwa muda mrefu. Moja ya
changamoto kubwa ni kuachwa nje ya mfumo
wa ajira rasmi na zisizo rasmi”.Anasema
Tukae Ngonyani ambaye ni dereva wa magari makubwa ya kusambaza vinywaji ya
kampuni ya Tanzania Breweries Limited katika kiwanda cha Ilala jijini Dar es
Salaam.
Pamoja na ukosefu wa ajira kuwa moja ya changamoto
kubwa inayowakabili wanawake ,Tukae anasema kuwa wanawake wengi nao wana tatizo
la kushindwa kujiamini na kuwa na kasumba ya kuchagua kazi na kudhani kuwa
baadhi ya kazi ni kwa ajili ya wanaume tu wakati hakuna kitu kama hicho.
“Inafurahisha hivi sasa akina mama wameweza kuwa
na mwamko wa kufanya kazi mbalimbali zinazofanywa kwa wingi na wanaume,hata
hivyo bado idadi yao ni asilimia ndogo na kuna haja ya kujitokeza zaidi ili kupunguza idadi kubwa ya wanawake
wasio na kazi.”Anasema. SOMA ZAIDI BOFYA HAPA
Akielezea
historia yake ya kazi alisema kuwa tangu
alipokuwa na umri mdogo alikuwa anatamani kufanya kazi za ufundi na alipomaliza
elimu yake ya msingi alijifunza ufundi umeme wa majumbani.
“Nilijifunza ufundi wa umeme wa majumbani nikawa
nafanya wiring na kazi nyinginezo za ufundi wa umeme kwenye nyumba mbalimbali
mitaani nikiwa na mafundi wa kiume kwa kuwa kwenye fani ya ufundi pia akina
mama ni wachache.”Anasema.
Tukae alisema kuwa mnamo mwaka 1987 aliomba kazi ya
ufundi umeme katika kampuni ya Tanzania Breweries Limited (TBL) kwa bahati mbaya hakufanikiwa kuipata badala yake alipata kazi ya kuwa Mhudumu wa
ofisini (Messenger) ambapo hata hivyo
hakusita kuifanya kazi hiyo.
“Nikiwa nafanya kazi ya uhudumu nilivutiwa na
jinsi nilivyokuwa nikiwaona wanaume wakiendesha vifaa mbalimbali vinavyosaidia
katika uzalishaji kiwandani na nilipomueleza bosi wangu kuwa nilitaka kujifunza
kuendesha magari madogo ya kupakia na kushusha mizigo (Fork Lifts)
hakunikatisha tamaa bali nilipatiwa fursa hiyo na kupatiwa mafunzo ya ndani na
baada ya muda mfupi nikamudu kazi hiyo na kufanikiwa kubadilisha kazi kutoka
kuwa mhudumu wa ofisi hadi kuwa dereva wa Folk Lifts”.
Anasema baada ya kuendesha magari hayo kwa kipindi
cha miaka mitano ndani ya kiwanda alitamani
kujifunza udereva wa magari makubwa baada ya kuvutiwa na madereva
aliokuwa akiwaona kiwandani hapo na barabarani wakiwa wanaendesha magari
makubwa ya mizigo.
“Nashukuru mume wangu aliyenitia moyo wa
kufanikisha ndoto yangu ambaye pia anafanya kazi ya udereva bila kusahau mabosi
wangu wa TBL kwa kuniwezesha kuhudhuria
kozi ya udereva katika chuo cha VETA kilichopo jijini Dar es Salaam na
kufanikiwa kufuzu vizuri kozi ya udereva wa magari makubwa na kupata leseni
inayostahili kwa kazi hiyo”
Kuhusu changamoto anazokabiliana nazo katika kazi
yake alisema zipo changamoto za kawaida kama zilizopo kwenye kazi nyingine .
“Naipenda kazi yangu na nafurahi kuona watu wengi kwenye jamii wakifurahi na
kunipongeza wanapoona naendesha lori kubwa la mizigo na hii inatokana na sababu
kuwa wamezoea kuona kazi hizi zikifanywa na wanaume pekee”.
Tukae ambaye ni mama mwenye mume, watoto na
wajukuu anasema kuwa anafurahi kufanya kazi katika kampuni kubwa ya TBL kwa
kuwa ina mifumo mizuri ya ajira yenye maslahi mazuri ikiwemo taratibu za
kuwapatia mafunzo ya mara kwa mara wafanyakazi wake na anakiri kuwa ajira yake imemwezesha kupata
mafanikio kimaisha.
Kuhusu
mipago yake ya baadaye alisema kwa sasa hana mpango wa kubadilisha kazi na
alimalizia kwa kuwataka akina mama wajitokeze na kujiamini kufanya kazi zote
bila kuchagua kwa kuwa hakuna kazi kwa ajili ya wanaume peke yao au wanawake
peke yao.
“Akina mama tuzingatie kauli mbiu ya Rais wetu wa
Tanzania Mh.John Magufuli isemayo ‘Hapa Kazi tu’ tufanye kazi na kuacha kuwa
wategemezi tutafanikiwa”.Alisisitiza.
0 comments:
Post a Comment