Naibu Katibu, Tume ya Utumishi wa Umma Bw.Edwin
Mikongoti akieleza kwa waandishi wa Habari kuhusu utekelezaji wa mpango wa serikali
wa kukasimu madaraka kwa wakuu wa
shule, vyuo na walimu wakuu kuhusu usimamizi wa utumishi
wa walimu ili kuongeza ufanisi,wakati wa Mkutano uliofanyika leo jijini Dar es Salaam,
katika ukumbi wa Idara ya Habari(MAELEZO).
Katibu
Msaidizi, Idara ya Utumishi wa Walimu,Tume ya Utumishi wa Umma(kulia) akiwaeleza
waandishi wa habari faida za mfumo wa ugatuaji madaraka ikiwa ni pamoja na
kuongeza ufanisi sehemu za kazi.wakati wa mkutano na waandishi wa habari uliofanyika
leo Jijini Dar es Salaam, katika ukumbi wa Idara ya Habari(MAELEZO).kushoto ni
Katibu Msaidizi, Idara ya Utumishi wa Walimu,Tume ya Utumishi wa Umma Bi.
Evelyne Omari.
Idara ya Utumishi wa
Walimu ya Tume ya Utumishi wa Umma kwa Sheria ya Utumishi wa Umma Na.8 ya 2002
Kifungu 6(4), Kanuni Na. 6(h) na Na. 35(2)(b) za Kanuni za Utumishi wa Umma za
Mwaka 2003 imepewa Mamlaka ya Kushughulikia Masuala ya Ajira na Nidhamu kwa
Walimu wote walio katika Utumishi wa Umma.
Kwa Mujibu wa Kifungu
21(2) cha Sheria ya Utumishi wa Umma Na. 8 ya Mwaka 2002 kama ilivyorekebishwa
na Sheria Na.18 ya Mwaka 2007 na kwa Kanuni Na.118 ya Kanuni za Utumishi wa
Umma ya mwaka 2003, Tume ya Utumishi wa Umma imepewa uwezo wa kukasimisha
madaraka yake kwa Wakuu wa Shule, Vyuo na Walimu Wakuu. Masuala yanayokasimishwa ni yale ya
kiutumishi na ushughulikiaji wa makosa madogo madogo ya kinidhamu kwa Walimu na
Wakufunzi walio vyuoni, Walimu wa Shule za Sekondari na Shule za Msingi.
Ili kuwezesha ufanisi
katika utekelezaji wa masuala ya kiutumishi Wakuu wa Vyuo vya Ualimu/ Vyuo
vya Maendeleo ya Jamii, Wakuu wa Shule na Walimu Wakuu wanatakiwa
kuwajibika katika kuwaelimisha Walimu taratibu za masuala ya ajira katika
maeneo ya:- Ajira na Usajili; Kuthibitisha kazini Walimu; Kubadilisha kazi/cheo
Walimu; Kupandisha vyeo Walimu.
Aidha watashughulikia
pia makosa madogo madogo ya kinidhamu na kutoa adhabu. Madaraka yamekasimiwa
kwa makosa ambayo kama yakithibitika adhabu zake kwa mujibu wa Kanuni Na. 118
ya Kanuni za Utumishi wa Umma, 2003 zitakuwa ni:- Onyo; Kusimamisha nyongeza ya
mshahara; Kufidia hasara au sehemu ya hasara ambayo mtumishi ataisababishia
serikali kutokana na kukosea au uzembe wake; na Karipio.
Utaratibu wa namna ya Utekelezaji wenye ufanisi wa
masuala yote yaliyokasimiwa ni kama ifuatavyo;-
Wakuu wa Shule / Vyuo na
Walimu Wakuu watatekeleza majukumu yao kwa kuzingatia Sheria, Kanuni, Taratibu
na Miongozo iliyopo na itakayokuwa inatolewa.
Mkuu wa Chuo, Shule au
Mwalimu Mkuu atawajibika kusimamia kikamilifu utekelezaji wa majukumu
yaliyokasimiwa kwake.
Masuala yote
yatakayoshughulikiwa katika mchakato ulioelezwa, ikiwa ni pamoja na vielelezo
na kumbukumbu zote za vikao zitatakiwa kutunzwa vizuri kwa matumizi ya baadaye.
Katibu wa TSD Mkoa
atakuwa na wajibu wa kushauri Wakuu wa Shule, Vyuo na Walimu Wakuu juu ya
uzingatiaji wa Sheria, Kanuni, Taratibu na Miongozo katika kutekeleza majukumu
waliyokasimishwa.
Mawasiliano kati ya Mkuu
wa Chuo/Shule, Mwalimu Mkuu na Mamlaka nyingine yatakuwa ni kwa njia ya
maandishi.
Iwapo Mkuu wa Shule/Chuo
au Mwalimu Mkuu atatenda kosa la kinidhamu (miongoni mwa makosa madogo madogo)
au hatatoa taarifa/atakataa kutoa taarifa au ataficha baadhi ya taarifa, Katibu
TSD Wilaya (Mamlaka yake ya Nidhamu) ataweza kuchukua hatua kwa kuzingatia
Kanuni 43 Sehemu B ya Jedwali la kwanza la Kanuni za Utumishi wa Umma, 2003.
Mafunzo/ Maelekezo kwa
Wakuu wa Shule au Vyuo na Walimu Wakuu kwa kushirikiana na Waajiri yatolewe na
pia kuwepo na mafunzo ya mara kwa mara.
Matarajio ya Tume ya Utumishi wa Umma kwa kukasimu
madaraka kwa Wakuu wa Shule, Wakuu wa Vyuo vya Ualimu / Vyuo vya Maendeleo ya
Jamii na Walimu Wakuu ni kwamba;- Mfumo huu utasaidia kushughulikia masuala ya
kiutumishi ya Walimu kwa haraka zaidi na kwa ufanisi; Badala ya kila Mwalimu
kuacha kufundisha darasani kwa lengo la kufuatilia masuala yake ya kiutumishi
Wilayani, sasa kutakuwa na utaratibu wa Mkuu wa Shule/Chuo au Mwalimu Mkuu
kuona kuwa ni wajibu wake na kwamba atawajibika iwapo Walimu walio chini yake
watakosa kupata huduma za kiutumishi.
Taarifa sahihi za Walimu
zitapatikana kutokana na Tange
itakayoandaliwa katika ngazi ya Chuo/Shule. Kudhibiti udanganyifu wowote
utakaofanywa na Walimu kama vile vyeti vya kughushi, viwango vya elimu, vyeo
walivyonavyo. Kuhakikisha Walimu wanapata ajira rasmi na kusajiliwa ndani ya
miezi mitatu tangu kuajiriwa.
Kusimamia vema zoezi la
kuthibitishwa kazini na kupandishwa vyeo; Kuchukua hatua mapema kwa wanaotenda
makosa ya kinidhamu; Kuamsha ari ya kazi na usimamizi wa maadili ya kazi ya
ualimu kwa karibu zaidi.
0 comments:
Post a Comment