Prof. Ibrahim Haruna Lipumba
Mwenyekiti wa Taifa CUF.
Chama Cha Wananchi (CUF) kimesikitishwa sana na vurugu
zilizotokea Mtwara tarehe 22 Mei 2013 na uvunjaji mkubwa wa haki za binadamu
uliofanywa na polisi tarehe 23 Mei 2013. Chimbuko la mgogoro wa gesi wa mikoa
ya Lindi na Mtwara ni kushindwa kwa serikali ya CCM kutekeleza ahadi zaka za
miradi ya kutumia gesi ya Msimbati na Mnazi Bay mkoani Mtwara na hasa ujenzi wa
kituo cha kufua umeme wa MW 300 na kuiunganisha Mtwara, Lindi na Ruvuma katika
gridi ya taifa.
CUF inalaani vikali vitendo vya kihalifu vya kuchomea
nyumba ya mwandishi wa habari wa Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC), Kassim
Mikongolo, na nyumba za baadhi ya viongozi wa CCM. Vile vile tunalaani vikali
vitendo vya kuhujumu miundombinu muhimu likiwemo daraja la Mikindani
linalounganisha Mkoa Mtwara na Mikoa ya Lindi, Pwani na Dar es Salaam.
CUF imesikitishwa sana na taarifa za vifo vya askari
wanne wa JWTZ kwa ajali ya gari iliyotokea Kilimahewa wakati askari hao wakisafirishwa
toka Nachingwea kwenda Mtwara kusaidia kudhibiti vurugu.Tumepeleka salamu za
pole kwa CDF Jenerali Mwamunyange na kupitia kwake kwa familia za marehemu.
Tunawapa pole askari wote waliojeruhiwa na kuwaombea kwa Mwenyezi Mungu wapone
haraka na waweze kurejea katika ulinzi wa taifa letu.
Vilevile tumesikitishwa na kifo cha raia wawili kwa
kupigwa risasi akiwemo mama mjamzito na raia wengi kujeruhiwa. Tunawapa pole
familia za marehemu na kuwaombea wote waloumia wapone haraka na waendelee na
shughuli zao.
Taarifa za vyombo vya habari vinaeleza kuwa ghasia
hizi zilianza baada ya hotuba ya bajeti ya Waziri wa Nishati na Madini
iliyosomwa katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kusisitiza ujenzi
wa bomba la kusafirisha gesi toka Mtwara kwenda Dar es Salaam.
Taarifa tulizozipata toka Mtwara zinaeleza kuwa jana kuanzia
asubuhi, wakati Waziri Nchimbi akisoma tamko la serikali bungeni kwa niaba ya
Waziri Mkuu kuwa hali ya Mtwara sasa ni shwari askari wa Jeshi la Polisi
walifanya vitendo vya kinyama kwa raia wasio na hatia.
Polisi walipita
katika nyumba za wananchi na kuwachomoa vijana, kuwapiga na kuwachukua
kuwapeleka kituo cha Polisi. Mabomu ya machozi na risasi za moto zilipigwa
hovyo hovyo.
Aidha katika maeneo ambayo vijana hawakuwepo
waliwapiga wake zao, watoto wadogo na hata wazee kwa madai kwamba vijana wao
wanasumbua. Binti mjamzito aitwae Fatuma alipigwa risasi na kufariki. Katika
eneo la Mkana Read, Polisi walichoma moto soko la wananchi, nyumba nyingi za
raia zimechomwa moto na polisi wamepora mali za watu zikiwemo za maduka ya
wafanyabiashara. Wananchi wengi wakiwemo wanawake wamelazimika kukimbia nyumba
zao. Taarifa tulizopata zinaeleza vitendo vya kinyama vya polisi vilisita baada
ya maafisa wa juu wa Jeshi la Polisi kufika Mtwara.
Vurugu zilizotokea Mtwara tarehe 22 Mei hazihalalishi
Jeshi la Polisi kupiga watu, kuua, kuchoma moto nyumba na vibanda vya biashara
na kupora mali za watu wasio na hatia. Vitendo hivi vya polisi kupora mali na
kuchoma vibanda vilitokea Tandahimba mwaka jana.
Weledi ndani ya Jeshi la Polisi uko chini sana.
