Na Mwandishi
Wetu
Mchekeshaji maarufu Eric Omondi na bendi ya muziki ya SARABI
kutoka Kenya wataungana na wanamuziki wa Tanzania Grace Matata na Leo Mkanyia
na bendi yake ya Swahilli Blues kukonga nyonyo za mashabiki wa muziki na
vichekesho jijini Dar es Salaam wakati wa onyesho la muziki jumamosi wiki hii.
Onyesho hilo ambalo limeandaliwa na CDEA:“Culture and
Development East Africa” kwa kushirikiana na Nafasi Art Space litafanyika
jumamosi ya tarehe moja mwezi wa nane mwaka huu, kuanzia saa moja jioni mpaka
asubuhi katika ukumbi wa Nafasi Art Space-Mikocheni.
Mratibu wa onyesho hilo Naamala Samson alisema kuwa mbali na
onyesho hilo pia kutakuwa na burudani kemkem kutoka kwa maDJ wa Santuri Safari
kutoka Kenya na Uganda ambapo kiingilio kitakuwa ni shilingi 10,000/- kupata
burudani za muziki wa bendi na kwa wale watakaoingia kwenye disco la kukesha ni
shilingi 20,000/-, na tiketi za V.I.P zitauzwa kwa shilingi 40,000/-.
“Wanamuziki wote wamefanya mazoezi ya kutosha na wamejiandaa
kikamilifu kwa onyesho hili la kihistoria, ni siku hiyo watanzania watapata
fursa ya kuonja ladha ya muziki wa Afrika Mashariki wenye vionjo vya nyumbani
na kupata vichekesho vya mwaka kutoka kwa Omondi” alisema Naamala.
Bendi ya Sarabi ni miongoni mwa bendi kubwa na zinazofanya
vizuri nchini Kenya na kuwepo kwake kwenye tamasha hili kutanogesha mambo na
kutoa burudani ya kutosha kwa wakazi wa Dar es Salaam na maeneo ya jirani.
0 comments:
Post a Comment