Mkurugenzi Mkuu wa kampuni hodhi ya rasilimali za reli Tanzania (RAHCO) Mhandisi Benhadard Tito.
Rais wa Jamhuri ya Jamhuri wa
Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amemsimamisha kazi Mkurugenzi
Mkuu wa kampuni hodhi ya rasilimali za reli Tanzania (RAHCO) Mhandisi Benhadard
Tito ili kupisha uchunguzi wa kina kufuatia ukiukwaji mkubwa wa taratibu za
manunuzi uliobainika katika mchakato wa utoaji wa zabuni ya ujenzi wa reli ya
kati.
Akitoa taarifa kwa vyombo vya
habari, Katibu Mkuu Kiongozi Balozi Ombeni Sefue amesema, Rais Magufuli
amefikia uamuzi huo baada ya kuitisha kikao cha wataalamu kutoka Wizara na
Taasisi mbalimbali za serikali ambazo zinahusika katika utekelezaji wa Mradi wa
Ujenzi wa Reli ya kati kwa kiwango cha kisasa yaani "Standard Gauge"
Amesema pamoja na kumsimamisha
kazi Mkurugenzi Mkuu wa RAHCO, Rais Magufuli ameivunja bodi ya RAHCO baada ya
kujiridhisha kuwa haikutekeleza ipasavyo wajibu wake katika kusimamia mchakato
wa zabuni hiyo na badala yake imeonekana kutetea kilichofanyika.
Aidha Rais Magufuli amemtaka
Mkurugenzi Mkuu wa RAHCO Mhandisi Benhadard Tito kutoa ushirikiano kwa vyombo
vya serikali vitakavyofanya uchunguzi zaidi kuhusu mchakato wa Zabuni hiyo.
Pia ameiagiza Mamlaka ya
udhibiti wa manunuzi ya umma (PPRA) kuchunguza na kuchukua hatua dhidi ya
kampuni za ukandarasi zilizopewa zabuni ya ujenzi huo endapo itathibitika kuwa
zimeshiriki katika ukiukwaji wa sheria.
Katika hatua nyingine Balozi
Sefue amesema, Rais Magufuli amevunja bodi ya Mamlaka ya Reli Tanzania (TRL)
kutokana na kutoridhishwa na jinsi bodi hiyo ilivyoshughulikia ripoti ya
uchunguzi wa mchakato wa ununuzi wa mabehewa ya treni.
Gerson Msigwa
Kaimu Mkurugenzi
wa Mawasiliano,
IKULU 22 Desemba,
2015
0 comments:
Post a Comment