Tunalaani vikali vitendo vya Jeshi la Polisi la kupiga watu, kuchoma nyumba na
kupora. Uongozi wa Jeshi la Polisi uchukue hatua za kinidhamu na kisheria dhidi
ya polisi waliohusika na vitendo hivyo. Tunatoa wito kwa asasi za haki za
binadamu na wanaotoa misaada ya kisheria kuwasaidia wahanga wa Mtwara kudai
haki zao.
Pamoja na kulaani vitendo hivi vya kihalifu na
kuchukua hatua za kisheria dhidi ya wale waliohusika na vitendo hivyo, Serikali
itafanya makosa makubwa na kuingiza nchi katika mgogoro wa muda mrefu na
wananchi wa mikoa ya kusini ikiwa itafumbia macho chimbuko la mgogoro huu na
kushikilia hoja nyepesi kuwa mgogoro huu ni matokeo ya uchochezi wa wanasiasa
wachache wanaojitafutia umaarufu.
Narudia Chimbuko la mgogoro wa gesi wa mikoa ya Lindi
na Mtwara ni kushindwa kwa serikali ya CCM kutekeleza ahadi za miradi ya
kutumia gesi ya Msimbati na Mnazi Bay mkoani Mtwara na hasa ujenzi wa kituo cha
kufua umeme wa MW 300 na kuiunganisha Mtwara, Lindi na Ruvuma katika gridi ya
taifa.
Mradi mwingine
ni kuanzisha kiwanda cha mbolea kitakachotumia gesi kama malighafi kama
ilivyopendekezwa na Wentworth resources wanaomiliki visima vya gesi ya Mnazi
Bay na Msimbati. Kama miradi hii ingeanza kutekelezwa nina uhakika wananchi
wengi wa mikoa ya kusini hawatapinga gesi ya ziada kusafirishwa Dar es Salaam.
Kauli ya Waziri Nchimbi Bungeni kuwa serikali
itawasaka waasisi wa vurugu hizi ndani na nje ya Mtwara ni juhudi za kutafuta
mchawi badala ya kutathmini kwa nini wananchi wa Mtwara hawaiamini kabisa
serikali ya CCM. Tumepata taarifa kuwa pana mpango kabambe wa kuwakamata
viongozi mbalimbali wa CUF na kuuaminisha umma kuwa wanaohusika na kuchochea,
kupanga na kutekeleza vurugu za Mtwara ni viongozi na wafuasi wa CUF.
Serikali ya CCM imekubuu katika kubambikia kesi nzito
watu wasiokuwa na hatia. CUF inafanya siasa kwa kujenga hoja. Katika suala la
gesi tumejenga hoja za kiuchumi na maendeleo na uwajibikaji wa kisiasa kuhusu
utekelezaji wa miradi ambayo CCM na serikali yake iliahidi kuitekeleza.
Viongozi wa CUF hawajachochea vurugu wametumia majukwaa ya mikutano ya hadhara
na maandamano ya amani kujenga hoja za kimsingi.
Mimi binafsi nilienda Mtwara mwaka jana nikazuwiwa
kufanya mkutano wa hadhara Mtwara mjini kwa madai kuwa hali siyo shwari wilaya
ya Tandahimba. Wananchi wa Mtwara walitaka nifanye mkutano huo pamoja na kuwa
umezuwiwa na polisi, nikawasihi tusifanye hivyo na wakakubali. Tarehe 14 Aprili
2013 nilikuwa Mtwara nikazuwiwa kufanya mkutano wa hadhara sikukaidi nikafanya
mkutano wa ndani. Maalim Seif, Katibu Mkuu wa CUF na Makamu wa Kwanza wa Rais
wa Zanzibar alitaka kufanya ziara ya mkoa wa Mtwara akaambiwa hana ruhusa ya
kufanya mikutano ya hadhara mkoa wa Mtwara na hivyo akasitisha ziara yake.
Kuwakamata viongozi wa CUF wa wilaya za Mtwara na
Lindi na wa kitaifa hakutamaliza mgogoro kati ya serikali na wananchi wa Mtwara
ikiwa serikali itaendelea kuwabeza, kuwadharau na kutowasikiliza. Badala yake itaongeza
chuki dhidi ya serikali.
