Katibu Mtendaji Bodi ya Filamu, Bi. Joyce Fissoo
akionyesha juu filamu ya “He hurts Me” kuhashiria uzinduzi
rasmi wa filamu hiyo uliofanyika hivi karibuni katika ukumbi wa Mbezi Garden
jijini Dar es Salaam.
Mtengenezaji wa filamu ya “He
hurts Me” Bi. Hilda Ngaja (kushoto) akiwa katika picha ya pamoja na mme
wake Mr. Mwambene (kulia) wakati wa uzinduzi wa filamu yake uliofanyika katika
ukumbi wa Mbezi Garden jijini Dar es Salaam.
********
Benedict
Liwenga-MAELEZO.
Katibu mtendaji Bodi ya Filamu Tanzania Bi.
Joyce Fissoo amezindua filamu mpya ya “He hurts me” (ameniumiza au amenitenda), filamu ambayo imetengenezwa na Bi. Hilda Ngaja
hivi karibuni jijini Dar es Salaam.
Bi. Fissoo ametoa pongezi kwa msanii huyo na
Kampuni ya Hilderly Straight
Film kwa kuthubutu kwao na ameongeza kuwa ana imani kuwa wadau
haowataendelea kuzalisha filamu bora, zenye weledi, maadili na zinazoweza
kuingia katika soko la ushindani. Pia amewashukuru washiriki wote kwa kushiriki kwao kikamilifu katika
kufanikisha filamu hiyo.
Bi. Fissoo amesema
kuwa filamu ya “He Hurts Me” (ameniumiza au amenitenda) ni kati ya filamu
zinazolenga kutoa elimu katika jamii na ni filamu inayoweza kuonwa na wanajamii
kwani imejikita katika kuelimisha, kuburudisha, kuadabisha na ni filamu
inayofaa kuingia sokoni.
“Maudhui mahususi ya filamu hii kwetu sote na jamii kwa ujumla
ni katika kutukumbusha umuhimu wa kuwapa
malezi mema watoto wetu, jamii zinazotuzunguka zina watu wa aina na tabia
mbalimbali ambazo kwa kiasi kikubwa zinaathiri nguvu kazi ya taifa”. Alisema
Bi. Fissoo.
Aidha, Bi. Fissoo amezungumzia suala kubwa juu
ya malezi kwa watoto na vijana pia akaongeza kuwa ujio wa filamu hii utakuwa ni
chachu na mchango mkubwa katika malezi na umekuja wakati ambapo taifa
linahitaji wazazi na walezi kushiriki
ipasavyo katika kuwezesha watoto na
vijana kukua katika misingi ya malezi bora.
Kwa upande mwingine
Katibu Mtendaji huyo amegusia masuala ya ukuaji wa tasnia ya filamu nchini na amesema kuwa tasnia hii imeendelea kukua
kwa kasi sana na hii inadhihirishwa na idadi kubwa ya filamu zinazozalishwa.
“Vijana na watu wa
makundi mbalimbali wamejikita katika tasnia hii. Ni ukweli usiopingika kuwa
tasnia ya filamu inatoa ajira nyingi”. Alisema Bi. Fissoo.
Bi. Fissoo amegusia pia masuala ya utamaduni na
jinsi gani utamaduni unavyoweza kumuathiri ama kumnufaisha mtu hivyo
amesisitiza kuzienzi tamaduni zetu.
“Napenda
kuwakumbusha waandaaji wa filamu na watengenezaji filamu wote nchini
kutengeneza filamu zisizodhalilisha , zisizolenga kuuza tu bali ziwe
zinazolinda maadili, zenye kutumia rasilimali , mandhari na lugha yetu ya
kiswahili katika kutangaza utaifa na utamaduni wetu ; hata majina ya filamu
zetu ni vema yawe kwa lugha ya kiswahili.Tupende na kuenzi utamaduni, maadili
na lugha yetu”. Alisisitiza Bi. Fissoo.
Bi. Fissoo alimalizia hotuba yake kwa kuwaasa wadau
wote wa filamu wakiwemo watengenezaji na wasambazaji wa filamu kuheshimu Sheria na Kanuni zinazosimamia
tasnia ya filamu nchini ambapo kwa sasa mwitikio wake umeanza kuwa mkubwa pia
amewasihi kupeleka sokoni filamu
zilizokamilisha taratibu zote na zilizowekwa stamp za TRA kwani Stamp hizo
zina lengo la kuondokana na wizi wa kazi za wasanii pia amewasihi wadau wote
kuunga mkono juhudi za serikali za kurasimisha tasnia za filamu na muziki kwani
nia ya urasimishaji huu ni kurejesha nidhamu na hadhi katika tasni hizi na
kuondokana na kilio cha muda
mrefu ambacho kwa kiasi kikubwa kimefanya wasanii wa filamu na muziki
kutonufaika na jasho lao.
Filamu ya “He hurts
Me” (ameniumiza au amenitenda) imekaguliwa na Bodi na kupewa daraja 16 yaani inaruhusiwa kuonwa na watu
kuanzia miaka 16 nakuendelea.
0 comments:
Post a Comment