MABASI mawili yamegongana uso kwa uso wilayani Sikonge mkoani Tabora na
kuua abiria 13, wakiwemo madereva wa mabasi hayo na kujeruhi wengine 73.
Moja ya mabasi hayo, lilikuwa likitokea mkoani Mwanza kwenda Mpanda na
lingine likitokea mkoani Mbeya kwenda Mwanza.
Taarifa kutoka eneo la tukio, ilieleza kuwa mabasi hayo yalipata ajali
hiyo leo saa 10.05 jioni katika eneo la Mlogoro, kilometa tatu kabla ya
kuingia katika mji wa Sikonge.
Mabasi hayo moja linamilikiwa na Kampuni ya AM Investment Namba T 803
ATN, lililokuwa likitokea Mwanza kwenda Mpanda. Lingine ni mali ya
kampuni ya Sabena Namba T 110 ARV, lililokuwa likitokea Mbeya kwenda
jijini Mwanza.
Akizungumza na gazeti hili kwa simu jana jioni, Kaimu Mganga wa Wilaya
ya Sikonge, Dk John Buswelu, alisema hospitali hiyo ilikuwa imeshapokea
miili 13 ya abiria waliokufa, huku mmoja ukiwa kiwiliwili bila kichwa.
Shuhuda wa ajali hiyo aliyekuwa sehemu ya tukio, Suleimani Kambuzi
alidai majeruhi waliotolewa katika ajali hiyo, walikuwa zaidi ya 70.
Alidai wengine walikuwa wakiendelea kutolewa na kupelekwa hospitalini.
Gazeti hili lilimtafuta Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tabora, Suzan Kaganda,
ambaye alikiri kufahamu kutokea kwa ajali hiyo.
Aliongeza kuwa taarifa rasmi ataitoa leo.
Ajali hiyo imetokea wakati
Watanzania hawajasahau ajali iliyotokea wakati wa Sikukuu ya Idd el
Fitri mwezi uliopita, na kuua watu 17 katika eneo la Pandambili wilayani
Kongwa mkoani Dodoma.
Ajali hiyo ilihusisha basi la kampuni ya Moro Best, lenye namba za
usajili T 258 AHV lililokuwa likitoka Mpwapwa kwenda Dar es Salaam.
Basi hilo liligongana uso kwa uso na lori la mizigo, lenye namba za
usajili T820 CKU -T 390 CKT, lililokuwa likitokea Dar es Salaam kwenda
Dodoma.
0 comments:
Post a Comment