Wakati wananchi wa Mtwara wamepoteza imani kwa uongozi
wa CCM na serikali yake, Serikali imezuia vyama vingine vya siasa na asasi za
kiraia kufanya shughuli za kuwasiliana na wananchi wa Mtwara na kwa hiyo
kuunyima umma miongozo ya kisiasa za demokrasia. Umma uliokata tamaa na
unaoamini unabezwa, kudharauliwa na kudanganywa na watawala unaweza kuchukua hatua
zenye madhara hata kwa maslahi yao wenyewe.
Serikali imekuwa inapotosha kwa makusudi madai ya
msingi ya wananchi wa Mtwara ambayo ni kuwa serikali itekeleze miradi ya gesi
iliyoahidi wananchi wa Mtwara. Badala yake wananchi wa mikoa mingine wanalishwa
sumu kuwa Wananchi wa Mtwara hawataki raslimali ya gesi iwanufaishe Watanzania
wengine. Umeme ukifuliwa Mtwara na kuunganishwa katika gridi ya taifa utatumiwa
na wote waliounganishwa na gridi ya taifa. Kiwanda cha mbolea cha Mtwara
kitazalisha mbolea itakayotumiwa nchi nzima. Wananchi wa Mtwara hawajasema
Watanzania wengine hawana haki ya kwenda Mtwara kupata ajira au kufanya
shughuli za kibiashara.
Wanaobomoa
umoja na mshikamano wa kitaifa ni wale wanaowabeza, kuwadharau na kuendelea
kuwadanganya wananchi wa Mtwara na kupandikiza sumu kwa Watanzania wengine kwa
kupotosha madai ya msingi ya wananchi wa Mtwara na kushindwa kwa serikali
kuwajibika kisiasa kwa ahadi ambazo viongozi akiwemo Rais alizitoa kwa wananchi
wa Mtwara.
Wananchi wa Mtwara zaidi ya elfu 24 wameweka sahihi na
kupeleka ombi (petition) kupitia Mhe. Habibu Mnyaa, Mbunge wa Mkanyageni
kujadili kutekelezwa kwa miradi ya gesi ya Mtwara. Spika Anna Makinda kazuwia
ombi hilo kujadiliwa.
Bunge limeshindwa kuisimamia serikali na kuhoji kwa
nini mradi wa kufua umeme MW 300 ambao katika mwaka wa bajeti wa 2011/12
ulitengewa na kutumia shilingi 540 milioni umesitishwa. Mpaka hivi sasa hakuna
kamati ya Bunge iliyoenda kusikiliza kilio cha Wananchi wa Mtwara badala yake
Spika amekuwa mstari wa mbele kuunga mkono vitendo vya serikali badala ya
kuhakikisha kuwa Bunge linaisisimamia serikali.
Katika hotuba ya bajeti ya mwaka huu, Waziri kaeleza
serikali kupitia TANESCO kwa kwa kushirikiana na kampuni ya Symbion itajenga
kituo cha kufua umeme cha MW 400 na kuunganisha Mtwara na gridi ya taifa
kupitia Songea.
Hata hivyo bajeti ya maendeleo haijautaja mradi huu
wala kutenga hata shilingi 1 kwenye mradi. Wananchi wa Mtwara wanaona
wanaendelea kudanganywa na serikali ya CCM. Mikogo, majigambo na kauli za
kejeli za Waziri wa Nishati kuhusu uelewa mdogo wa wananchi wa Mtwara katika
masuala ya gesi zinazidi kuongeza chuki na jazba za wananchi.
Mpaka hivi sasa serikali imekataa kuweka wazi mkataba
wa ujenzi wa bomba na upembuzi yakinifu wa mradi huu. Hotuba ya bajeti ya
Waziri wa Nishati haielezi kama Wentworth Resources wanaoendesha visima vya
gesi wataweza kuzalisha gesi kukidhi ukubwa wa bomba la kusafirisha gesi kutoka
Mtwara kwenda Dar es Salaam na ahadi mpya za miradi ya kutumia gesi mkoani
Mtwara.
Linalonistusha na kunitisha ni kwa nini viongozi wa
juu wa serikali hawataki kuwa wawazi kuhusu mradi huu na wako tayari kupotosha,
kuwagawa wananchi na kudanganya alimuradi mradi huu utekelezwe na usihojiwe?
