Mgeni Rasmi kwenye Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa
Umma Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Utawala Bora Kapteni Mstaafu George Mkuchika
akizungumza kuzindua Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma iliyoanza leo
kwenye viwanja vya Mnazi Mmoja jijini
Dar es Salam.
******
WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais
Utawala Bora, Kapteni Mstaafu George Mkuchika amesema kuwa Tanzania inashika
nafasi ya pili kati ya nchi tano za Shirikisho la Afrika Mashariki katika suala
la Utawala Bora na vita dhidi ya Rushwa.
Waziri Mkuchika amayasema hayo
wakati akizindua Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma iliyoanza leo kwenye
viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam.
Alisema kuwa tangu Serikali ya
Awamu ya Kwanza, Serikali ya Tanzania ilitangaza vita dhidi ya Rushwa na imekuwa
ikiimarisha mapambano dhidi ya adui huyo hadi katika Serikali ya Awamu ya Nne
chini ya Rais Jakaya Kikwete.
“Katika nchi za Afrika
Mashariki suala la Utawala Bora na Vita dhidi ya Rushwa, Tanzania tunashika
nafasi ya pili, Rwanda ni ya kwanza, ya tatu ni Uganda na ya nne ni Kenya”
alisema Waziri Mkuchika.
Waziri Mkuchika alikuwa
akizungumzia madai yanayotolewa na baadhi ya watu hapa nchini kuwa Serikali ya
Tanzania haina dhamira ya kupambana na Rushwa.
Alikanusha madai hayo na
kusema kuwa Serikali ya Tanzania ina dhamira ya kupambana na Rushwa ndio maana
imepitisha Sheria dhidi ya Rushwa,Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa
nchini (Takukuru) ina matawi kila mkoa na kila wilaya.
Alisema kiashiria kingine cha kuthibitisha kuwa
Serikali ya Tanzania inapamabana na Rushwa ni kufikishwa mahakamani kwa watu
wanaotuhumiwa na Rushwa.
Hata hivyo, alibainisha kuwa
mtumishi wa Takukuru hawezi kuwafikisha watu mahakamani bila ya kupata taarifa
kutoka kwa wananchi.
Hivyo aliwataka Watanzania
wote kutambua kuwa wana wajibu wa kupambana na rushwa kwa kutoa taarifa kwa
mamlaka husika ili kufanikisha vita hiyo dhidi ya Rushwa.
Waziri Mkuchika aliwakumbusha
Watanzania kuwa mtumishi yeyote wa umma kumhudumia mwananchi ni haki yake,
hivyo mtumishi anayeomba Rushwa ili atoe huduma anashiriki katika tendo la
Rushwa.
Kutokana na hali hiyo, aliwaomba
watumishi wajiepushe na Rushwa kwani Rushwa inawanyima watu haki, kukiwa na malalamiko
anayepata haki ni yule anayetoa Rushwa.
Baadhi ya watumishi wa Umma wakifuatilia Maadhimisho ya Wiki
ya Utumishi wa Umma yaliyoanza leo kwenye viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es
Salam.
Afisa Habari wa Wizara ya Ushirikiano wa Afrika
Mashariki Robi Bwiru akimueleza jambo mmoja wa wananchi waliotembelea banda la
Wizara hiyo wakati wa Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma iliyoanza leo
kwenye viwanja vya Mnazi Mmoja jijini
Dar es Salam.
Baadhi ya wananchi wakipata maelezo kuhusu shughuli
zinazofanywa na Wizara ya Ushirikiano wa Afrika Mashariki , wakati
walipotembelea banda la Wizara hiyo.
0 comments:
Post a Comment