Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi Duniani
(UNHCR), limeiomba radhi Serikali ya Tanzania kufuatia taarifa waliyoitoa
kwenye Mkutano wa 64 wa Kamati Tendaji (EXCOM) ya shirika hilo uliofanyika
Geneva, Uswisi tarehe 30 Septemba hadi tarehe 4 Oktoba, 2013.
Katika taarifa
yao kuhusu Afrika, UNHCR ilieleza kuwa Tanzania imewafukuza Wakimbizi wa Rwanda
na Burundi katika operesheni ya kuwaondoa Wahamiaji haramu inayoendelea nchini.
UNHRC imeiomba radhi Serikali ya Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania kupitia barua yake ya tarehe 2 Oktoba, 2013. Barua hiyo imeandikwa
na Mkurugenzi wa UNHCR Kanda ya Afrika Bw. George Okoth-Obbo kwenda kwa Naibu
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhe. Pereira Ame Silima aliyeongoza ujumbe wa Tanzania katika Mkutano
huo unaofanyika kila mwaka.
Katika barua hiyo, UNHCR imeeleza kusikitishwa na
taarifa hiyo ambayo si ya kweli na imekiri kwamba Serikali ya Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania imekuwa ikishirikiana kwa karibu na UNHRC katika ngazi
zote kuhakikisha kwamba hakuna mkimbizi anayerejeshwa kwao katika zoezi la
kuwakamata na kuwarejesha kwao wahamiaji haramu linaloendelea nchini Tanzania.
Aidha, Bw. Okoth Obbo ameeleza kuwa UNHCR na Jumuiya ya Kimataifa kwa ujumla inatambua
na kuthamini kwa dhati mchango mkubwa ambao Tanzania imeutoa na inaendelea
kuutoa katika kuwahifadhi wakimbizi wa mataifa mbalimbali kwa kipindi cha
takribani miaka 40.
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imepokea
kauli hiyo na kueleza kwamba inatarajia na inaamini kwamba UNHCR itaendelea kutoa
taarifa sahihi zenye kutoa picha halisi inayoonesha namna Serikali ya Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania inavyotekeleza wajibu wake kuwalinda na kuwahifadhi Wakimbizi kwa mujibu
wa Sheria za nchi na mikataba ya Kimataifa ambayo nchi imeridhia.
Imetolewa
na Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali
WIZARA YA MAMBO YA NDANI YA NCHI
06, Oktoba, 2013
0 comments:
Post a Comment