Gesi ya Mnazi Bay, Mtwara iligunduliwa toka mwaka 1982
lakini mpaka hivi sasa haijatumiwa kikamilifu. Kampuni ya Artumas ilianza
utaratibu wa kuichimba gesi mwaka 2006 na kuitumia kufua umeme wa Megawati 18.
Tarehe 17 Oktoba 2007 kampuni ya Artumas ilitoa taarifa ya mpango wake wa
kujenga kituo cha kufua umeme wa MW 300. Mpango huu ulitarajiwa kugharamiwa
toka Mfuko wa Maendeleo wa Uholanzi - Netherlands Development Finance Company.
Gharama za mradi wa kufua umeme zilikadiriwa kuwa dola za Marekani 225.
Kampuni maalum ya kuendesha mradi huu ya Tanzania
Generation Company Ltd (TANGEN) ilisajiliwa ili kujenga na kuendesha mradi huu.
Kampuni hii ingekopa dola milioni 160 na dola milioni 65 zingechangiwa kama
hisa na kampuni nyingine zikiwemo mifuko ya pensheni ya Tanzania na kampuni ya
madini ya Barrick International.
Kampuni nyingine maalum ilitarajiwa kuanzishwa ili
ijenge msongo wa umeme (nguzo za nyaya za kusambaza umeme) na kuunganisha umeme
wa Mnazi Bay kwenye gridi ya taifa. Mradi huu ungegharimu dola milioni 400.
Mradi huu ulitarajiwa kugharamiwa na mifuko ya pensheni ya Tanzania na
wawekezaji kutoka Mashariki ya Kati. Mpango huu ulikubaliwa na serikali na
ukaingizwa katika Mpango Kabambe wa Taifa wa kufua na kusambaza umeme (National
Power Development Master Plan). Mradi huu wa kufua umeme MW 300 Mtwara
ulipangwa uwe umekamilika mwaka wa 2012. Tovuti ya Tanesco inaueleza mpango huu
kuwa ni wa muda wa kati. Bila shaka serikali iliukabali mradi huu baada ya
kuufanyia utafiti na upembuzi yakinifu.
Mtikisiko wa sekta ya fedha na uchumi wa dunia wa
mwaka 2008 uliathiri kampuni ya Artumas. Thamani ya hisa moja ya Artumas
iliporomoka toka dola za Marekani 10.80 mwezi wa Aprili 2008 na kufikia dola
0.12 mwezi wa Machi 2009. Kampuni ilipata matatizo makubwa ya ukata na ilibidi
serikali iisaidie dola milioni 7 ili iweze kuendelea na ufuaji wa umeme wa MW
18 Mtwara. Barrick International ilijitoa katika mradi wa TANGEN. Katika
kujiunda upya Kampuni ya Artumas Group Inc. iliamua kubadilisha jina lake na
kuwa Wentworth Resources Limited na kuteua menejimenti mpya.
Tarehe 10 Juni 2009 Rais Kikwete alipokuwa
anawahutubia Wabunge na Wananchi katika Ukumbi wa Kilimani Dodoma kuhusu athari
za mtikisiko wa uchumi duniani alieleza “Kwa sababu ya matatizo ya uchumi
uwekezaji wa vitega uchumi kutoka nje umepungua.
Wawekezaji wamekuwa wanakosa fedha kutoka mabenki na
masoko ya mitaji. Matokeo yake ni kuchelewa au kukosa kabisa au kuahirishwa
miradi mikubwa ambayo ingetoa mchango muhimu kwa ukuaji wa uchumi wetu na
ajira. Kwa mfano: Mradi wa umeme wa MW 300 kule Mtwara kwa sababu ya Barrick
Gold Ltd. kujitoa na Artumas peke yake haina uwezo wa kifedha; mradi wa nickel
Kabanga, mradi wa aluminium smelter, Mtwara; mradi wa usambazaji umeme mkoani
Mtwara, miradi ya viwanda vya saruji na mbolea Mtwara.”
Kwa kauli ya
Rais ambayo wananchi wa Mtwara na Watanzania kwa ujumla waliisikia kwani hotuba
hii ilirushwa live na Shirika la Utangazaji la Tanzania – Radio na Televisheni
na vyombo vingine vya habari.
