MALINZI AWAPONGEZA YANGA
Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu
nchini TFF, Jamal Malinzi ametuma salamu za pongezi kwa Mwenyekiti wa klabu ya
Young Africans, Yusuf Manji kufuatia timu yake kutwaa Ubingwa wa Ligi Kuu ya
Vodacom msimu wa 2014/2015.
Katika salamu zake za pongezi,
Malinzi amesema kutwaa Ubingwa wa VPL ni jambo muhimu na sasa wanapaswa kuanza
maaandalizi kwa ajili ya michuano ya kimataifa barani Afrika mwakani.
Klabu ya Young Africans imetwaa
Ubingwa wa Ligi Kuu nchini kwa mara ya 25 (ishirini na tano) jana, baada ya
kuibuka na ushindi wa mabao 4-1 dhidi ya timu ya Polisi Morogoro katika uwanja
wa Taifa huku ikiwa na michezo miwili mikononi kabla ya ligi kumalizika.
Waziri wa Habari, Vijana Utamuduni na
Michezo, Dr. Fennela Mkangara anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika sherehe za
kukabidhi Kombe la Ubingwa wa Ligi Kuu ya Vodacom Mei 6, 2015 katika mchezo
kati ya Azam FC dhidi ya Young Africans.
VILABU VPL
VYAPIGWA FAINI, WAAMUZI WAFUNGIWA
Ruvu Shooting imepigwa faini ya sh. 300,000 (laki tatu) kwa
kuzingatia Kanuni ya 14(9) ya Ligi Kuu kwa kutoingia kwenye vyumba vya
kubadilishia nguo (changing room) katika mechi namba 149 dhidi ya Kagera Sugar
iliyochezwa Uwanja wa Kambarage mjini Shinyanga
Pia Ruvu Shooting
imepigwa faini ya sh. 500,000 (laki tano) kwa kutoingia vyumbani wakati wa
mapumziko kwenye mechi hiyo. Adhabu hiyo imetolewa kwa kuzingatia Kanuni ya
14(13) ya Ligi Kuu.
Stand United imepigwa faini ya sh. 500,000 (laki tano) baada
ya washabiki wake kuwatupia chupa za maji wachezaji wa akiba wa timu ya Polisi
Morogoro katika mechi iliyochezwa Uwanja wa Kambarage mjini Shinyanga. Adhabu
hiyo imetolewa kwa mujibu wa Kanuni ya 42(1) ya Ligi Kuu.
Naye Meneja wa Polisi Morogoro, Manfred Luambano alitolewa
kwenye benchi la Polisi Morogoro kwa kosa la kutoa lugha za kashfa kwa mwamuzi
msaidizi namba moja Martin Mwalyanje. Suala lake linapelekwa kwenye Kamati ya
Nidhamu ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kwa ajili ya hatua za
kinidhamu.
Kipa wa Ndanda SC, Wilbert Mweta amefungiwa mechi tatu na
kupigwa faini ya sh. 500,000 (laki tano) kwa kumkanyanga na kutaka kumpiga
mwamuzi Eric Onoka kwenye mechi namba 155 dhidi ya Polisi Morogoro iliyochezwa
Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro. Adhabu hiyo imetolewa kwa mujibu wa Kanuni ya
37(5) ya Ligi Kuu. Kabla ya kufanya kitendo hicho alikuwa ameonyeshwa kadi
nyekundu.
Meneja wa Kagera Sugar, Mohamed Hussein anapelekwa kwenye
Kamati ya Nidhamu ya TFF kwa kutoa lugha ya matusi kwa waamuzi na kutaka
kumpiga mwamuzi msaidizi namba 2, Said Mnonga kwenye mechi namba 158 dhidi ya
Azam FC iliyochezwa Uwanja wa Azam Compex jijini Dar es Salaam.
Naye Kipa Andrew Ntala wa Kagera Sugar amefungiwa mechi tatu
na kupigwa faini ya sh. 500,000 (laki tano) kwa kuingia kwenye vyumba vya
waamuzi na kuwatolea lugha ya matusi mazito ya nguoni baada ya mechi hiyo.
Adhabu hiyo imetolewa kwa mujibu wa Kanuni ya 37(5)(c) ya Ligi Kuu.
Mwamuzi wa mechi kati ya Azam FC na Kagera Sugar, Stephen
Makuka na mwamuzi msaidizi namba mbili Said Mnonga wameondolewa kwenye orodha
za waamuzi wa Ligi Kuu na kufungiwa miezi 12 kwa kushindwa kumudu mchezo kwa
uzembe. Adhabu hiyo imetolewa kwa kuzingatia Kanuni ya 38(1) ya Ligi Kuu.
Pia Kamishna wa mechi hiyo Bevin Kapufi amefungiwa mwaka
mmoja kwa kutoa taarifa isiyo sahihi. Adhabu hiyo imetolewa kwa uzingativu wa
Kanuni ya 39(1) ya Ligi Kuu. Naye Kamishna wa mechi namba 159 kati ya Mbeya
City na Simba, Joseph Mapunda amepewa onyo kutokana na ripoti yake kuwa na upungufu.
Simba imepigwa faini ya sh. 300,000 (laki tatu) kwa
kuzingatia Kanuni ya 14(9) ya Ligi Kuu kwa kutoingia kwenye vyumba vya
kubadilishia nguo (changing room) katika mechi namba 159 dhidi ya Mbeya City
iliyochezwa Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya. Pia Simba imepigwa faini ya sh.
500,000 (laki tano) kwa kutoingia vyumbani wakati wa mapumziko kwenye mechi
hiyo. Adhabu hiyo imetolewa kwa kuzingatia Kanuni ya 14(13) ya Ligi Kuu.
Mgambo Shooting imepigwa faini ya sh. 100,000 (laki moja)
kwa kuchelewa kufika kwenye kikao cha kitaalamu cha maandalizi ya mechi
(technical meeting) dhidi ya Ruvu Shooting. Mechi hiyo namba 161 ilichezwa
Uwanja wa Mabatini mkoani Pwani, na adhabu hiyo imetolewa kwa mujibu wa Kanuni
ya 14(2)(a) ya Ligi Kuu.
LIGI YA MABINGWA WA MIKOA SASA MEI 9
Michuano ya Ligi ya Mabingwa wa Mikoa
(RCL) sasa itaanza Jumamosi Mei 9, 2015 badala ya Jumamosi Mei 2, 2015 kama ilivyokua
imetangazwa awali.
Uamuzi huo umefanyika ili kutoa fursa
kwa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kukamilisha maandalizi ya
mwisho ikiwemo ukaguzi wa viwanja ambavyo vitatumika katika RCL na masuala
mengine ya kumsingi.
Tunaomba radhi kwa usumbufu ambao
utakuwa umejitokeza kutokana na taarifa hii ya kusogeza mbele kuanza kwa ligi,
lakni pia kuzitakia kila la kheri timu zinazoshiriki katika maandalizi yao.
Ratiba ya mashindano
itatolewa/kutumwa leo kama ilivyopangwa awali.
0 comments:
Post a Comment