Afisa
Uhusiano wa Mamlaka ya Chakula na Dawa Bi. Gaudensia Simwanza KUSHOTO akieleza
kwa waandishi wa Habari kuhusu mpango wa mafunzo na Ufuatiliaji kwa wazalishaji
wadogo wa bidhaa za Chakula unaoratibiwa na mamlaka hiyo, wakati wa mkutano uliofanyika
ukumbi wa Idara ya Habari leo Jijini Dar es Salaam KULIA ni Mkaguzi wa Chakula
toka Mamlaka Hiyo Bw. John Mwingira.
Ndugu wanahabari,
Napenda
kwa heshima na taadhima kutumia fursa hii kwa niaba ya Menejimenti ya TFDA na
wafanyakazi wote kwa ujumla kuwakaribisha katika mkutano huu. TFDA ni taasisi ya Serikali iliyopo chini ya
Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii iliyoundwa chini ya sheria namba 1 ya
Chakula, Dawa na Vipodozi Sura 219 kwa
lengo la kudhibiti ubora na usalama wa chakula, dawa,
vipodozi na vifaa tiba ili kulinda afya za wananchi. Hii inamaanisha kuwa wanaolindwa ni sisi sote ikiwa ni
pamoja na jamaa zetu na wananchi kwa ujumla.
Ndugu wanahabari,
Leo
tumekutana hapa kwa lengo la kupeana taarifa kuhusu mkakati wa TFDA katika
kuwaendeleza wajasiriamali wa chakula kwa lengo la kulinda afya ya walaji, lakini pia kufanya vyakula hivyo
kuweza kumudu ushindani wa soko la ndani na nje na kuleta matokeo makubwa sasa.
Ndugu wanahabari,
Suala la usalama wa vyakula ni la msingi kwa sababu lina
athari kubwa kiafya, kiuchumi na kijamii.
Hata
hivyo, kama hazikudhibitiwa ipasavyo matumizi ya bidhaa hizi yanaweza kuleta
madhara makubwa ikiwa ni pamoja na kusababisha ulemavu, kupoteza maisha na hata
kudhoofisha uchumi wa nchi. Kwa sababu hiyo TFDA kama
taasisi iliyopewa dhamana ya usimamizi wa bidhaa hizo inahakikisha kwamba
vyakula vinavyouzwa katika soko la Tanzania vinakidhi viwango vya usalama,
ubora na ufanisi.
TFDA ina majukumu mengi kwa mujibu wa Sheria. Miongoni
mwa majukumu hayo ni pamoja na udhibiti wa uhifadhi, usafirishaji, usindikaji,
uagizaji na usambazaji vyakula. Katika kutekeleza jukumu lake, TFDA inasajili
majengo yote yanayotumika katika usindikaji wa vyakula ikiwa ni pamoja na
utoaji wa vibali vya usindikaji, uingizaji na usafirishaji nje vyakula.
Majukumu mengine yanayofanywa na TFDA ni pamoja na ufuatiliaji usalama wa
vyakula kwenye soko na utoaji wa elimu kwa wadau mbalimbali.
Ufanisi
wa utekelezaji wa majukumu haya unawezekana kutokana na mifumo mizuri ya utendaji kazi iliyojiwekea
ikiwa ni pamoja na kufanya kazi kulingana na viwango vya kimataifa vya ISO
9001: 2008.
Ndugu wanahabari,
TFDA kama taasisi ya udhibiti wa vyakula, tunatambua kuwa
tuna wajibu wa kuwasaidia wasindikaji wadogo wa vyakula ili waweze kukua na
kuzalisha vyakula kwa mujibu wa Kanuni bora za uzalishaji ili viweze kumudu
ushindani wa soko la ndani na nje kutokana na biashara huria na kuzalisha
chakula salama.