Miradi ya
kutumia gesi ni pamoja na kufua umeme MW 300, kutengeneza mbolea inayotumia
gesi kama malighafi, aluminium smelter inayohitaji umeme mwingi, na kiwanda cha
saruji ambacho kinatumia umeme na kinu chake kinaweza kutumia gesi. Wananchi
wakamuamini Rais wetu na wakaelewa kuwa miradi hii imekwama kwa sababu ya
mtikisiko wa uchumi na kwamba serikali inajitahidi kutafuta njia mbadala ya
kujikwamua ili miradi hiyo iendelee.
Wakati wa kampeni ya uchaguzi wa 2010, Rais Kikwete
aliwaeleza wananchi wa Mtwara akichaguliwa ataendeleza miradi ya Mtwara
itakayotumia gesi ya Mnazi Bay. Maelezo ya Ilani ya CCM ya Uchaguzi wa 2010,
ibara ya 63 kifungu (j) Kuzalisha umeme (300MW) kutokana na gesi asili ya Mnazi
Bay (k) Kupanua mitambo ya kusafisha gesi na bomba la kusafirisha gesi kutoka
Songo Songo hadi Dar es Salaam.
Mitambo ya kufua umeme ya Dar es Salaam ilitegemewa
itumie gesi ya Songosongo kwani bomba la kutoka Songosongo hadi Somanga mpaka
Dar es Salaam lingepanuliwa. Toka mwaka 2010 kampuni ya Globeleq- Songas
ilijiandaa kutekeleza mradi wa kuongeza uwezo wa bomba la gesi kutoka
Songosongo – Somanga – Dar es Salaam ili likidhi mahitaji ya gesi ya vituo vya
kufua umeme Dar es Salaam kikiwemo kituo cha Kinyerezi. Serikali iliisitisha
kampuni hiyo isiendelee na mradi huo ambao hivi sasa ungekuwa umekamilika na
kuongeza uwezo wa kufua umeme kwa kutumia gesi kwa alau MW 200.
Rais Kikwete alipoenda Mtwara kuhudhuria sherehe ya
Mashujaa tarehe 25 Julai 2011 alizungumza na wananchi wa Mtwara na kueleza
miradi ya maendeleo itakayotekelezwa kwa kutumia gesi ya Mnazi Bay ikiwemo
ufuaji wa umeme wa MW 300 na kupanua bandari ya Mtwara.
Tarehe 12 Oktoba 2011, Ikulu ilitoa taarifa kwa vyombo
vya habari kuwa “Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya
Mrisho Kikwete leo, Jumatano, Oktoba 12, 2011, amepokea ripoti kutoka makampuni
mawili ya kimataifa kuhusu Mpango Kabambe ya mradi mkubwa wa umeme ambao
utaunganisha kwenye Gridi ya Taifa mikoa yote sita ambayo kwa sasa haiko kwenye
gridi hiyo. Rais Kikwete amepokea ripoti hiyo kutoka makampuni ya China
National Machinery&Equipment Import&Export Corporation (CMEC) ya China
na Siemens ya Ujerumani ambayo kwa pamoja yanatarajia kujenga kituo kikubwa cha
kuzalisha umeme kutokana na gesi katika eneo la Mnazi Bay, mjini Mtwara na pia
kujenga njia ya kusafirisha umeme ya kilomita 1,100 kutoka Mtwara hadi Singida.
Mradi huo mkubwa wa umeme wa megawati 300 utakaogharimu karibu dola za Marekani
milioni 684 na utakaozalisha umeme wa moja kwa moja na wenye nguvu kubwa ya 300
kV (300 kV High Voltage Direct Current – HVDC) utagharimiwa kwa pamoja na mkopo
kutoka Benki ya Exim ya China na Serikali ya Tanzania.”
Mikoa sita ambayo bado haijaunganishwa na gridi ya
taifa ni Lindi, Mtwara, Ruvuma, Rukwa, Kigoma na Kagera. Mradi huu pamoja na
kufua umeme wa MW 300 Mtwara ungekamilisha kuunganisha mikoa yote ya Tanzania
kwenye gridi ya taifa. Taarifa iliendelea kueleza “Kuunganisha mikoa yote ya
Tanzania kwenye Gridi ya Taifa ilikuwa moja ya ahadi kubwa zilizotolewa na
Serikali ya Rais Kikwete wakati anaingia maradakani na kwa kuuunganisha mikoa
hiyo sita kwenye Gridi hiyo, Serikali hiyo itakuwa imetimimiza ahadi hiyo.”
