Watoto mapacha
kutoka wilayani Kyela mkoani Mbeya waliokuwa wamepelekwa na serikali chini ya
Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii kufanyiwa upasuaji mkubwa wa kuwatenganisha
wakiwasili nchini Tanzania kutokea nchini India walipokuwa wakipatiwa matibabu
katika hospitali ya watoto ya Appolo. Kulia ni Mkuu wa Kitengo cha
Magonjwa ya Nje wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii Dkt. Edward Sawe, mama
mzazi wa watoto hao Bi. Grace Joel na Daktari aliyekuwa akiwaangalia nchini
India Dkt.Glory Joseph.
Watoto hao
wakiwa wamebebwa na Daktari aliyekuwa akiwaangalia
nchini India Dkt.Glory Joseph (kushoto) na mama mzazi wa watoto hao Bi. Grace
Joel.
Mama
mzazi wa watoto hao Bi. Grace Joel akiwa
amewabeba watoto wake Elikana Erick (kushoto) na Eliud Erick (kulia) mara baada
ya kuwasili katika Uwanja wa ndege wa kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere
jijini Dar es Salaam.
**********
Na. Aron Msigwa –
MAELEZO
Hatimaye watoto mapacha
kutoka wilayani Kyela mkoani Mbeya waliokuwa wamepelekwa na serikali chini ya
Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii kufanyiwa upasuaji mkubwa wa kuwatenganisha jana
jioni wamerejea nchini wakitokea nchini India katika hospitali ya watoto ya
Appolo walikokuwa wanapatiwa matibabu.
Mara baada ya kuwasili
katika Uwanja ndege wa Kimataifa wa
Mwalimu Julius Nyerere wakiwa wameambatana
na mama yao mzazi Grace Joel na Daktari aliyekuwa akiwaangalia nchini
India ambaye pia alikuwa masomoni akisomea magonjwa ya Moyo kwa watoto Dkt.
Glory Joseph wamepokewa na Mkuu wa Kitengo cha Magonjwa ya Nje wa Wizara ya
Afya na Ustawi wa Jamii Dkt. Edward Sawe
na baadhi ya wauguzi kutoka Taasisi ya Mifupa (MOI) .
Mapacha hao wa kiume
wakiwa wenye furaha na afya njema
walichukuliwa katika gari maalum na kupelekwa katika Taasisi ya Mifupa (MOI)
ambako watakaa kwa muda mfupi na kisha kuruhusiwa kuelekea wilayani Kyela
jijini Mbeya ambako ndiko walikozaliwa.
Kwa upande wake mama mzazi wa watoto hao akizungumza
kwa furaha mara baada ya watoto wake kupatiwa matibabu ya kuwatenganisha kwa
mafanikio makubwa amesema kuwa sasa maisha yake yamebadilika na ataishi kwa
furaha na watoto wake.
“Najisikia furaha sana
kwa hatua niliyofikia mpaka hapa watoto wangu Eliudi na Elikana sasa ni wazima
naishukuru sana Serikali kupitia Wizara ya Afya kwa msaada ilionipatia”
amesema.
Kwa uipande wake Daktari
aliyekuwa akiwaangalia nchini India ambaye pia alikuwa masomoni akisomea
magonjwa ya Moyo kwa watoto Dkt. Glory Joseph akizungumzia matibabu ya watoto
hao nchini India amesema kuwa hatua ya kuwatenganisha imekamilika na mwezi wa 8
mwaka huu watarudi tena nchini India kwa
ajili ya uchunguzi na matibabu zaidi
ya afya zao.
“Ni kwamba watoto hao
wametenganishwa, kwa wakati huu wanaelekea MOI ambako watakaa kwa muda na
baadaye wataruhusiwa kwenda kwao Mbeya kujumuika na jamaa zao” amesema.
Kwa upande wake msemaji
wa wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii Bw. Nsachris Mwamwaja amesema kuwa watoto
hao waliwasili jana jioni na ndege ya shirika la ndege la Oman baada ya
kumaliza matibabu ya awamu ya kwanza.
Amesema upasuaji huo
mkubwa wa kuwatenganisha watoto hao ulichukua saa 18 na kufafanua kuwa kati ya hizo saa 13 zilitumika kutenganisha viungo
vilivyoungana sehemu ya chini ya uti wa mgongo,sehemu ya utumbo mpana,njia ya
mkojo,kibofu cha mkojo na sehemu za uume huku saa 5 zikitumika kuunganisha
sehemu zilizotenganishwa.
“Kumbukumbu zinaonyesha
kuwa mpaka sasa duniani upasuaji wa aina hii umefanikiwa mara tano kutenganisha mapacha watoto wa kiume walioungana”
amesisitiza.
Ameongeza kuwa matibabu
hayo ni juhudi za serikali katika kuhakikisha kuwa huduma za afya zinatolewa kwa kila mwananchi kila inapowezekana na kutoa
wito kwa jamii kujenga utaratibu wa kuwafikisha mapema kwenye vituo vya afya wale
wote wenye matatizo ya kiafya badala ya kuwafikisha pindi hali zao zinapokuwa
mbaya.
0 comments:
Post a Comment