Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Mheshimiwa Dkt. Dorothy Gwajima, amepongeza mchango wa sekta binafsi na mashirika yasiyo ya kiserikali katika kuimarisha ustawi wa jamii, hususan watoto, vijana na familia, wakati wa ziara yake ya kutembelea miradi ya SOS Children’s Villages Tanzania iliyofanyika Ngaramtoni, wilayani Arumeru mkoani Arusha.
Dkt. Gwajima amesema ameridhishwa na utekelezaji wa programu zinazolenga malezi chanya, ulinzi wa mtoto, maendeleo ya awali ya mtoto (ECD) na uwezeshaji wa kiuchumi kwa vijana na familia, akisisitiza kuwa jitihada hizo zinaendana na sera na miongozo ya Taifa. Amesema malezi bora na mazingira salama kwa watoto ni msingi wa kujenga Taifa imara.
Aidha, amesisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya Serikali, mashirika ya kiraia na jamii katika kuhakikisha utekelezaji wa programu za maendeleo una matokeo endelevu, huku akiwataka wadau kuendelea kuzingatia mipango ya Taifa, hususan katika kukomesha ukatili dhidi ya wanawake na watoto.
Katika ziara hiyo, Waziri Gwajima ameshiriki kukabidhi pikipiki 15 zenye thamani ya shilingi milioni 40 kwa vijana wanufaika wa miradi ya SOS Children’s Villages Tanzania, akibainisha kuwa hatua hiyo inalenga kuwawezesha vijana kujitegemea kiuchumi kupitia ajira binafsi na ujasiriamali.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Arumeru, Mhe. Seleman Msumi, amesema Serikali itaendelea kushirikiana na wadau wa maendeleo katika kuimarisha ustawi wa watoto, vijana na familia, akipongeza mchango wa SOS Children’s Villages Tanzania katika malezi, ulinzi wa mtoto na uwezeshaji wa vijana wilayani humo.
Naye Mkurugenzi wa SOS Children’s Villages Tanzania, Thomas Kipng’ili, amesema kupitia Mradi wa Arusha Re-Innovation uliotekelezwa kwa miaka minne, shirika limewafikia vijana zaidi ya 1,000, ambapo 229 waliwezeshwa mitaji. Amesema mradi huo pia umewezesha walezi wa malezi mbadala 450, watoto 3,538 na familia 1,211 katika Halmashauri za Jiji la Arusha, Arusha DC, Meru na Karatu. Jumla ya shilingi milioni 173.5 zilitolewa kuwawezesha wanufaika 121, hatua iliyosaidia kuboresha ustawi wa watoto 346 waliokuwa katika mazingira hatarishi.














0 comments:
Post a Comment