Maelezo haya yametolewa na Ikulu na vyombo vya habari
vikayatangaza na wananchi wa Mtwara wakasikia. Kutekeleza mradi wa kufua umeme
kutaifanya Mtwara iwe na umeme wa kutosha kushawishi kampuni kuanzisha viwanda
hasa ukizingatia ahadi ya Rais Kikwete ya kupanua bandari ya Mtwara. Mwaka wa
fedha wa 2011/12 serikali ilitenga na kutumia shilingi 540 milioni fedha za
maendeleo za mradi wa Mnazi Bay 300MW Development Project. Baada ya hapo mradi
huu haukutengewa fedha tena. Badala ya mradi huu kuendelezwa kama Rais
alivyowaahidi wananchi wa Mtwara na Watanzania kwa ujumla badala yake wanasikia
serikali imezindua mradi wa kujenga bomba la kusafirisha gesi toka Mtwara kuja
Dar es Salaam.
Kwa taarifa ya Ikulu gharama za mradi wa kufua umeme
wa MW 300 Mtwara na kuiunganisha mikoa sita katika gridi ya taifa gharama yake
ni dola milioni 684. Mradi wa kutandaza bomba la gesi unagharimiwa na mkopo wa
dola milioni 1220 kutoka Benki ya Export Import Bank ya China. Ni wazi gharama
za kufua umeme Mtwara na kuunganisha mikoa sita kwenye gridi ya taifa ni ndogo
zaidi kuliko gharama za kutandaza bomba la gesi.
Msongo wa umeme za kV 400 unajengwa kuunganisha Iringa
– Dodoma – Singida na Shinyanga. Mradi huu unatekelezwa na Benki ya Maendeleo
ya Afrika. Nyaraka ya mradi unaonyesha gharama za kujenga umeme za kV 400 ni
dola za Marekani 600,000 kwa kilomita 1.
Gharama za kujenga bomba la gesi lenye kipenyo (upana wa nchi 36) ni dola
1,309,636 kwa kilomita 1. Kwa madhumuni ya kufua umeme, gharama ya kujenga
bomba la gesi ni zaidi ya mara mbili ya gharama za kunganisha Mtwara na Dar es
Salaam. Isitoshe unaweza kuongeza ufuaji wa umeme Mtwara na kusamabaza kwa
msongo huo huo.
Ujenzi wa bomba la Dar es Salaam Mtwara umeanza bila
kuwa na mipango ya kuhakikisha kuwa kutakuwepo na gesi ya kutosha kuisafirisha
hadi Dar es Salaam. Bomba hili litakuwa na uwezo wa kusafirisha futi za ujazo
bilioni 200. Uwezo wa gesi ya Mnazi Bay na Msimbati kwa hivi sasa ni futi za
ujazo bilioni 80. Hakuna mpango unaoeleweka wa kupata futi za ujazo bilioni 120
ili bomba la gesi liweze kutumiwa kikamilifu.
Mpaka hivi sasa gesi kiasi cha futi za ujazo trilioni
33.7 imegunduliwa katika bahari yenye kina kirefu. Uchimbaji wa gesi hii bado
haujaanza. Inaweza kuchukukua miaka 7 – 10 kabla ya shughuli ya uchimbaji wa
gesi kukamilika. Kampuni zilizogundua gesi bahari kuu bado hazijafanya uamuzi
wa utaratibu wa kuichimba na kuisafirisha gesi hadi nchi kavu. Kwa kuwa gharama
za kujenga bomba la gesi chini ya bahari ni za juu sana, kampuni hizi
zitapendelea kutandaza bomba kwenda nchi kavu kwenye eneo lililo fupi kuliko
yote.
