Mimi
Dr Cyril August Chami, Mbunge wa Moshi Vijijini (CCM) napenda kueleza
masikitiko yangu kwa taarifa za uzushi na za kutunga kuwa eti mke wangu
asiye na jina amemuua mfanyakazi wetu Mwislamu kwa sababu "marehemu"
alikataa kwenda kanisani.
Mimi sina mfanyakazi wa jina hilo la Mariamu. Wala sina mfanyakazi
mwenye umri wa miaka 16. Hatuna tatizo lolote la mfanyakazi yeyote
kupigwa, achilia mbali kuuawa.
Lakini taarifa hizo ambazo ni za uongo mtupu zimewashtua wengi kwa
sababu zimejengwa katika misingi ya chuki za kidini. Mwandishi alilenga
kuifanya jamii iamini kwamba mke wangu ambaye ni Mkristo anawalazimisha
wafanyakazi wetu wasio Wakristu waikane dini yao na kuwa Wakristo.
Alilenga kuibua chuki dhidi ya Waislamu na familia yangu.
Kwa hakika, mikakati hii ya kuichafua familia yangu inasababishwa na
harakati za ubunge Moshi Vijijini 2015.
Wapinzani wangu wanajua wazi
kuwa hawana hoja ya msingi ya kuwafanya wapiga kura wasinirudishe kwenye
nafasi ya ubunge. Kwenye jukwaa na hata kwenye medani ya maendeleo
wanakwama. Kwa mfano, kabla ya barabara za lami kuanza kujengwa walisema
mimi sina ushawishi wa kuifanya Serikali kuzijenga. Sasa zimejengwa na
zinaendelea kujengwa wanajenga hoja kuwa sihusiki wala Serikali ya CCM
haihusiki, bali ni Benki ya Dunia inajenga!!!
Wananchi wanawauliza kwani
kabla ya Dr Chami kuwa mbunge Benki ya Dunia haikuwepo? Wanakosa hoja!
Hivyo hivyo kwa mashule, maji, vyuo vya ufundi nk.
Kwa hiyo kwa upeo wao wanaona silaha pekee waliyo nayo ni kuzua kashfa
dhidi yangu. Miezi michache iliyopita walizua nimeuza shamba la KNCU kwa
shilingi bilioni 4 wakati mimi sina wadhifa wowote KNCU.
Eti nimeuza
nyumba mbili za Coffee Curing Moshi wakati mimi sina wadhifa wowote
Coffee Curing.
Walipoona tuhuma hizo za kutunga hazijakubalika masikioni mwa wapiga
kura wa Moshi Vijijini, sasa wamezua hili la mke wangu kuua ili
Waislamu wa Moshi Vijijini wanione mtu nisiyefaa.
Sasa mimi napenda kuwauliza maswali haya:
Huyo mke wangu muuaji anaitwa nani? Inaingia akilini kweli kwamba mke
huyo muuaji hafahamiki jina kwa hao "majirani" wetu wa kufikirika?
Binti Mariamu kauawa mji upi? Kwa nini majirani hao wenye uchungu
hawajatoa taarifa kwa RPC wa mkoa au kanda husika?
Maiti kahifadhiwa hospitali ipi? Au "mke" wangu amekaa naye ndani baada
ya kumuua na majirani wamekaa kimya tu?
Kwa desturi za dini ya Kiislamu binti huyo angeshazikwa sasa maana kwa
mujibu wa habari hiyo ya kizushi, "aliuawa" usiku wa kuamkia jana.
Je,
kazikwa makaburi yapi na yako mji gani? Nani kahudhuria hayo mazishi?
Kwa nini vyombo vya habari visituonyeshe hayo mazishi?
Kwa nini RPC mhusika asimkamate huyo mke wa mbunge fedhuli namna hiyo na
muuaji asiyevumilika?
Kwa nini polisi hawajaniita mimi Dr Chami kunihoji kuhusu huyo "mke"
wangu?
Si wanajua niko jimboni Moshi Vijijini na RPC Boaz wa Kilimanjaro
anafahamu niko jimboni, tena jana nimeutembelea msikiti mmoja kwa
minajili ya kuutafutia umeme na maji?
Sote tunafahamu kuwa kuna mkuu mmoja wa mkoa alimuua mtu kwa kumpiga
risasi na alikamatwa akapelekwa mahabusu.
Huyo mke wa Dr Chami ni
maarufu kuliko Mkuu wa Mkoa? Kwa nini asikamatwe tuione sura yake
magazetini?
Majibu ya maswali haya HAYAPO kwa sababu kila kitu kimetungwa kwa
kujenga chuki tu. Hakuna Mariamu, hakuna kipigo, hakuna kifo.
Ila kuna
UBUNGE WA MOSHI VIJIJINI. Ndio unaopiganiwa, hamna kingine.
Napenda kuwaasa wanasiasa wenzangu kuwa Watanzania wa leo si wa jana. Si
jambo rahisi kuwaghilibu kwa staili hii. Waende kwa wananchi wachape
kazi. Wasipofanya hayo wakadhani uongo wa mitandao utawapa ubunge
watashangazwa mwaka kesho 2015.
Mimi naendelea kuwaahidi wapiga kura wangu utumishi wa dhati.
Nawapa
pole ndugu zangu wa Kiislamu kwa usumbufu walioupata. Waislamu wa Moshi
Vijijini wananifahamu kama kiongozi nisiyewabagua kwa sababu ya dini
yao. Wanafahamu kuwa nawapenda na nafahamu kuwa wananipenda sana. Ndiyo
maana wengi wamejiuliza iweje tena mke wangu amwage damu ya Mwislamu kwa
sababu iliyotajwa. Naendelea kuwaahidi Waislamu wote upendo na
ushirikiano siku zangu zote za kuwatumikia.
Wasalaam
Dr Chami.
0 comments:
Post a Comment