Makocha
wa timu za Taifa za Tanzania (Taifa Stars) na Burundi (Intamba Mu Rugamba),
Salum Mayanga na mwenzake Niyungeko Alain Olivier wameahidi burudani ya nguvu
kwenye mechi yao itakayochezwa kesho (Aprili 26 mwaka huu) Uwanja wa Taifa, Dar
es Salaam.
Mechi
hiyo ya kirafiki ambayo ni sehemu ya maadhimisho ya Muungano wa Tanganyika na
Zanzibar itachezeshwa na refa Anthony Ogwayo kutoka Kenya na itaanza saa 10
kamili jioni. Ogwayo atasaidiwa na Gilbert Cheruiyot na Oliver Odhiambo wote
pia kutoka Kenya. Mwamuzi wa mezani atakuwa Israel Mujuni wa Tanzania wakati
Kamishna ni Charles Ndagala.
Mayanga
amesema wanatumia mechi hiyo kama sehemu ya maandalizi ya mechi za mchujo za
Kombe la mataifa ya Afrika, na ameahidi kuchezesha baadhi ya wachezaji
waliopatikana kwenye mpango wa maboresho ya Taifa Stars inayodhaminiwa na
Kilimanjaro Premium Lager.
Naye
Niyungeko amesema amekuja na kikosi imara ambacho pia kitakuwa na washambuliaji
wa Simba, Amisi Tambwe na Didier Kavumbagu wa Yanga, lengo lao ni kuhakikisha
wanapata ushindi kwa vile Taifa Stars imekuwa ikiwasumbua kila wanapokutana
nayo.
Viingilio
katika mechi hiyo ni sh. 5,000 kwa viti vya rangi ya chungwa, bluu na kijani.
Kwa VIP A kiingilio kitakuwa sh. 20,000 wakati VIP B na C ni sh. 10,000.
Wakati
huo huo, Kocha Mkuu mpya wa Taifa Stars, Martinus Ignatius Maria maarufu kama
Mart Nooij atatambulishwa kwa waandishi wa habri kesho Jumamosi (Aprili 26
mwaka huu) saa 8 kamili mchana kwenye ukumbi wa mikutano wa Uwanja wa Taifa.
KENYA YAWASILI
KUIVAA NGORONGORO HEROES
Timu
ya vijana ya Kenya inatarajiwa kuwasili nchini leo (Aprili 25 mwaka huu) saa 1
usiku tayari kwa ajili ya mechi dhidi ya Tanzania (Ngorongoro Heroes).
Mechi
hiyo ya marudiano ya michuano ya Afrika kwa vijana wenye umri chini ya miaka 20
itachezwa Jumapili (Aprili 27 mwaka huu) kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Viingilio katika mechi hiyo vitakuwa sh. 2,000 na sh. 5,000.
Kenya
na Ngorongoro Heroes zilitoka suluhu katika mechi ya kwanza iliyochezwa
Machakos wiki tatu zilizopita. Mshindi baada ya mechi ya marudiano atacheza na
Nigeria katika raundi itakayofuata.
Ngorongoro
Heroes inaendelea kujinoa kwa ajili ya mechi hiyo chini ya Kocha John Simkoko.
Mechi hiyo itachezeshwa na waamuzi kutoka Burundi wakiongozwa na Pacifique Ndabihawenimana
wakati Kamishna ni Tarig Atta Salih kutoka Sudan.
0 comments:
Post a Comment