Statoil imegundua gesi nyingi eneo la Zafarani bahari
kuu eneo la mkoa wa Lindi. Hivi sasa wanatazama maeneo ya Kilwa kuweza kuweka
kituo cha nchi kavu. Bandari ya Lushungu kata ya Limalyao, wilaya ya Kilwa
ambayo ina kina kirefu cha bahari yaelekea kuwavutia. Kwa hivi sasa hakuna
uhakika gesi iliyogunduliwa bahari kuu itapelekwa Mtwara. Uamuzi wa kujenga
bomba kubwa umefanywa haraka haraka bila kutathmini kikamilifu faida zake
kiuchumi. Jambo la kujiuliza kwa nini uamuzi huu umechukuliwa na kuacha
kutekeleza mradi wa kufua umeme Mtwara wenye mantiki kiuchumi, kijamii na
uwajibikaji wa kisiasa?
Wentworth Resources wamefanya upembuzi yakinifu
(feasibility study) na kubaini kwamba njia nzuri ya kibiashara na kiuchumi ya
kutumia gas wanayoweza kuzalisha Mnazi bay hivi sasa ni kuanzisha kiwanda cha
kutengeneza mbolea na kemikali nyingine Mtwara. Kiwanda cha mbolea chenye faida
kubwa kinaweza kuanzishwa na kuendeshwa hata kama akiba ya gesi iliyogunduliwa
siyo kubwa sana kama ilivyo Mnazi Bay. Mradi wa kujenga kiwanda unaweza
kukamilishwa kwa muda mfupi. Pamoja na mbolea kiwanda kitazalisha methanol
yenye soko kubwa duniani. Kiwanda kitatumia hewa ukaa (carbondioxide) na kwa
hiyo kuweza kupata fidia ya kuboresha mazingira. Uongozi wa Wentworth Resources
una uzoefu wa miaka mingi katika miradi ya kutumia gesi. Wanajua wanalolieleza.
Hata hivyo serikali imewamrisha kupeleka gesi watakayozalisha kwenye bomba la
gesi la kwenda Dar es Salaam.
Serikali imeanzisha mgogoro wa gesi kwa kuanza
kutekeleza mradi mkubwa wa kutandaza bomba la mafuta na kuacha miradi yenye
manufaa makubwa kiuchumi na kijamii kwa taifa letu. Uchunguzi huru na wa kina
ufanyike kubaini sababu za serikali kuacha miradi ya kutumia gesi Mtwara na
kukumbatia mradi wa kutandaza bomba. Ripoti aliyopewa Rais ya mradi wa kufua
umeme Mtwara na kuunganisha mikoa 6 katika gridi ya taifa itolewe ili
Watanzania waweze kuelewa mantiki ya mradi huu. Mkataba wa mkopo na utekelezaji
wa mradi wa kutandaza bomba la gesi uwekwe wazi. Serikali iruhusu kampuni ya
Wentworth resources kuendelea na mradi wa kiwanda cha mbolea. Rais aende Mtwara
kuwaeleza wananchi kuwa ahadi alizoeleza za kutumia gesi Mtwara zitatekelezwa.
Vyama vya siasa na asasi za kiraia viruhusiwe kufanya
mikutano ya hadhara kueleza njia za kidemokrasia za kudai haki za kiuchumi za
wananchi wa Mtwara. Bunge liunde kamati teule ya kuchunguza kwa nini Mradi wa
Kufua umeme MW 300 umesitishwa na serikali, upembuzi yakinifu wa mradi wa bomba
la gesi na mikataba yote inayohusiana na mradi huu.
Sakata hili la gesi ya Mtwara linaonyesha wazi kuwa
hatuna sera muafaka na mkakati wa kuendeleza sekta ya gesi kwa manufaa ya taifa
letu na Wananchi wa kawaida. Badala ya gesi kuwa neema inaelekea kuwa itakuwa
balaa na laana. Sera ya gesi inapaswa kuweka taratibu zitakazohakikisha kuwepo
kwa uwekezaji wa kutosha katika sekta hii na utakaolinufaisha taifa letu bila
kuathiri motisha kwa wawekezaji wenye teknolojia ya kutafuta na kuchimba gesi.
Wananchi wa Mtwara wanahitaji kushirikishwa. Serikali iwe wazi na kutoa taarifa
sahihi kuhusu miradi ya gesi.
Prof. Ibrahim Haruna Lipumba
Mwenyekiti wa Taifa, Mei 24 2013
0 comments:
Post a Comment