Takwimu zinaonesha asilimia 75 ya viwanda vya vyakula
nchini ni viwanda vidogo (Kwa mujibu wa upembuzi yakinifu uliofanyika 2004/5) ambapo
kukua kwa viwanda hivi kutakuwa na mchango mkubwa katika; kuongeza ajira na
kipato katika ngazi ya kaya, kukuza kilimo cha mazao ya chakula kutokana na
kuwepo na soko la mazao ya vyakula na kuchangia katika pato la taifa.
TFDA inatambua kuwa viwanda vidogo vina nafasi kubwa ya
kuchangia katika pato la Taifa kutokana na uwingi wake lakini pia vinaweza
kutoa mchango mkubwa katika kuleta athari za kiafya ikiwa bidhaa zake
hazitakidhi viwango vya usalama na ubora.
Ndugu wanahabari,
Kwa kuzingatia mambo hayo niliyotaja, TFDA imeamua kuja
na mkakati wa kuwafundisha wajasiriamali wadogo wa vyakula ili kuwawezesha wasindikaji hawa kujua sheria, kanuni na miongozo
inayohusu usindikaji wa chakula salama pamoja na kuongeza kiwango cha
uzingatiaji wa kanuni bora za uzalishaji wa vyakula.
Hadi sasa mafunzo hayo yametolewa kwa wajasiriamali 417
kutoka katika Kanda zote katika mikoa ya Dar es Salaam (90), Singida (44),
Mbeya (76), Arusha (54), Dodoma (98) na Mwanza (55).
Ndugu
wanahabari,
Aidha, kutoka mwaka 2012/13, TFDA imekuwa inaendesha
mpango wa majaribio kwa wasindikaji wadogo wa mafuta ya alizeti mkoani
Singida ili kuelekeza namna ya kuboresha
uzingatiaji wa matakwa ya Sheria kuhusu misingi ya usafi na uzalishaji bora.
Mpango huu umehusisha hatua mbalimbali ikiwa ni pamoja
na;
i.
Kufanya tathmini ya kiwango cha uzingatiaji wa sheria
ii.
Kuainisha maeneo yenye mapungufu
iii.
Kuandaa mafunzo yanayozingatia mapungufu yaliyojionesha
iv.
Kuwasilisha taarifa ya tathmini kwa wadau pamoja na wasimamizi wa sheria
katika eneo husika
v.
Kukubaliana namna ya kutatua upungufu na kuwa na ratiba ya utekelezaji kwa
mambo ya muda mfupi, muda wa kati na muda mrefu
vi.
Ufuatiliaji wa makubaliano
vii.
Tathmini ya jumla kwa makubaliano ya muda mfupi na wa kati ili kujua
kiwango cha utekelezaji.
Lengo la mpango huu ni kusambazwa nchi nzima ikiwa utaleta
matokeo mazuri kwa mkoa huu wa Singida ambao ni wa majaribio ifikapo mwaka
2016/17.
Ndugu
wanahabari,
Kwa
kuhitimisha, TFDA inatoa shukurani kwa ushirikiano ambao mmekuwa mkiuonesha
katika kutoa taarifa za kiudhibiti pale inapotokea pamoja na kuelimisha jamii.
Rai yetu
kwenu ni kuendelea kutumia kalamu zenu katika kuwaondolea hofu wananchi kuhusu
usalama na ubora wa bidhaa za chakula, dawa, vipodozi na Vifaa tiba vilivyopo
katika soko kutokana na mifumo thabiti iliyowekwa na TFDA.
Aidha, tunatoa
wito kwa wananchi kwamba ikiwa mtu atabaini au kuwa na mashaka juu ya usalama
na ubora wa bidhaa hizo basi asisite kuwasiliana nasi kupitia ofisi zetu za
Makao Makuu na za Kanda zilizopo Extenal Mabibo, Mwanza, Arusha, Mbeya, Dodoma
na Ofisi za Waganga wakuu wa Mikoa na Wilaya au kutoa taarifa katika kituo
chochote cha polisi kilicho jirani naye.
0 comments:
Post a Comment