Msemaji wa Wizara ya Nishati
na Madini Bi. Badra Masoud akiwaeleza waandishi wa habari (hawapo
pichani)mapema leo jijini Dar es Salaam kuhusu mpango wa Serikali wa kuunda
kikosi maalum cha kukabiliana na tatizo la wizi wa umeme na kuimarisha ukaguzi
ili kubaini wateja wasio waaminifu na kuwachukulia hatua za kisheria. Kulia ni
Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Habari (MAELEZO) Bi. Zamaradi Kawawa. (Picha na
Fatma Salum- Maelezo).
***************
Na Greyson Mwase, Dar es
Salaam
Kutokana na wizi wa umeme
kukithiri na kuliingizia hasara Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Wizara ya
Nishati na Madini imeliagiza Shirika hilo kuimarisha kikosi chake cha ukaguzi
wa watumiaji wa umeme ili kubaini wateja wasio waaminifu wanaoiba umeme na kuwachukulia
hatua za kisheria.
Hayo yamesemwa na Msemaji wa Wizara ya Nishati na Madini Badra Masoud alipofanya
mkutano na waandishi wa habari kwa ajili ya kuendelezea mafaniko na changamoto katika usimamizi wa sekta ya
umeme.
Masoud alisema Wizara inatarajia
kuunda kikosi maalum kitakachojumuisha wataalam kutoka katika taasisi
mbalimbali kwa ajili ya kukabiliana na tatizo hilo linalolikosesha
mapato shirika la TANESCO.
Alisema kikosi hicho kitajumuisha wataalam kutoka
TANESCO, Wizara ya Nishati pamoja na vyombo vya usalama na kuongeza kuwa hatua
hii imekuja baada ya Wizara kubaini kuwa kuna
baadhi ya watu wanaohujumu miundombinu ya TANESCO kama vile kuchoma nguzo
za umeme, kuiba mafuta ya transfoma pamoja na nyaya za umeme na kuwataka kuacha kufanya hujuma hizo kwani
watakaogundulika wataendelea kuchukuliwa hatua za kisheria.
Akielezea zoezi
hilo, Masoud alisema kuwa hivi
sasa sasa vyombo vya dola katika mkoa wa Lindi vinaendelea kuwasaka na kuwatia
nguvuni wale wote waliohusika kuchoma nguzo za umeme wa msongo mkubwa
unaosafirisha umeme kutoka Mtwara kwenda Lindi katika vijiji vya Hingawali na
Njonjo mkoani Lindi na kusababisha mikoa hiyo miwili kukosa umeme na
kusababisha hasara kwa TANESCO.
Masoud alizitaka Taasisi mbalimbali za Serikali na zisizo za
Kiserikali kuzingatia matumizi bora ya umeme ili kudhibiti upotevu wa nishati
ya umeme na kusisitiza kuwa utaratibu
huu wa matumizi bora ya umeme hufanywa pia na nchi nyingi duniani kwa ajili ya
kukabiliana na upotevu wa umeme.
Aliongeza kuwa kuna baadhi ya
taasisi huwa zinaacha umeme ukiendelea kupotea baada ya muda wa kazi kama vile
kuacha viyoyozi, taa, kompyuta na vifaa
vingine vinavyotumia umeme vikiendela kutumia umeme hivyo kusababisha
upotevu mkubwa wa umeme
ambao ungetumika katika maeneo mengine
au kuokoa fedha ambazo hutumika kuzalisha umeme huo.
Akielezea hali ya upatikanaji
wa umeme nchini Masoud alisema kuwa hali ya umeme nchini ni nzuri na hakuna mgawo
wowote unaoendelea hivi sasa kwani hali ya uzalishaji ni nzuri pamoja na
mabwawa ya maji ambayo hutumika kuzalisha umeme kukauka.
Alisisitiza kuwa kiasi cha
umeme kinachopatikana kwa sasa ni megawati 1500 huku matumizi ikiwa ni kati ya megawati
800 na 900 kutokana na umeme huo kuzalishwa kwa kiasi kikubwa kutokana na gesi
asilia pamoja na mafuta mazito na dizeli.
0 comments:
Post a Comment