Katibu wa kamati ya serikali ya maandalizi ya mbio za
Uhuru marathon Tanzania Innocent Melleck Katikati akizungumza na waandishi wa
habari jijini Dar Es Salaam juu ya udhamini wa kampuni ya bia nchini Tbl
kupitia kinywaji chake kisicho na kilevi cha GrandMalt ambapo kimetoa jumla ya
shilingi milioni ishirini (20,000,000) kushoto ni mkurugenzi msaidizi wa idara
ya habari maelezo Tiganya Vincent na kulia ni meneja masoko wa Tbl Fimbo
Butalla.
******
KAMPUNI ya Bia Tanzania
(TBL) kupitia kinywaji chake kisicho na kilevi cha GrandMalt imejitokeza
kudhamini mbio ndefu za Uhuru, Uhuru Marathon, kwa kiasi cha Sh milioni 20.
Akitangaza udhamini huo jijini
Dar es Salaam jana, Meneja Masoko wa TBL, Fimbo Butallah alisema, wameona ni
vyema kudhamini mbio hizo kwani zina lengo zuri zaidi la kuimarisha umoja,
amani na mshikamano miongoni mwa Watanzania.
Kuhusu udhamini huo,
Butallah alisema, Sh milioni 13.4 zitatumika kwa ajili ya kutoa zawadi
mbalimbali kwa washindi, huku Sh milioni 6.6 zikiwa ni kwa burudani
zitakazofanyika siku ya mkesha wa kuamkia mbio hizo.
“Ukweli ni kwamba taifa
lolote duniani linapigania kuwa na uchumi imara na pasipokuwa na amani hakuna
uchumi utakaoweza kukua, hivyo TBL kama kampuni inayotengeza bidhaa za hapa
nyumbani imeona ni muhimu kuungana na Watanzania wenzetu wote kuhakikisha kuwa
mbio hizi zinafanyika katika hali ya mafanikio makubwa na kuwa za kufana zaidi.
“Nitoe rai pia kwa
makampuni ya ndani na nje ya nchi kujitokeza na pia kuendelea kutoa chochote
walichonacho ili kufanikisha mbio hizi zenye kubeba dhima ya Taifa letu lakini
pia wajitokeze kwa wingi kushiriki mbio hizi.
“Kwa zawadi hizi tulizotangaza
leo tunaamini zitakuwa kichocheo kwa wakimbiaji wetu kufanya mazoezi ya kutosha
ili kuhakikisha fedha hizi zinabaki ndani ya ardhi ya Tanzania,” alisema.
Naye Katibu wa Kamati ya
Uhuru Marathon, Innocent Melleck aliwaomba Watanzania kujitokeza kwa wingi
kushiriki mbio hizo ambazo zina nia kubwa ya kutukumbukusha wajibu wetu wa
kutunza na kulinda amani, umoja na mshikamano miongoni mwetu.
Alisema zawadi kwa mshindi
wa kwanza inatarajiwa kuwa Sh 1,500,000 kwa wakimbiaji wa kilomita 21 na 42,
hii ni kwa upande wa wanawake na wanaume.
Mshindi wa pili kwa mbio
hizo iwe kwa upande wa wanawake au wanaume kwa kilomita 21 au 42 ataondoka na
Sh 800,000 wa tatu Sh 600,000 wanne Sh 300,000 na watano apata Sh 150,000.
Mbio hizi zinatarajiwa
kufanyika jijini Dar es Salaam hapo Desemba 8, mwaka huu ambapo zitaanzia na
kumalizikia katika Viwanja vya Leaders club.
Rais Jakaya Kikwete
anatarajiwa kushiriki mbio hizi, huku wabunge zaidi ya 100 wakiongozwa na Spika
Anne Makinda wakiwa wamejisajili kwa ajili ya kushiriki.
Mbio hizo zimegawanywa
katika makundi makuu manne ambayo ni kilomita 3 kwa ajili ya viongozi, kilomita
5 kwa watu wote na kilomita 21 na 42 ambazo ni maalum kwa wakimbiaji nguli.
0 comments:
Post a Comment