Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib
Bilal, akiwa katika mazungumzo na Mwenyekiti wa Kampuni ya JETRO,
Hiroyuki Ishige, wakati walipokutana na kwa mazungumzo akiwa katika
ziara yake nchini Japan, leo Mei 20, 2014.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib
Bilal, akiwa katika mazungumzo na Rais wa JAICA, Akihiko Tanaka,
yaliyofanyika wakati walipokutana kwa mazungumzo akiwa katika ziara yake
nchini Japan, leo Mei 20, 2014. Kulia ni Waziri wa Uchukuzi, Dkt.
Harrison Mwakyembe (wa pili kulia) ni Balozi wa Tanzania nchini Japan,
Salome Sijaona.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib
Bilal, akibadilishana zawadi na Mwenyekiti wa Kampuni ya JETRO, Hiroyuki
Ishige, baada ya mazungumzo yao wakati Makamu Dkt Bilal, akiwa katika
ziara yake nchini Japan, leo Mei 20, 2014.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib
Bilal, akibadilishana zawadi na Waziri wa Biashara, Uchumi na Viwanda wa
Japan, Toshimitsu Motegi, baada ya mazungumzo yaliyofanyika ofisini kwa
Waziri huyo akiwa katika ziara yake nchini Japan, leo Mei 20, 2014.
************
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ameanza leo ziara
ya Kikazi nchini Japan, ziara inayolenga kuongeza ushirikiano baina ya
Japan na Tanzania ikizingatia maeneo ya uwekezaji na ubadilishaji wa
teknolojia baina ya nchi hizi mbili.
Mheshimiwa Makamu wa Rais baada ya
kuwasili nchini hapa na kukutana na viongozi wa Ubalozi wa Tanzania
nchini Japan ulio chini ya Balozi Salome Sijaona, alianza ziara hiyo kwa
kutembelea Ofisi ya Wizara ya Biashara Uchumi na Viwanda na kukutana na
Waziri wa Wizara hiyo Mheshimiwa, Toshimitsu Motegi, ambaye
alimfahamisha Mheshimiwa Makamu wa Rais kuhusu maeneo ambayo Japan
imekuwa ikishirikiana na Tanzania, sambamba na yale ambayo ingetarajia
kushirikiana zaidi katika siku zijazo.
Akiwa wizarani hapo Mheshimiwa Makamu wa Rais
alipata taarifa kuhusu makampuni ya Japan ambayo yana nia ya kuwekeza
Tanzania na kuelezwa namna yalivyojipanga kushirikiana na Tanzania
kutimiza azma zao za uwekezaji na pia akatumia nafasi hiyo kuwaeleza
kuwa Tanzania inashukuru kuona Japan ikitangaza fursa za uwekezaji
nchini Tanzania.
Pia aliufahamisha uongozi wa wizara hiyo kuwa kwa sasa
kuna ushindani mkubwa wa kiuwekezaji nchini Tanzania hasa katika sekta
za mafuta na gesi na hivyo kazi ya Tanzania ni kutazama fursa ambazo
zitakidhi matakwa ya Wananchi wake na kutoa nafasi kwa makampuni ya
kigeni yanayotambua na kuthamini sera za uwekezaji zilizopo nchini huku
yakiwa radhi kuchangia katika kupunguza umaskini nchini badala ya
kutafuta faida peke yake. "Nafahamu kampuni kutoka Japan zina nia njema
ya kustusaidia kukabiliana na umaskini wa wananchi wetu, tunashukuru
sana kwa moyo huo na karibuni kuwekeza Tanzania," alisema.
Baada ya kikao hicho Mheshimiwa Makamu wa Rais
alipata fursa ya kufanya mazungumzo na Mwenyekiti wa JETRO, Hiroyuki
Ishige, ambaye aliongozana na baadhi ya viongozi wa kampuni hi yo na
kuzungumzia nia ya Japan kutanua uwekezaji wa makampuni yao nje ya
Japan, sambamba na Makampuni ya Nje kuwekeza Japan.
Uongozi wa JETRO ulieleza nia yake ya kufungua ofisi
ya kuhamasisha uwekezaji nchini Tanzania na ukafafanua kuwa mazungumzo
ya kufikia lengo hilo yanaenda vizuri huku wakimtaka Mheshimiwa Makamu
wa Rais kuendelea kuwasaidia ili wafanikishe azma hiyo. Balozi wa Japan
nchini Tanzania, Masaki Okada, alifafanua kuwa ujio wa JETRO nchini
Tanzania utafungua ukurasa mpya katika uwekezaji na pia utasaidia nchi
hizi mbili kudumisha uhusiano wake ambao sasa unaakisi katika masuala ya
teknolojia na uchumi.
Sambamba na hilo, Mheshimiwa Makamu wa Rais alipata
nafasi ya kukutana na Ujumbe kutoka JICA, ulioongozwa na Rais wake,
Akihiko Tanaka, ambao uliishukuru serikali ya Tanzania kukubaliana na
miradi mbalimbali wanayoitekeleza nchini Tanzania huku akisisitiza
umuhimu wa kukuza ushirikiano baina ya nchi hizi mbili ili wananchi wa
nchi zote wazidi kunufaika.
Kwa upande wake Mheshimiwa Makamu wa Rais ambaye
katika ziara hii ameambatana na Waziri wa Uchukuzi Dk. Harrison
Mwakyembe alifafanua kuwa, Tanzania inathamini uhusiano wake na Japan
sambamba na mchango wake katika sekta mbalimbali na kwamba Tanzania ina
tamaa kubwa ya kuona urekebishaji wa miundombinu yake hasa Reli ya Kati
maeneo ambayo yamekabidhiwa kwa Japan yanafanyiwa kazi kwa wakati ili
kukuza uchumi wa Tanzania na nchi jirani zinazotegemea Bandari ya Dar es
Salaam katika kupitisha mizigo yake.
0 comments:
Post a Comment