Washiriki wa mafunzo ya makandarasi wanawake
wakifuatilia mjadala wa mafunzo hayo mjini Kibaha mkoani Pwani.
Mgeni rasmi wa mafunzo ya makandarasi wanawake Bi,
Elizabeth Tagora katika picha ya pamoja na washiriki wa mafunzo hayo.
Mratibu wa mafunzo hayo Mhandisi Rehema Myeya
akimkaribisha mgeni rasmi Bi, Elizabeth Tagora ili kufungua mafunzo hayo.
Makandarasi wanawake
nchini wametakiwa kujiendeleza kiuchumi na kitaaluma kila wakati ili wawe na
uwezo wa kushindana na makandarasi wengine katika zabuni za miradi mikubwa ya
ujenzi hapa nchini.
Mkurugenzi wa Sera na Mipango
wa iliyokuwa Wizara ya Ujenzi Bi, Elizabeth Tagora amesema hayo wakati
akifungua mafunzo ya siku tano ya makandarasi wanawake yalioanza leo mjini Kibaha
mkoani Pwani.
“Mafunzo haya
yatawawezesha kufahamu vitu vya msingi wakati wa kujaza zabuni na ununuzi wa
kazi za ujenzi na hivyo kuwawezesha kushindana kwa usawa na hata kushinda zabuni
na kutekeleza ujenzi wa miradi ya barabara kwa usahihi”, amesema Bi, Tagora.
Mkurugenzi huyo
amesema Wizara ya Ujenzi,Uchukuzi na Mawasiliano itaendelea kuutekeleza sera mbalimbali zenye lengo la
kuongeza ushiriki wa wanawake katika sekta ya ujenzi hapa nchini ili
kuwawezesha makandarasi wanawake nchini waweze kupanda na kufikia ngazi za juu za
ukandarasi na hivyo kuwa na fursa sawa ya ushindani na wanaume wakati wa kuomba
zabuni za miradi ya ujenzi wa barabara.
“Kumbukeni
kuunganishwa kwa wizara kunawaongezea fursa ya kuomba miradi mingi zaidi katika
sekta ya viwanja vya ndege na maeneo ya bandari nchini kote hivyo ni jukumu
lenu kuzingatia mafunzo haya na kuongeza ujasiri wa kuthubutu kuombamiradi
mikubwa na kuitekeleza kwa ubora unaotakiwa” amesisitia Bi, Tagora.
Mkurugenzi huyo wa Sera na Mipango amezungumia umuhimu wa mafunzo hayo kwa makandarasi wanawake na
kuwataka kuwa chachu ya kujiendeleza zaidi na kuhakikisha wanakuwa na malengo
yanayotekelezeka kila mwaka ili kujitathmini.
Naye mratibu wa
mafunzo hayo kutoaka Wizara ya Ujenzi,Uchukuzi na Mawasiliano Eng. Rehema Myeya
amesema tangu kuanzishwa kwa mafunzo ya kuwewezesha makandarasi wanawake kuwa
na uwezo wa kujaza zabuni na mikataba ya ujenzi idadi ya makandarasi wanawake
nchini imeongezeka ambapo sasa zaidi ya kampuni
za makandarasi 200, zinashiriki katika ujenzi wa barabara nchini kote.
Eng. Myeya amesema
mafunzo hayo ambayo ni endelevu yatakuwa yakitolewa katika kila kanda ili
kuongeza idadi ya makandarasi wanawake na kuchochea hamasa katika kila mkoa na
hivyo kukuza uchumi wa wanawake na jamii kwa ujumla.
Makandarasi Wanawake
kutoka mikoa ya Dar es salaam, Tanga, Kilimanjaro, Morogoro na Singida wameshiriki
mafunzo hayo yenye lengo la kuwawezesha kujua namna bora ya kujaza zabuni na
utekelezaji wa miradi ya barabara kwa kuzingatia mkataba.
0 comments:
Post a Comment