Nafasi Ya Matangazo

January 27, 2016

Mafundi wa Shirika la MajiSafi na Majitaka Dar es Salaam (DAWASCO) wakiondoa mipira ya Maji kwenye bustani ya mboga mboga eneo la Kawe wilaya ya Kinondoni Jijini Dar es salaam ambapo watu 8 wameshikiliwa kwa tuhuma za kuihujumu Miundo mbinu ya Dawasco na kusababishia upotevu mkubwa wa Mapato kwa Shirika. (picha kwa hisani ya DAWASCO)

Wamiliki wa mashamba ya bustani ya Mboga mboga waliyokutwa wikitumia Maji ya Wizi kwenye kuendesha Bustani hizo wakiwa chini ya ulinzi baada ya kukamatwa na DAWASCO katika operesheni iliyofanyika mapema wiki hii. Jumla ya watuhumiwa 8 wamekamatwa na wanatarajiwa kufikishwa kwenye vyombo vya sheria hivi karibuni.

******************
Shirika la Majisafi na Majitaka Dar es salaam (DAWASCO) limewakamata watu 8 wenye mashamba eneo la Sakoveda mbezi Juu wilayani Kinondoni baada ya kugundulika wakiliibia Maji shirika hilo.

Akizungumza wakati wa operesheni ya mtaa kwa mtaa kuhakiki matumizi sahihi ya Maji kwa watumiaji wakubwa wa Maji eneo hilo, Meneja wa Kawe, Bwn Crossman Makere alisema operesheni hiyo ni mwanzo tu wa kutumbua uovu unaofanywa na watumiaji Maji kwa mgongo wa Ulimaji Mashamba na uuzaji maua ulioshika kasi jijini Dar es Salaam. SOMA ZAIDI BOFYA HAPA.
“Dawasco tunajiendesha kwa kuzalisha Maji na kuhudumia wananchi na gharama zote hizo ni kutokana na mapato yanayopatikana ndani ya shirika kutokana na Ankara ya Maji inayolipwa na mteja.

“kwahiyo inapotokea watu wanafanya hujuma za aina yoyote ieleweke kwamba shirika linaingia hasara kubwa ambayo haiwezi kuvumiliwa kwa namna yoyote.

“hivyo basi tumeamua kufanya ukaguzi wa mashamba na bustani zote za mboga ili kubaini ni kina nani wanaohujumu shirika kwa kujiunganishia Maji kupitia njia za panya” Alisema Bwn Makere

Aliongeza kuwa watu hao 8 wamekamatwa baada ya kupata taarifa toka kwa wasamalia wema juu ya kuwepo kwa maunganishio yaliyofanywa usiku wa manane ambayo yanapeleka Maji kinyemela katika mashamba hayo yenye ukubwa wa ekari zaidi ya 3.

“tumegundua maungio ya Inchi Moja zaidi ya 2 yanayopeleka Maji kwenye mashamba hayo ambayo wanalima zaidi mboga za majani kama mchicha na spinachi kwenye shamba hilo ambapo licha ya kuwataka wahusika wajieleze kuhusu Maji wananyotumia kustawisha mboga hizo hawakuwa na majibu sahihi” alisema Bwana Makere

Kwa upande wake, Mmoja wa wamiliki wa shamba hilo Bi Rahabu Vicent alisema tangu aanze kilimo hapo alikuta Maji yameunganishwa na hawakujua aliyeunganisha na yeye anategemea zaidi Maji ya Mto unaopita pembeni ya Mashamba yetu hivyo Maji ya DAWASCO anayatumia ila kwa kiasi kidogo.

Watuhumiwa hao walipoulizwa kama wanautaratibu wa kulipa Ankara zao kila mwezi kwa Maji ya Dawasco wanayotumia, Bi Rahabu alisema tangu waanze kutumia Maji hayo hawajawahi kupata bili yoyote toka DAWASCO na hawakufatilia kupata utaratibu wa kulipia kwani hata Mita ya Maji hawana.

Kwa upande wa mjumbe wa serikali ya Mtaa wa Sakuleda Bwn Cwell Mbeye alikiri kufahamu biashara hiyo kufanyika katika eneo hilo na kusema wananchi walishalipigia kelele suala hilo kwani wafanyabiashara hao walisababisha huduma ya Maji katika eneo hilo kukosekana kutokana na wao kuhujumu miundombinu ya Maji katika eneo lao.

‘Tunaishukuru DAWASCO kuja kufanya operesheni hii kwani tunaamini sasa kilio cha wananchi wa eneo hili kukosa Maji kitapungua na sasa huduma hiyo itarudi baada ya wabadhilifu hao kujulikana na miundombinu yao kukamatwa” alisema Bwn Mbeye


Watuhumiwa waliokamatwa ni  Rose Paint, Anna Ndegeru, Chrispina Joseph, Kokubanza Herbert, Sifaeli Eliud, Sophia Mahenge, Rahabu Vicent  na Kesi hiyo imefunguliwa katika kituo cha polisi Kawe  na shauri litapelekwa Mahakama ya Jiji kwa ajili ya hukumu.
Posted by MROKI On Wednesday, January 27, 2016 No comments

0 comments:

Post a Comment

  • Facebook
  • Twitter
  • Youtube

Labels

Blog Archive

Nafasi Ya Matangazo