CHAMA
cha Waandishi wa Habari za Michezo Tanzania (TASWA) kinasikitika
kuwajulisha wadau wake kuwa bonanza la wanahabari lililopangwa kufanyika
kesho viwanja vya Sigara (TCC) Chang’ombe sasa litafanyika viwanja vya
Leaders Klabu, Kinondoni Dar es Salaam siku hiyo hiyo ya Aprili 6,2013.
Uamuzi
huo wa kushtukiza umefikiwa kwenye kikao cha dharura kilichofanyika
jana usiku kati ya TASWA ambao ni waandaaji na wadhamini wa bonanza hilo
Kampuni ya Bia Tanzania (TBL) kutokana na kushindwa kuafikiana baadhi
ya mambo na menejimenti ya viwanja hivyo.
Tunawaomba
sana radhi wanahabari kwa usumbufu mkubwa ambao wataupata kutokana na
mabadiliko haya, lakini tunaamini yamefanyika kwa dhamira nzuri yenye
nia ya kuboresha bonanza letu na kwa kiasi kikubwa litafana kwa asimilia
100.
Dhamira ya TASWA ni
kuona inakuwa na bonanza zuri lisilokuwa na aina yoyote ya kwikwi,
hivyo tayari tumeshamalizana na menejimenti ya viwanja vya Leaders Klabu
na kila kitu kitakuwa safi kuliko maelezo.
Pia
tunaishukuru menejimenti ya viwanja vya Sigara kwa ushirikiano iliotupa
kwa nia ya kufanya bonanza hilo eneo lao, ingawa ndoto zetu
hazikutumia, lakini tunaamini siku za usoni tunaweza kufanya nao kazi.
Tunasisitiza
lengo la bonanza letu ambalo mgeni rasmi atakuwa Waziri wa Uchukuzi,
Dk. Harrison Mwakyembe ni kuwaweka pamoja waandishi wote wa habari bila
kujali ni wa siasa, michezo, uchumi, afya na mambo mengine pamoja na
wafanyakazi wa vyombo mbalimbali vya habari, ili kubadilishana mawazo na
kufurahi pamoja.
Awali
bonanza letu ilikuwa lifanyike Leaders Klabu, lakini tulilihamishia
viwanja vya Sigara kutokana na wadau wengi kuomba wapate nafasi ya
kwenda kutazama mechi ya Kombe la Shirikisho kati ya Azam ya Tanzania na
Barrack Young Controllers ya Liberia kesho. Hata hivyo tunaamini
wahariri wa habari za michezo watajipanga vizuri kulingana na mabadiliko
hayo na hakuna litakaloharibika.
Pia
katika kuboresha bonanza hilo litakalotumbuizwa na bendi ya Extra Bongo
na kundi la taarabu la Jahazi Modern, kutafanyika mchezo wa soka kati
ya wanahabari ambao wameoa na wale ambao hawajaoa utakaofanyika baada ya
michezo ya kawaida baina ya vyombo vya habari kumalizika.
Bonanza
litaanza saa tatu asubuhi kwa washiriki kucheza michezo mbalimbali
ikiwemo soka, netiboli, wavu, kuruka kichura, aina mbalimbali za riadha,
kuvuta kamba na kucheza muziki. Bonanza litamalizika saa moja usiku.
Ahsanteni.
Amir Mhando
Katibu Mkuu TASWA
05/04/2013
0 comments:
Post a Comment