Nafasi Ya Matangazo

July 29, 2013

Na Anne Kiruku,EANA Kukosekana kwa utashi wa kisiasa kwenye vita dhidi ya rushwa  katika Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) kunatokana na jinsi kampeni za uchaugzi wa kisiasa zinavyofadhiliwa.
Mkutano wa kanda uliofanyika mjini Kigali, Rwanda hivi karibuni umefafanua kwamba ufadhili huo umechochea upendeleo katika uteuzi wa nafasi mbalimbali za umma,utoaji wa tenda na mikataba mengine ya huduma katika jamii.

Washirika wa mkutano huo wamewataka viongozi wa EAC waongoze vita dhidi ya rushwa kwa kusimamia ipasavyo utawala bora na kuzingatia uwajibikaji, uwazi na utawala wa sheria na siyo maneno tupu bila vitendo.

 Mkutano hu pia umependekeza kuoanisha sheria zinazohusu vita dhidi ya rushwa katika kanda  hiyo na kujumuisha kipengele cha uwajibikaji wa kisiasa.

Athari hasi za rushwa mkutano uliambiwa ni kubwa zaidi kwa makundi yaliyo katika hali ya unyonge kama vile wanawake, watoto na masikini katika jamii.

''Ili kulifikia lengo la kuwa na Afrika Mashariki yenye mafanikio na umoja wa kisiasa, wadau wote hawanabudi kuzingatia utaratibu wa uwazi na uwajibikaji,'' wajumbe wa mkutano huo walifafanua katika mapendekezo yao ambayo Shirika Huru la Habari la Afrika Mashariki (EANA) lilipata nakala yake. 

Mkutano wa Nne wa Mwaka wa EAC juu ya utawala bora umewaleta pamoja wajumbe kutoka serikali za nchi wanachama na wadau binafsi wanaojihusisha na masuala ya kukuza utawala bora.

Mkutano huo ulioandaliwa na EAC umetoa jukwaa la majadiliano ya mambo muhimu yanayohusu utawala bora yanayogusa mwenendo mzima wa mtangamano wa jumuiya.Washiriki walibadilishana uzoefu na kupanga njia nzuri ya kukuza utawala bora na mtangamano wa kanda.

Wakati wa ufunguzi wa mkutano huo, Spika wa Bunge la Rwanda, Rose Mukantabana alikiri kwamba rushwa ni ''kansa kwa maendeleo ya kiuchumi.''

Alirudia kwamba rushwa inakandamiza demokrasia na kubeza utawala wa sheria.
Posted by MROKI On Monday, July 29, 2013 No comments

0 comments:

Post a Comment

  • Facebook
  • Twitter
  • Youtube

Labels

Blog Archive

Nafasi Ya Matangazo