MWANDISHI wa habari wa ITV,
Ufoo Saro, aliyejeruhiwa kwa risasi jana asubuhi, alilazimika kuvumilia
majeraha ili kujiokoa yeye mwenyewe na wadogo zake watatu waliokuwa wakipigwa
risasi, baada ya mama yake mzazi, Anastazia Saro (58), kuuawa.
Mauaji hayo ya kusikitisha,
yalifanyika katika eneo la Mbezi Kibwerere, nyumbani kwa mama yake Ufoo, ambako
alikuwa akiishi na wadogo zake Ufoo ambao ni Goodluck, Innocent na Jonas.
Mtuhumiwa wa unyama huo ametajwa kuwa ni Anthery Mushi, ambaye ni baba mtoto wa
Ufoo na siku ya tukio wawili hao walitokea Mbezi Magari Saba nyumbani kwa Ufoo,
kwenda kuzungumza kifamilia na mama mzazi wa mwandishi huyo.
Mushi (40) ni Mhandisi wa
Kitengo cha Mawasiliano katika Shirika la Umoja wa Mataifa (UN) nchini Sudan na
aliwasili nchini juzi na kwenda moja kwa moja nyumbani kwa Ufoo eneo la Mbezi
Magari Saba.
Kwa mujibu wa Kamanda wa
Polisi Mkoa wa Kinondoni, Camillius Wambura, Ufoo amejeruhiwa katika paja na
tumboni, mama yake mzazi alikufa papo hapo baada ya kupigwa risasi ya kifuani
na mtuhumiwa Mushi ambaye naye alijiua baada ya kujipiga risasi kichwani katika
eneo la kidevuni. Akizungumza na gazeti hili jana mdogo wake Ufoo, Goodluck
alisema:
Walikuja wakiwa pamoja (Ufoo
na Mushi) mapema alfajiri wakiwa ndani ya gari ya Ufoo, saa 12 na kabla ya
kuingia ndani, alitusalimia kisha wakaingia sebuleni na kuanza mazungumzo na
mama.
SOMA ZAIDI BOFYA: HABARILEO ONLINE
0 comments:
Post a Comment