JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
WIZARA YA MAMBO YA NDANI YA NCHI
JESHI LA POLISI TANZANIA
TAARIFA
YA KAMANDA WA POLISI MKOA WA DODOMA KWA VYOMBO VYA HABARI TAREHE 06/07/2015
Nina imani kila mmoja anayo taarifa kuwa wiki hii hapa Dodoma kutakuwa na
Mkutano Mkuu wa Chama cha Mapinduzi.
Mkutano huo utajumuisha Viongozi wa Kitaifa na Wajumbe wengi. Kutokana na unyeti wa mkutano huo mawazo na masikio
ya watu wengi wa ndani na nje ya Tanzania watayaelekeza katika Mkoa wetu kutaka
kujua nini kinachoendelea.
Kwa vile mkutano huo utakusanya watu wengi, Jeshi la Polisi Mkoa wa Dodoma likishirikiana
na vyombo vingine vya Dola tumeimarisha ulinzi ili wageni na wenyeji waweze
kufanya shughuli zao kwa amani, usalama na utulivu. Ulinzi huo umeimarishwa pamoja na mambo
mengine ikiwa ni pamoja na doria za miguu, magari, pikipiki na Mbwa na Farasi.
Ili Jeshi la Polisi na vyombo vingine vya Dola waweze kufanya kazi hiyo kwa
ufanisi, linaomba ushirikiano wa Wananchi wa Dodoma na wageni kwa kutupa taarifa
pale watakapoona mtu/watu au jambo lolote linaloashiria uhalifu ili hatua za
haraka ziweze kuchukuliwa.
Aidha wamiliki na wahudumu wa nyumba za kulala wageni waimarishe ulinzi wa
maeneo yao, kuwashauri na kuhifadhi mali za wateja na kutoa taarifa kwa Jeshi
la Polisi pale wanapoona watu/wageni wanaowahisi ni wahalifu, kwani uhalifu
ukitokea katika eneo lako ni dosari kwa biashara yako.
Pia tunaomba kila mmoja atambue na kukumbuka kila mara kuwa ulinzi na
usalama unaanza na yeye mwenyewe kwanza.
Nitoe onyo kwa wale wenye mawazo ya kupanga kufanya uhalifu wa aina yeyote
ile uwe wa kijinai au wa usalama barabarani atambue atashughulikiwa kwa nguvu
zote kwa mujibu wa sheria za Nchi na asitokee wa kumlaumu mtu kama atakuwa
amevunja sheria.
Niwashauri wale wote ambao wanataka kuja Dodoma katika wiki hii kama hana
shughuli maalum inayomlazimu kuja ni vizuri asije ili kuepuka usumbufu maana
wengine wanaweza kuja tu kwa lengo la kuja kushuhudia kinachoendelea au kwa
ajili ya ushabiki tu.
Imetolewa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma
0 comments:
Post a Comment