Nafasi Ya Matangazo

April 09, 2014

Mkurugenzi wa ASET, Asha Baraka akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kuingia makubaliano na kampuni ya Proin Promotions Ltd ya kutengeneza kazi zao kwa ubora zaidi. Kampuni hiyo tayari imetengeneza DVD ambazo huwezi kunakili kwa lengo la kupambana na wezi wa kazi za wasanii. kulia ni Meneja Masoko wa kampuni hiyo, Evans Steven na Afisa Mauzo, Kaisi Masoud.
 ********
BENDI ya muziki wa dansi nchini ya African Stars 'Twanga Pepeta', wameingia mkataba maalumu na kampuni ya Proin Promotions Limited kwa ajili ya utengenezaji wa kazi zao. 

Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Mkurugenzi wa Twanga Pepeta, Asha Baraka, alisema mkataba huo una manufaa kwa bendi hiyo kutokana na kutaka kuwanufaisha wanamuziki na wasanii wa nchini kwa ujumla. Baraka alisema kampuni hiyo ambayo awali ilikuwa ikijishughulisha na usambazaji wa kazi za filamu, imeamua kuingia mkataba na bendi yake kutokana na ubora wao. 

Alisema wasanii nchini wanatakiwa kunufaika na kazi wanayoifanya, na Prain wameihakikishia Twanga kuwa kazi zao sasa zimetengenezwa kwa ubora wa hali ya juu kiasi cha kumshinda mtu yeyote kuirudufu. 

"Tunataka maendeleo ya wasanii, tumekuwa tukiwakumbatia zaidi wasanii wa nje, lakini muunganiko wetu sasa utasaidia kuinua hali ya kipato sahihi kwa wanamuziki tulionao," alisema Baraka. 

Kwa upande wake, Ofisa Masoko wa Prain Promotions, Evance Steven, alisema kampuni yao imeamua kuingia kwenye muziki na kuichagua Twanga Pepeta kuwa bendi ya kwanza kutokana na kazi yao wanayofanya katika burudani. 

Steven alisema kazi kubwa waliyoanza nayo katika albamu ya Twanga Pepeta ya Dunia Daraja ni kuhakikisha kuwa haiwezi kunakiliwa (kurudufiwa) upya na maharamia wa kazi za kisanii nchini kama ilivyozoeleka. 

"Tumewahakikishia wenzetu wa Twanga Pepeta kuwa kazi zao sasa ziko salama kuuzwa kihalali kutokana na kuziwekea programu maalumu ya kushindwa kunakilika, hivyo kila mtu atanunua kihalali kazi za bendi hii za Dunia Daraja," alisema ofisa huyo. 

Twanga itaanza kuuza kazi hizo katika kila maonesho yao huku zikionekana kufungwa katika ubora wa hali ya juu alipokuwa akiwaonesha waandishi wa habari utofauti mkubwa uliofanywa na Prain, ambapo pia zina stika maalumu za TRA (Mamlaka ya Mapato Tanzania).
Posted by MROKI On Wednesday, April 09, 2014 No comments

0 comments:

Post a Comment

  • Facebook
  • Twitter
  • Youtube

Labels

Blog Archive

Nafasi Ya Matangazo