Balozi
wa Sweden nchini Tanzania Mh. Lennarth Hjelmaker (kulia) na Mratibu
Mkazi wa mashirika ya Umoja wa Mataifa na mwakilishi wa Shirika la
Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) nchini, Alvaro Rodriguez
wakitiliana saini makubaliano ya msaada wa fedha hizo mbele ya waandishi
wa habari (hawapo pichani) wakati wa hafla hiyo iliyofanyika jana
jijini Dar es Salaam kwenye ofisi za ubalozi huo.
Balozi
wa Sweden nchini Tanzania Mh. Lennarth Hjelmaker (kulia) na Mratibu
Mkazi wa mashirika ya Umoja wa Mataifa na mwakilishi wa Shirika la
Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) nchini, Alvaro Rodriguez
wakibadilishana hati hizo za makubaliano hayo.
********
Na Mwandishi wetu
SWEDEN imeyapatia mashirika ya Umoja wa Mataifa yaliyopo hapa nchini jumla ya shilingi bilioni 42/- ili kusaidia katika miradi yake ya maendeleo inayofanya nchiini Tanzania.
Makubaliano ya fedha hizo yametiwa saini jana kati ya Balozi wa Sweden Lennarth Hjelmaker na Mratibu wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa nchini Tanzania Alvaro Rodriguez.
Fedha hizo ambazo ni sawa na dola milioni 24, zitaelekezwa kwenye miradi ya UNDAP inayoendana na sera za Sweden za kuwezesha masuala ya utawala bora, ustawi wa jamii, wanawake na watoto na usawa wa kijinsia.
Kwa mujibu wa Balozi wa Sweden, fedha hizo zitasaidia utekelezaji wa Mkukuta, Mkuza na Matokeo makubwa sasa (BRN) mipango inayofadhiliwa na mashirika ya Umoja wa Mataifa .
Alisema ni matumaini yake kuwa fedha hizo zitaboresha hali ya kufanya biashara, kuwekeza kwa lengo la kutoa ajira zaidi,kuwezesha uchaguzi huru, kuimarisha huduma za jamii, kuimarisha mipango, uwajibikaji na kuimarisha mawasiliano ya radio kwa ajili ya upashanaji habari vijijini ili kusaidia maamuzi yenye mtazamo mpana zaidi miongoni mwa watu wa vijijini.
Katika hafla hiyo Balozi wa Sweden alisema pamoja na kutoa fedha hizo kwa mashirika ya Umoja wa Mataifa, nchi yake itaendelea na makubaliano yaliyofikiwa na serikali ya Tanzania na kuendelea kutoa misaada yake ya kimaendeleo.
Akijibu swali la kwanini wanatoa fedha kwa mashirika ya Umoja wa Mataifa pekee, na kama wameacha kutoa misaada ya moja kwa moja serikalini, Balozi huyo alisema misaada ya taifa hilo imelenga kupata matokeo yanayotakiwa na kwamba itaendelea kusaidia pia taasisi nyingine zisizo za kiserikali na serikali yenyewe.
Aidha Balozi Lennarth Hjelmåker alisema kwamba Tanzania imekuwa mfano bora kabisa wa mashirika ya Umoja wa Mataifa kwa kuwezesha ufanisi mkubwa wa miradi ya maendeleo yaliyolenga kuwawezesha watanzania kupiga hatua mbele na kuhakikisha kuwapo kwa amani.
Alisema wanafurahia kusaidia masuala ya utawala bora, kazi kwa vijana, usawa wa kijinsia na kuwapo kwa uchaguzi huru na wenye amani.
0 comments:
Post a Comment