MNYANGE atakayefanikiwa kuibuka mrembo wa
kitongoji cha Sinza ‘ Redds Miss Sinza 2014’ katika shindano
litakalofamyika kesho Ijumaa kwenye Ukumbi wa Meeda Night Club uliopo Sinza jijini
Dar es Salaam atazawadiwa kitita cha Sh. 300,000.
Akizungumza jana jijini, Mratibu wa
shindano hilo, Tinna Makutika, alisema kuwa mshindi wa pili atajinyakulia Sh. 200,000,
mshindi wa tatu Sh. 100,000 huku warembo wengine waliobakia kila mmoja
ataambulia zawadi ya kifuta jasho ya Sh. 50,000.
Mratibu wa shindano hilo alisema kuwa
maandalizi ya kinyang’anyiro hicho yamekamilika na anaamini Sinza mwaka huu
itafanikiwa kutwaa taji la taifa ambalo linashikiliwa na mrembo kutoka Dodoma.
Alisema kuwa warembo wake wamejiandaa
kuonyesha ushindani na kila mmoja amejipanga kufanya vizuri ili kushinda taji
la Sinza usiku wa leo.
"Mwaka huu nina warembo wazuri na wenye
vigezo vyote, naamini mwaka huu nitarudisha heshima ya watu wa Sinza
ya kufanikiwa kutoa mshindi wa taji la Redd's Miss Kinondoni na Redd's Miss Tanzania mwaka 2014”, alisema
Tinna.
Aliongeza
kuwa wamejipanga kuendeleza mazuri yaliyofanywa na Brigitte Alfred,
ambaye alitwaa taji la taifa na kupata nafasi ya kuitangaza nchi kwenye
mashindano ya dunia ya Miss World.
Alisema pia shindano
hilo linatarajiwa kuwa na burudani mbalimbali ikiwamo bendi mahiri ya muziki wa dansi, FM Academia
‘Wazee wa Ngwasuma’ ambao wanatamba na Chuki ya Nini.
Kiingilio cha juu
katika shindano hilo ni Sh. 10,000 kwa viti maalum na vya kawaida ni Sh. 5,000.
Aliwataja warembo 12
watakaochuana ni Liliani Sandi,Priscar Sarakikya,Agnes Mwikombe,Esta
Wilson,Rose Lucas,Zubeda Saburi,Tuku Harison,Dorine Benne,Farida
Iddy,Qeenlatifa Hashim,Jane Masawe na Wahida Ahmed.
Naye Meneja wa
kinywaji cha bia ya Redd’s Original, Victoria Kimaro, alisema ni muda muafaka
kwa wapenzi wa tasnia ya urembo nchini wanatakiwa kujitokeza kwa wingi
kuhudhuria shindano hilo ili kushuhudia namna kitongoji cha Sinza kilivyo na
bahati ya kutoa warembo wenye ushindani katika fainali za taifa.
Victoria alisema
kuwa wadau wa sanaa ya urembo wanatakiwa kuona sanaa hiyo ni sehemu inayowapa
nafasi wasichana kutimiza ndoto zao na hatimaye kujiendeleza kimaisha.




0 comments:
Post a Comment